Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa ahirisho la mwisho katika kesi ya kutumia lugha ya matusi dhidi ya Rais John Magufuli inayomkabili mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee.
Akizungumza leo Ijumaa Juni 1, 2018 Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ametoa ahirisho hilo la mwisho kwa upande wa mashtaka baada ya wakili wa Serikali mwandamizi, Patrick Mwita kudai kesi ilipangwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa, hawana shahidi ikiwa ni mara ya tatu.
Baada ya kutolewa maelezo hayo, hakimu Simba alitoa ahirisho la mwisho na kupanga kesi hiyo kusikilizwa tena Juni 29, 2018 kwa mashahidi wa upande wa mashtaka kuanza kutoa ushahidi.
Katika kesi hiyo Mdee anadaiwa kufanya kosa hilo Julai 3, 2017 Makao Makuu ya Chadema yaliyopo mtaa wa Ufipa wilaya ya Kinondoni.
Anadaiwa kutamka “anaongea hovyo hovyo, anatakiwa afungwe breki” kitendo ambacho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Halima alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Julai 10, 2017. Katika kesi hiyo mbunge huyo anatetewa na mawakili, Peter Kibatala, Jeremiah Mtobesya na Hekima Mwasipu.
Post a Comment