Mwagala News

Kitaifa, Kimataifa, Siasa, Michezo na Burudani

Latest Post

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam leo Jumatatu, Januari 22, 2018 imemhukumu mwalimu wa sanaa ya kujihami, ‘Martial Arts’ na msanii wa filamu za Kibongo, Salum Njwete maarufu Scorpion miaka saba jela kwa kosa la kumjeruhi na kumtoboa macho kinyozi, Said Mrisho, pia mahakama imemtaka kulipa faini ya Sh. milioni 30 kwa ajili ya fidia kwa majeruhi huyo.
Tokeo la picha la HUKUMU YA SCORPION
Kwa upande wake, mlalamikaji katika kesi hiyo Mrisho amelia mahakamani hapo akidai adhabu aliyopewa Scorpion haitoshi ikilinganishwa na kosa alilotenda huku akieleza kuwa atakwenda kwa Rais Dkt. John Magufuli kumueleza masikitiko yake.

“Sijaridhika na hii hukumu, huyu mtu amenitoboa macho nimekuwa kipofu, amenitia kilema cha maisha siwezi kufanya tena kazi zangu za kuniingizia kipato, nina watoto walikuwa wanasoma shule nzuri sasa hivi wanakwenda kuteseka, hata kama nikilipwa hiyo fidia ya Milioni 30 itanisaidia kitu gani?  Nitakwenda kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda anipeleke kwa Rais Magufuli ili nikamueleze haya aweze kunisaidia,” alisema Mrisho.

Njwete alikuwa akikabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni  unyang’anyi wa kutumia silaha na kumjeruhi Mrisho kwa kumchoma kisu sehemu mbalimbali za mwili zikiwemo tumboni na mabegani na kisha kumtoboa macho, kitendo anachodaiwa kutenda Septemba 6, mwaka juzi  katika eneo  la Buguruni Shell, jijini Dar es Salaam. Pia, anadaiwa kumwibia mali yenye thamani ya Sh 476,000/-.

Kesi hiyo imeamriwa na Hakimu Flora Haule ambapo wakili wa serikali alikuwa ni Hussein Hitu kwa niaba ya Juma Nassoro.  Wakili wa upande wa utetezi alikuwa Frank Tawale kwa niaba ya Nassoro Katuga.


Picha inayohusiana

Na Mwandishi Wetu.

Watanzania wametakiwa kuenzi sanaa na utamaduni waliona kwa ajili ya kizazi kijacho ili kukijendea uzalendo wa kupenda nchi yao.

Hayo yamesema na Mkurugenzi wa Tamasha la Sauti za Busara, Yusuf Mahmoud wakati akielezea ujio wa Tamasha la 15 linalotarajiwa kufanyika Ngome Kongwe, Unguja - Zanzibar kwa kushirikisha wanamuziki na vikundi mbali mbali vya sanaa kutoka pande zote za bara  la Afrika na Ulaya.

“Katika Tamasha hili, ni sehemu ambapo watu wenye weledi wa sanaa mbalimbali hukutana, kuanzia kwa wakurugenzi wa matamasha mpaka kwa wazalishaji wa muziki, mameneja wa wanamuziki, wasambazaji wa muziki, wote hawa huja hapa Zanzibar mwezi Februari kuja kushuhudia utamu wa midundo ya muziki wa Ukanda wa Afrika Mashariki,” anasema Mkurugenzi wa Tamasha la Sauti za Busara, Yusuf Mahmoud.

Anaongeza kuwa, “Hili siyo tu tukio ambalo watumbuizaji wa Tamasha pekee huhudhuria, bali hata baadhi ya wanamuziki ambao hawapo katika orodha ya kutumbuiza huja kwa minajili ya kujifunza kutoka kwa wale wanaofanya maonesho mbalimbali, na pia hupata fursa ya kufahamiana na wadau muhimu wa tasnia yao na kutengeneza mahusiano ya kikazi kwa miezi ijayo, hata zaidi ya hapo baada ya tamasha kuisha.”  

Likisifika kuwa miongoni mwa matamasha yanayoheshimika, Sauti za Busara likiwa na kauli mbiu ya “Kuunganishwa na Muziki” kwa mwaka huu, linawakutanisha pamoja zaidi ya wanamuziki 460 katika visiwa vya Zanzibar.

Likiwa ni tamasha ambalo limeshuhudia ukuaji mkubwa katika uadhimishwaji wake na mwaka huu ukiwa wa 15, Tamasha hili linavutia wataalamu wa habari na muziki kutoka katika kila pembe ya Afrika, Ulaya na mahali pengine, ambapo hutoa jukwaa la kipekee kwa wanamuziki wa Afrika Mashariki kuutanganza muziki wao duniani.

“Kila mwaka, kila mwanamuziki anayepata fursa ya kutumbuiza katika jukwaa la Sauti za Busara, hualikwa kuzunguka katika miji mbalimbali duniani na kufanya maonesho kwenye matamasha yanayofanyika katika nchi hizo. Wanamuziki ambao hupata fursa ya kualikwa aghalabu, ni wale ambao wamethibitika katika maonesho yao kuwa wabunifu, wenye kuzungumza ujumbe fulani, na wanaocheza muziki wenye utambulisho fulani,” anasema Yusuf, akiwataja Msafiri Zawose, Jagwa Music, Leo Mkanyia, Tausi Women’s Taarab na Maulidi ya Homu ya Mtendeni kama mifano ya vikundi vya Kitanzania ambavyo tayari vimekwishaitwa katika safari za kimataifa baada ya kuonekana katika Tamasha la Sauti za Busara.  

Kulingana na maelezo ya Mkurugenzi wa Tamasha la Sauti za Busara, Yusuf  Mahmoud, Tamasha la Sauti za Busara ni fursa adhimu ambayo wanamuziki kutoka Tanzania hawatakiwi kukosa, kwa kuwa fursa kama hizi ni chache na ngumu kuzipata ndani ya Afrika.  

“Watu wa rangi tofauti huungana kwa pamoja kusheherekea muziki wa Kiafrika. Matarajio na msisimko ni mkubwa, hoteli zinazopatikana Stone Town huwa zinajaa katika wiki ya tamasha zikiwahudumia watu wanaotoka katika kila kona ya Tanzania, Afrika na Ulaya,” anasema Yusuf.

Kwa makadirio ya haraka, tamasha linachangia kiasi cha Dola za Marekani 7 milioni katika uchumi kila mwaka, kikiwa ni kipindi cha mavuno kwa biashara nyingi zinazofanyika kwenye kila pembe ya Zanzibar na sehemu zingine, na kulifanya Tamasha la Sauti za Busara kuwa zaidi ya ‘Tamasha la Muziki’. 

Hata hivyo, licha ya kuwa na mafanikio hayo yote, lakini changamoto kubwa inayolikumba tamasha hili ni ufadhili, na ndiyo sababu hata tamasha la mwaka 2016 lilifutwa na kusababisha hasara kubwa sana kwa biashara nyingi visiwani Zanzibar.

“Tunaendelea kutegemea fedha za wafadhili kutoka katika balozi mbalimbali, ambapo balozi za Norway na Uswisi zikiwa miongoni mwa wafadhili wakubwa, zikisaidia mafunzo na jitihada za ujengaji uwezo,” anasema Mkurugenzi wa Tamasha la Sauti za Busara, Yusuf Mahmoud.

Tamasha la Sauti za Busara 2018 linafadhiliwa na Ubalozi wa Norway, Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania na Zambia, Africalia, Mozeti, Zanlink, Memories of Zanzibar, Zenj FM, Chuchu FM, Tifu TV, Music In Africa, Ikala Zanzibar Stone Town Lodge, Emerson Zanzibar, Coastal Aviation, 2Tech Security, Ubalozi wa Ujerumani, Golden Tulip Dar City Centre.

Wakati kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo ya Kinondoni na Siha, zikianza kwa vitimbi, mgombea wa CCM, Maulid Mtulia amewekewa pingamizi lenye vipengele vitano.

Uchaguzi huo utakaoshirikisha vyama 12, utafanyika Februari 17 huku ukitarajiwa kuwa na mpambano mkali baina ya CCM na Chadema inayoungwa mkono na vyama vitano vya Ukawa ambavyo NLD, NCCR-Mageuzi, CUF ya upande wa Maalim Seif Sharif Hamad na Chaumma iliyojiunga hivi karibuni.

Uchaguzi huo unafanyika baada ya waliokuwa wabunge, Godwin Mollel (Siha, Chadema) na Maulid Mtulia (Kinondoni, CUF) kujivua uanachama kwa maelezo kuwa wanamuunga mkono Rais John Magufuli na baadaye kujiunga na CCM.

Chama hicho tawala kimewapitisha wawili hao kutetea majimbo hayo bila ya kuendesha mchakato wa ndani.

Kwa staili kama hiyo, Chadema imemsimamisha Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu katika jimbo la Kinondoni na Elvis Mosi (Siha).

Tayari CCM katika jimbo la Siha na CUF upande wa mwenyekiti anayetambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba wamezindua kampeni jana.

Wagombea walirejesha fomu juzi katika ofisi ya jimbo la iliyopo Magomeni.

Lakini saa chache kabla ya kuanza kampeni, Mwalimu aliwasilisha pingamizi dhidi ya mgombea wa CCM, akiwa na hoja tano, ikiwemo ya kutofanya mrejesho wa gharama za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Wakili wake, Frederick  Kihwelo amesema  kuwa kwanza, Mtulia  hajafanya mrejesho wa gharama za uchaguzi wa mwaka 2015, alipogombea kwa tiketi ya CUF.

“Jambo hili hufanywa na mtu yeyote aliyegombea nafasi ya udiwani, ubunge na urais na haijalishi kama alishinda au kushindwa,” alisema Kihwelo.

“Unapaswa kuandaa mchanganuo wa gharama zako za uchaguzi na kuzipeleka ofisi ya NEC.”

Alisema hoja ya pili ni Mtulia kushindwa kukidhi matakwa ya kisheria kwa kutojaza kwa usahihi fomu zake, kwa madai kuwa zimepigwa muhuri wa katibu wa CCM badala ya muhuri wa chama hicho tawala.

“Muhuli ulipigwa katika fomu yake unasomeka wa katibu wa chama badala ya muhuri wa chama. Hii inaonyesha chama hakijamthibitisha kugombea. Jambo hili liliwasumbua sana Chadema mwaka 2014 kwa baadhi ya wagombea wao kuenguliwa, ” alisema Kihwelo.

Alisema hoja ya mwisho ni Mtulia kujaza fomu akieleza kuwa anajishughulisha na kilimo cha mbogamboga, jambo ambalo Kihwelo amesema si kweli.

“Hiki kilimo cha mbogamboga amekianza lini kwa sababu tunajua alikuwa mbunge. Tunamtaka athibitishe hili,” alisema.

Msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa Kinondoni, Latifa Almasi alisema wamepokea mapingamizi lakini haweka wazi idadi yake, na kubainisha kuwa leo msimamizi mkuu wa uchaguzi huo, Aron Kagurumjuli, atayatolea ufafanuzi

MBUNGE wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga wamefikishwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya leo Jumatatu, Januari 22, 2018 kusikiliza kesi inayomkabili  ya kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.

Sugu na Masonga walifikishwa mahakamani hapo Ijumaa iliyopita Januari 19, 2018 lakini  mahakama ilizuia dhamana zao na kuwarejesha rumande hadi leo ambapo hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo, Michael Mteite alitoa uamuzi huo na kwamba kesi hiyo inatakiwa isikilizwe mfululizo kwa muda mfupi huku washtakiwa wakiwa wanafika mahakamani hapo wakitokea mahabusu.

“Mahakama hii inataka kusikiliza kesi hii kwa muda mfupi sana, ndani ya wiki moja kuanzia Jumatatu ijayo (leo)  iwe imeamuriwa, hivyo washtakiwa wataendelea kuwekwa mahabusu,” amesema Mteite.

Sugu na Masonga wameshtakiwa kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli ambayo waliyatoa katika mkutano wa hadhara walioufanya Desemba 30 mwaka jana katika viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya wakati wakiwahutubia wananchi.

NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, RUVU

KAMATI ya Bunge ya Maji, Mifugo na Kilimo, imeipongeza Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka, (DAWASCO), kwa kazi nzuri ya usimamizi wa miradi ya uboreshaji wa huduma za ugawaji na usambazaji maji  katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Akizungumza kwenye majumuisho ya ziara ya kamati hiyo baada ya kutembelea miradi inayotekelezwa na kusimamiwa na DAWASA na DAWASCO Dar es Salaami na mkoa wa Pwani leo Januari 20, 2018, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe.Emmanuel Papian, alisema. Kazi iliyofanyika ni kubwa na Kamati imeona jinsi gani fedha za serikali zimetumika.

Hata hivyo Mwenyekiti huyo alisema, miradi mingi inatekelezwa kwa fedha za mkopo  kutoka India, lakini Kamati imebaini kuwa kila kitu kinafanywa na makampuni ya kutoka India, jambo ambalo sio sahihi sana.
“Inawezekana kuna mahali ambapo tumezidiwa, au kujichanganya, na kama ni kwenye component ya huo mkopo iliandikwa, kuna jambo la kuangalia na kujadili.” Alisema Mhe. Papian.

Aidha Mhe. Papian alisema Kamati inashauri kuwa watendaji wa ndani (Wakandarasi) wanapomaliza hii miradi basi vijana wa Kitanzania lazima wawe wameshajua na kufundishwa na wajifunze kila kitu ili waweze kuendesha miradi hii kikamilifu.
Ziara ya Kamati hiyo ilianzia makao makuu ya DAWASA, ambapo Kamati ilipokea taarifa ya utendaji ya DAWASA na DAWASCO, na kasha walipata fursa ya kutembeela baadhi ya miradi hiyo ambayo ni ujenzi wa matenki makubwa ya kuhifadhia maji ya Changanyikeni, Salasala, vituo vya kusukuma maji vya Makongo na Salasala.
Kamati pia ilitembelea eneo la utandazaji mabomba ya kusambaza maji huko Mpiji Machimbo na kumalizia ziara yao kwa kutembelea mitambo ya maji ya Ruvu chini na Ruvu Juu.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Romanus Mwangi’ngo alisema, Mradi wa uboreshaji wa huduma za ugawaji na usambazaji maji katika baadhi ya maeneo ya Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani unaendelea kwa kasi katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam na katika Miji ya Bagamoyo na Kibaha na tayari umefikia asilimia 72.2 kukamilika.
“Mradi huu unatekelezwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka, (DAWASA), ulianza rasmi Machi mwaka 2016 na unatarajiwa kukamilika Februari 28, 2018.” Alisema.
Akifafanua zaidi kuhusu kazi zinazofanyika kwa sasa, Mhandisi Mwang’ingo alitaja kuwa ni pamoja na ujenzi wa matenki tisa (9) ya kuhifadhi na kusambaza maji yenye ukubwa wa kuhifadhi kati ya lita za ujazo milioni 3.0 hadi milioni 6.0 ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vine vya kusukuma maji na ununuzi na ufungaji wa pampu kubwa za kusukuma maji 16.
Kazi nyingine ni pamoja na ununuzi wa transfoma na ufungaji njia za umeme wa msongo mkubwa, ununuzi na ulazaji mabomba yatakayokuwa na urefu wa jumla ya kilomita zipatazo 477.
“Maeneo yatakayofaidika na mradi huu ni pamoja na Salasala, Bunju, Wazo, Makongo, Changanyikeni, Bagamoyo, Mpiji, Zinga, Kiromo, Kitopeni, Ukuni, Buma, Mataya na ukanda maalum wa WPZA ambayo ni maeneo yanayohudumiwa na mtambo wa Ruvu Juu.” Alifafanua.
Aidha maeneo mengine yatakayofaidika na mradi huu ni pamoja na Mbezi Louis, Kiluvya, Kibamba, Mbezi, Msakuzi, Makabe, Malamba Mawili na Msigani na maeneo hayo yote yanapata huduma ya maji kutoka mtambo wa Ruvu Juu uliozindulkiwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli Juni 21, 2017.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya DAWASA, Bw.;aston T. Msongole, alisema ni nia ya DAWASA kuhakikisha maeneo yote ambayo hayajafikiwa na huduma ya maji hususan baadhi ya maeneo ya wilaya mpya ya Kigamboni, ni kuhakikisha huduma hiyo inawafikia.
“Tayari tumechimba visima virefu vyenye uwezo wa kutoa maji mengi ya kumaliza tatizo la ukosefu wa maji kwenye maeneo hayo lakini tatizo ni uhaba wa fedha za kutengeneza mfumo wa kuyasambaza maji hayo kwa walaji” Alisema Bw.Msongole.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Romanus Mwangi’ngo(kushoto), akifafanua jamnbo mbele ya Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maji, Mifugo na Kilimo, Mhe. Emmanuel Papian, (Kulia) na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo, walipotembelea ujemnzi wa tenki la kuhifadhia na kusambaza maji la Salasala nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam leo Januari 20, 2018.
 
 Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Maji, Mifugo na Kilimo, Mhe. Daniel; Nsanzugwanko, (katikati) akizunguzma jambo na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Romanus Mwangi’ngo, (kushoto) na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maji, Mifugo na Kilimo, Mhe. Emmanuel Papian, walipotembelea mtambo wa maji wa Ruvu Juu, Mlandizi mkoani Pwani.
 Kaimu Mwewnyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maji, Mifugo na Kilimo, Mhe. Emmanuel Papian, (Kushoto) na mjumbe wa Kamati hiyo, Mhe. Daniel Nsanzugwanko, (katikati), wakimsikilzia Mhandisi P.G. Rajani wa kampuni ya WAPCOS limited ya India, wakati wa ziara ya Kamati hiyo kwenye eneo la ujenzi wa mtambo wa kusukuma maji wa Salasala.
 Taswira ya maendeleo ya ujenzi wa tenki kubwa la kuhifadhi na kusambaza maji la Salasala ukiwa umefikia hatua ya ufunikaji kabla ya kumwaga zege.
 Mafundi wakisuka non do tayari kwa kumwaga zege kwenye tenki la Salasala.
 Modester Mushi (kushoto), ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa ufundi DAWASA akiwa na Afisa Habari na UHusiano wa Jamii Mwandamizi wa Mamlaka hiyo, Bi.Mecky Mdaku wakati wa ziara hiyo ya Kamati ya Bunge huko Salasala.
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe.Emmanuel Papian, (kushoto), akizungumza jambo na Meneja Uhusiano wa Jamii, DAWASA, Bi. Neli Msuya.
 Kamati ikipokea taarifa ya utendaji ya DAWASA/DAWASCO mwanzoni mwa ziara hiyo.
Meneja Uhusiano wa Jamii, DAWASA, Bi. Neli Msuya, akigawa taarifa ya DAWASA kwa wajumbe wa Kamati.
 Baadhi ya wajumbe wa Kamati, wakisikiliza taarifa hiyo.
 Mjumbe wa Kamati, Mhe,Kuntyi Yusuph Majala, akizunhgumza wakati wa Kamati ikipkea taarifa.
 Mhandisi Mwangi’ngo, akitoa taarifa ya utendaji ya DAWASA.
 Picha ya pamoja ya Kamati na watendaji wa DAWASA/DAWASCO na wajenzi.
 Sehemu ya mtambo wa maji Ruvu Chini.
  Sehemu ya mtambo wa maji Ruvu Chini.

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget