Kitaifa, Kimataifa, Siasa, Michezo na Burudani

December 2017

Kufuatia sakata la umiliki wa kampuni ya mawasiliano ya Airtel, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Disemba 28, 2017 iliziandikia benki zote na taasisi za kifedha ambazo zimekuwa zikisimamia akaunti za iliyokuwa Celtel, Zain au Airtel kuwasilisha taarifa hizo.

BoT imezitaka taasisi hizo ama benki kueleza kama zimewahi kuendesha ama zinaendesha akaunti zinazohusiana na kampuni tajwa.

Aidha, taasisi zote ambazo zitakuwa zina akaunti za kampuni hiyo tajwa, zimetakiwa kuwasilisha jina la akaunti, namba ya akaunti, aina ya fedha zilizomo kwenye akaunti na kiwango cha mwisho kilichokuwemo kwenye akaunti hadi Disemba 27, 2017.

Taarifa za akaunti hizo zinazotakiwa kuwasilishwa ni kaunzia Januari 1, 2000 hadi Disemba 27, 2017.

Taarifa zinazotakiwa kuwasilisha zinatakiwa kuwa katika nakala ngumu (hardcopy) na nakala teke (soft copy) na zilitakiwa kuwasilishwa  jana saa 5 asubuhi.

Ikiwa imebaki siku moja kabla ya kuuaga mwaka 2017, mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ametoa waraka akilaani ukiukwaji wa haki za binadamu na kuminywa kwa uhuru wa kutoa mawazo.

Waraka huo alioutoa jana Alhamisi Desemba 28,2017 akiwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya anakopatiwa matibabu tangu Septemba 7,2017 aliposhambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi kwenye makazi yake Area D mjini Dodoma.

Lissu pia amezungumzia tukio la kutoweka mwandishi wa habari wa kujitegemea wa kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Azory Gwanda ambaye leo ni siku ya 39 tangu alipotoweka akiwa wilayani Kibiti mkoani Pwani anakofanyia kazi zake.

“Watanzania ambao wamekuwa wakitumia uhuru wao wa maoni kutoa mawazo wamekuwa wakikamatwa na kushtakiwa mahakamani... mwanachama wa Chadema, Ben Saanane na mwandishi wa Mwananchi (Azory Gwanda) wametoweka na hawajulikani walipo. Hakuna uchunguzi au taarifa za kutoweka kwao,” amesema. 

Lissu ambaye pia ni mwanasheria wa Chadema amesema vyombo vya habari  vimekuwa katika wakati mgumu baada ya kukutana na mkono wa sheria, ikiwamo kufungiwa pale vinapoandika habari zinazotafsiriwa kuwa ni za kichochezi au uongo.

Kupitia waraka huo alioupa jina ‘Barua kutoka kitanda cha Hospitali ya Nairobi’ amezungumzia pia mambo yaliyojitokeza na yanayoendelea katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Waraka huo ameutoa siku tatu baada ya kusimama kwa mara ya kwanza tangu Septemba 7,2017 aliposhambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi.

Amesema kumekuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu na utawala bora, huku viongozi wa upinzani na wanaharakati wakikamatwa na kuwekwa mahabusu.

Lissu amesema kutokana na watawala kuwashughulikia wanaowakosoa, uhuru wa kutoa maoni umeminya na mijadala haipo.

“Mikutano ya kisiasa imezuiwa na polisi, viongozi wanakamatwa, wabunge nikiwemo mimi (Lissu) tumekamatwa mara nyingi kwa sababu zinazohusu majukumu yetu ya kazi,” amesema.

Amesema, ‘’Hakuna njia rahisi kufikia uhuru sehemu yoyote na wengi wetu tutapitia bonde la kivuli cha kifo kabla ya kufikia mlima wa matamanio yetu.”

Pia, amevilaumu vyombo vya dola akisema tangu Septemba 7,2017 aliponusurika kuuawa akiwa eneo lenye ulinzi mpaka sasa hakuna mtuhumiwa hata mmoja anayeshikiliwa kuhusika na tukio hilo.

Kuhusu onyo la Serikali kwa viongozi wa dini kutojihusisha na masuala ya kisiasa lililotolewa  Alhamisi Desemba 28,2017 na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Lissu amesema ni mwendelezo wa kuwazuia watu wasitumie uhuru wao kuzungumza na kukosoa.

Wakati Jeshi la Polisi Tanzania kupitia kanda maalum ya Dar es salaam likitangaza kuwa lazima litamhoji Askofu na kiongozi wa kanisa la Full Gospel Bible Fellowship Zachary Kakobe kwa madai ya kutoa maneno ya kashfa kwenye mahubiri yake, wapo Wanasiasa walioguswa na taarifa hii na mmoja wapo ni Mbunge wa Nzega Mjini Hussein Bashe.

Kupitia akaunti ya twitter Mbunge Hussein Bashe ameandika ;"Kesho tutazitaka Taasisi za Dini zihamasishe amani,Maendeleo, zipongeze ni muhimu kukubali kukosolewa, Serikali haitakiwi kufanya hivi kama hazivunji sheria.

"Taasisi za Dini zina haki ya kutoa maoni yao juu ya siasa,Uchumi na maswala yote ya kijamii, viongozi wa Dini wana nafasi yao"


Watoto kutoka mitaa mbalimbali ya kata ya Kipunguni wakilifuata gari la matangazo la Sauti Jamii Kipunguni na kuzipokea kwa furaha huduma mbalimbali zilizokuwa zikitolewa ikiwa ni kugawa vipeperushi na kutoa elimu bure, mapema jana katika uzinduzi wa kampeni ya Akeketwi mtu mwaka 2018.
Mchungaji wa kanisa la Sinai Pentecostal Ndugu. Imani Juma Feruzi akibandika karatasi yenye ujumbe(posters) katika pikipiki mapema jana, katika uzinduzi wa kampeni ya akeketwi mtu mwaka 2018 iliyoandaliwa na Sauti Jamii Kipunguni ili kupinga vitendo vya Ukeketaji na Rushwa ya ngono.

Mwanaharakati wa Sauti Jamii Kipunguni Bi. Tausi Msangi akibandika karatasi yenye ujumbe(posters) katika moja ya duka la dawa linalopatikana katika kata ya kipunguni, mapema jana katika uzinduzi wa kampeni ya Akeketwi mtu mwaka 2018.
Wanaharakati wa Sauti Jamii Kipunguni wakiwa na watoto mbalimbali wa kata ya hiyo wakiwa wameshika mabango yenye jumbe tofauti tofauti kuashiria kuchoshwa na vitendo vya ukeketaji vilivyoshamili katika kata hiyo, mapema jana katika uzinduzi wa kampeni ya Akeketwi mtu mwaka 2018.

Mkurugenzi wa Sauti Jamii Kipunguni Bw. Selemani Bishagazi akigawa vipeperushi kwa wakazi mbalimbali wa kata ya Kipunguni eneo la Machimbo, katika uzinduzi wa kampeni ya akeketwi mtu mwaka 2018 mapema jana jijini Dar es salaam.
Wanaharakati wa kata ya kipunguni wakicheza kwa pamoja na watoto wa kata hiyo mara baada ya kuwapa elimu juu ya kupinga ukeketaji na rushwa ya ngono mapema jana jijini Dar es salaam.

Wanaharakati wa kata ya Kipunguni wakiwa katika picha ya pamoja mapema jana jijini Dar es salaam.


Na Vicent Macha

Kituo cha sauti jamii Kipunguni jana tarehe 29 mwezi desemba kimezindua kampeni mahususi ya kutoa elimu mtaa kwa mtaa, iliyofuatiwa na zoezi  kugawa vipeperushi pamoja na kubandika karatasi zenye jumbe mbalimbali katika kata hiyo.

Akiongoza kampeni hiyo Mkurugenzi wa Sauti jamii Kipunguni Bw. Selemani Bishagazi alisema kuwa lengo kuu la kampeni hiyo kuangazia sehemu kuu mbili ambazo ni kupinga ukeketaji katika kata hiyo lakini pia rushwa ya ngono katika jamii ya kitanzania.

Aidha Bw. Bishagazi alidai kuwa kampeni hiyo imelenga kupinga vitendo vya ukeketaji ambavyo vinavyotarajiwa kutekelezwa mwakani 2018 kwani ndio mwaka mahususi kwa kukeketa hususani kwa makabila yanayotokea mkoani mara ambayo yameshamili katika kata hiyo.

Aliendelea kusema kuwa watekelezaji wakuu wa mambo haya ni watu tunaoishi nao katika jamii zetu na kesi zake zinakuwa ngumu kusikilizwa kutokana kwamba watekelezaji wa hayo ni baba, mama au shangazi hivyo inaleta ugumu katika kutoa ushahidi na mtoto anaogopa kwa kuwa anajua mzazi wake au ndugu yake atafungwa kwa sababu yake.

“Wanaharakati wengi wamekuwa wakisubiri zoezi la kukeketa lianze ndipo waanze kuwakamata wahusika wakiwa tayari wameshakeketa, lakini kwetu sisi tumeona tuzuie kabla watoto hawa hawajafanyiwa ukeketaji ili kuweza kuwakomboa juu ya mila na tamaduni mbaya kama hizi” alisema bishagazi

“Kampeni hii itakuwa ni endelevu lakini pia tutajaribu kuwa karibu na wananchi ili waweze kutupa taarifa mbalimbali kuhusu wakeketaji na tutakaa nao chini tutajaribu kuwapa elimu juu ya madhara ya ukeketaji ili waachane na mambo hayo ya kizamani na mila potofu ya kukeketa na waweze kuwa watu wema katika jamii”. Alisema Mkurugenzi huyo

Lakini pia katika maeneo mengi hususani maeneo ya kazi, vyuoni, mashuleni maeneo ya biashara wananchi wanalazimishwa sana kutoa rushwa ya ngono ili waweze kupata huduma stahiki wanayohitaji, ndio maana sauti jamii kipunguni imeamua kuanzisha kampeni hii ya kupinga rushwa ya ngono katika jamii zetu.

Sauti jamii kipunguni kwa kushrikiana na mashirika rafiki kama Global Fund na TGNP na mengineyo tutawezeza kutoa elimu kwa wananchi na kuwawajibisha waajili, madaktari, walimu na watu wote walio katika sekta za Umma na binafsi ili waweze kupinga na kutoa taarifa kwa vyombo husika endapo wataombwa rushwa ya ngono watu hao.

                          ANGALIA VIDEO HII KUJUA KILICHOENDELA ZAIDI...

                  

Serikali imewataka wasanii kutengeneza kazi nzuri zenye ubora zinazozingatia maadili ya Kitanzania ili kuwavutia wawekezaji wengi wanaotaka kudhamini kazi  hizo katika kuziandaa na kuzisambaza.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe wakati akizindua Mfumo wa MaxBurudani ulioandaliwa  na Kampuni ya MaxMalipo ambapo ameishukuru Kampuni hiyo kwa kuamua kuchukua dhamana ya kusambaza kazi za wasanii ili kuondoa kero ya muda mrefu ya wizi wa kazi za wasanii hao kupitia njia mbalimbali walizokuwa wanatumia wasanii hao ambazo zilikua zikiwalipa kiasi kidogo.
“Nimefurahishwa sana na Mfumo huu namna ambavyo utaweza kutatua changamoto ya wizi wa kazi za wasanii wetu kwa vile umeonyesha wazi namna ambavyo msanii anaweza kunufaika na kazi yake kuanzia idadi ya kazi zake zilizoenda sokoni,asilimia anazopata kwa kazi yake ambayo ni kuanzia 40-50 pamoja na kumuwezesha kutouza Haki Miliki yake kama walivyokuwa wanafanya hapo awali.”Alisema Mhe.Mwakyembe.
Aidha amewataka Wasanii kutengeneza kazi zenye ubora ambazo zitakidhi vigezo vyinavyotakiwa na Kampuni hiyo ambapo pia ameiagiza Kampuni hiyo kutochukua kazi yeyote ambayo itakuwa haina ubora wala kuwa na maadili.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Mhandisi James Kasati amesema kuwa Mfumo wa MaxBurudani inalengo la kuhakikisha wasanii wananufaika na kazi zao kwa kuwa ndio kundi lililoajiri vijana wengi hapa nchini.
Mhandisi Kasasi ameongeza kuwa Mfumo huu utatumia mawakala wa Max Malipo katika kusambaza kazi hizo ambapo Msanii atatakiwa kupeleka kazi ambayo itakuwa imekidhi vigezo vya kusmbazwa na Kampuni hiyo ndani na nje ya nchi kwa zile nchi ambazo Kampuni hiyo ina matawi.
“Mfumo huu utatumia teknolojia katika kusambaza kazi za wasanii,kulinda Haki Miliki za Wasanii lakini pia msanii kujua takwimu sahihi za mchanganuo wa kazi yake pamoja na namna ambavyo anaweza kulipa kodi kwa Serikali”.Alisema Mhandisi Kisati.
Naye Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Bibi.Joyce Fissoo amesema kuwa Bodi yake inapokea Kampuni au mtu yeyote ambae anataka kusambaza kazi za wasanii endapo tu atakuwa anawalipa Wasanii hao kile wanachostahili kupata kupitia kazi hizo.
Aidha Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bw. Godfrey Muingereza mbali na kuipongeza Kampuni hiyo kwa Wazo zuri lakini pia ameishauri kuona ambavyo inaweza kuwasadia wasanii hao kupata  mikopo itakayowasaidia kuandaa na kutengeneza kazi nzuri.
Mfumo huo tayari umeanza kupokea baadhi ya kazi za wasanii tayari kwa kuzisambaza ambazo ni Filamu ya Kampuni ya J For Life, Albamu ya Fiesta  pamoja na Albamu ya Msanii wa Nyimbo za Injili Bw. Godluck Gosbert.

Mbunge wa Jimbo la Siha, Mkoani Kilimanjaro kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Dk. Godwin Oloyce Mollel, aliyetangaza kujivua uanachama wa chama chake na kujiuzulu ubunge amewashukuru wananchi wake wa Siha kwa ushirikiano mkubwa waliompa wakati akiwa madarakani.

Godwin Mollel amejiuzulu nafasi yake ya Ubunge pamoja na kujivua uanachama wa CHADEMA huku akiomba wanachama wa Chama cha Mapinduzi kumpokea na kusema kuwa sababu kubwa iliyomfanya ahame ni kutokana na kuridhishwa na utendaji kazi wa Rais John Pombe Magufuli katika kupigania rasilimali za nchi



Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala akiongea katika Maulidi hiyo, Dar es salaam.

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala amewataka Watanzania kuhuisha kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) kwani Maulid inafundisha kupinga Dhulma, Ugaidi na Umuhimu wa Amani.
 
“Moja ya funzo ilikuwa ni kupambana na dhulma, na ndio maana Mtume akasema Msaidie ndugu yako akiwa amedhulumu au akiwa amedhulumiwa, kubwa ni kupinga vita dhulma, dunia leo hakuna shaka kuwa imegubikwa na dhulma katika Nyanja zote, ili kuiondoa dhulma tunaihitajia vikao hivi vya Maulid ya Mtume Muhammad (s.a.w.w).” amesema Sheikh Jalala

Sheikh Jalala amesema hayo leo katika Sherehe za kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) imeyofanyika katika ukumbi wa Urban Rose Hotel, Jijini Dar es salaam.


Aidha Sheikh Jalala amesema kuwa tunapokuwa tunakumbuka kuzaliwa Mtume Muhamad (s.a.w.w)tunasoma mafundisho yake yalikuwa yanapinga aina zote za Ubaguzi.


“Dunia leo imegubikwa na kuwafanya watu kuwa wanyonge, kuwagawanya watu katika matabaka, ubaguzi bado upo hata kama ni wa kifikra bado unatawala dunia, Mtume Muhammad (s.a.w.w) alipambana na Ubaguzi.”


“Mtume Muhammad (s.a.w.w) alikuja kuwafundisha watu kuwa watu wote wako sawa, leo dunia imekuja kuwagawanya watu, watu wa ulimwengu wa tatu, ulimwengu wa pili, watu wenye haki ya kumiliki, watu wasiokuwa na haki ya kumiliki, watu wanaofaidika na rasilimali walizonazo, watu wasiofaidika na rasilimali walionazo” amesema Sheikh Jalala



Sheikh Jalala amesema kuwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) katika mafunzo aliyoyafunza ni funzo la amani, kwamba Mungu tunaemuabudu ni Mungu wa Amani kwa mungu siku zote inatoka Amani, leo tunaona kwa pamoja mashariki ya kati na dunia kwa ujumla imegubikwa na kitu kinachoitwa ugaidi, imegubikwa na ukatili kupita kiasi, imegubikwa ni kuchinjana ni mateso hujawahi kuyaona hata kuyasikia katika maisha yako.


“Niseme kwa masikitiko makubwa kauli ya Raisi wa Marekani Donard Trump yakuufanya Mji mtakatifu wa Palestina Masjid Aqswa mji mtakatifu wa Jerusalem, ambapo ndani yake kuna Qibla ya Waislamu kuufanya mji mkuu badala ya Teleavivi hiki ni kinyume na ubinadamu na nikinyume na tofauti katika kuenzi Amani, kupenda watu kukaa vizuri, wakae kwa salama”.Amesisitiza Sheikh Jalala
Kadhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam amabae ni Imam Mkuu wa Msikiti wa Manyema Sheikh Hamid Jongo akiongea na Waandishi.


Kwa Upande wake Kadhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ambae pia ni Imam Mkuu wa Masjid Manyema Sheikh Hamid Jongo amewataka watanzania kulinda na kuienzi amani, utulivu na mshikanamo tulionao waislamu na wakristo hapa nchini.

“Natoa wito kwa watanzania hivi tulivyo amani, ushirikiano na utulivu tuupiganie kwani hii ndio jihadi yetu kuhakikisha vitu hivi vinadumu amani, utulivu na mshikamano na kuishi kwa kuridhiana baina ya watu wa dini zote” amesisitiza Sheikh Jongo.

Mwanasheria Mkuu wa Mgodi wa dhahabu wa Geita(GGM) David Nzarigo akipandishwa kwenye gari ya Polisi Baada ya agizo la  Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh,Kangi Lugola.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh,Kangi Lugola akipokea taarifa ya shughuli zinazofanywa na Mgodi huo.

Mganga Mkuu wa Mgodi ambaye pia anasimamia kitengo cha mazingira Mgodini wa Dhahabu wa Geita(GGM)akitoa taarifa ya namna ambavyo mgodi umekuwa ukihifadhi mazingira.

Mkuu wa Wilaya ya Geita,Mwl Herman Kapufi akitazama baadhi ya nyaraka wakati ambapo Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh,Kangi Lugola.

Mwanasheria Mkuu wa Mgodi wa dhahabu wa Geita(GGM) David Nzarigo akipelekwa kwenye gari la polisi na askali baada ya agizo la Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh,Kangi Lugola.

Moja kati ya Nyumba ambayo hipo ndani ya eneo la Mgodi.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh,Kangi Lugola akikagua madarasa ambayo yanaonekana kuharibiwa na mipasuko.


 Na Joel Maduka,Geita
Mwanasheria Mkuu wa Mgodi wa dhahabu wa Geita(GGM) David Nzarigo amekamatwa na serikali baada ya kukutwa na nyaraka za serikali .
                                                                                                                                   
Mwanasheria huyo amekamatwa kwa  amri ya Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh,Kangi Lugola alipotembelea Mgodi huo ambapo pamoja na mambo mengine amebaini mgodi huo kuwa unaendesha shughuli zake bila kufuata sheria ya mazingira .

Mhe. Lugola akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili  Wilayani Geita ameagiza kukamatwa kwa mwanasheria  Mkuu  wa Mgodi wa dhahabu wa  Geita (GGM) David Nzogila baada ya kukutwa na nyaraka za serikali ambazo hazijawa rasmi kutumika kutoka taasisi  ya wakala wa utafiti wa jiolojia Tanzania(GST).

 Hata hivyo katika hali hisiyo ya kawaida na  bila kutarajia mwanasheria huyo aliyekuwa akiukingia kifua mgodi huo  ili usikumbane na rungu la fidia ya uharibifu wa kimazingira kama sheria inavyotamka alijikuta akimweleza Naibu Waziri kuwa anayo ripoti ya GST aliyodai haijaeleza iwapo mgodi huo unahusika moja kwa moja kwenye uharibifu hivyo mgodi huo usibebeshwe mzigo huo.

Kutokana na hali hiyo,Naibu Waziri Lugola aliomba apatiwe riporti hiyo ili ajiridhishe lakini mwanasheria huyo akijibu kwa kujiamnini alimtaka kiongozi huyo wa juu   kutumia mbinu zake kuipata Serikalini lakini yeye  hawezi kutoa nyaraka ya serikali, jambo  lililomkasirisha Naibu Waziri  wa Muungano na Mazingira na kutoa agizo la kukamatwa mara moja.

Diwani wa kata ya mtakuja Constatine Morandi ameelezea kuwa wananchi wamekuwa wakisumbuliwa muda mrefu na mgodi bila ya kupatiwa fidia  na kwamba kutokana na wao kuwa ndani ya bikoni kumesababisha kutokupatiwa huduma mbali mbali za kijamii  hivyo ni vyema kwa serikali wakaweka nguvu kuwasaidia wananchi hao.

Bw Abdallah Omary-Mkazi Nyamalembo alimweleza Naibu waziri  kwamba wamekuwa wakiishi maisha ya mashaka kutokana na hali ilivyo ya maeneo hayo ya mgodini na kwamba mgodi ulikwisha wai kuwapatia fidia ya shilingi elfu ishirini jambo ambalo limeonekana kuwa ni udhalilishaji kwani pesa hiyo ni ndogo.


 Kwa upande wake Makamu wa Rais wa mgodi huo Saimon Shayo,alisema kuwa  eneo ambalo wananchi wamekuwa wakilalamika kuhusu suala la fidia hadi sasa kuna nyumba mbili na kwamba fidia ya kwanza walilipa kiasi cha sh,Bilion Moja na waliipatia serikali iweze kuwafidia wananchi.

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget