Na Beatrice Lyimo
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Magufuli ametoa wito kwa nchi zinazokinzana ambazo zipo ndani ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki kutanguliza maslahi ya Taifa mbele na kuweka nyuma
maslahi binafsi kwa maendeleo ya nchi.
Wito huo ameutoa jana jijini Dar
es Salaam wakati wa Mkutano wa 18 wa Wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki, alipokuwa akibainisha baadhi ya mafanikio yaliyopatikana
ndani ya uongozi wake.
Rais Magufuli ambaye amemaliza
muda wake wa Uenyekiti wa Jumuiya hiyo alisema kuwa, katika uongozi
wake Jumuiya imejitahidi kupunguza uhasama miongoni mwa pande
zinazokinzana hususani katika nchi za Burundi na Sudani ya Kusini.
“Nitoe pongezi za dhati kwa
msuluhishi wa mgogoro wa Burundi, Rais Museven pamoja na mpatanishi wa
mgogoro huo Rais Mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa wamefanya kazi kubwa
sana,” alisema Dkt. Magufuli.
Aidha, alibainisha baadhi ya
mafanikio yaliyopatikana katika uongozi wake ambapo kumekuwa na
maendeleo ya miundombinu ikiwemo usafiri ambapo kumekuwa na miradi
mbalimbali ya barabara iliyokamilika na mengine tayari imeshafanyiwa
upembuzi yakinifu.
Vilevile, Rais Magufuli amesema
kuwa kumekuwa na mafanikio katika utekelezaji wa agenda ya utangamano
ambapo utekelezaji wa eneo la ushuru wa forodha unaendelea vizuri.
“Katika kipindi chetu cha uongozi
tumeweza kusimamia utekelezaji wa baadhi ya masuala yanayohusu soko la
pamoja ambapo limeanza kutekelezwa,kuhusu ushirikiano wa fedha tumeweza
kufanikisha uandaaji wa miswada miwili ambayo ipo tayari kupelekwa
katika Bunge la Afrika Mashariki,” alifafanua Rais Magufuli.
Akifafanua zaidi Rais Magufuli
amesema kuwa katika suala la utawala bora na demokrasia Jumuiya imepiga
hatua katika eneo hili ambapo utawala bora na mambo ya kidemokrasia
yameimarika, pia kukuza uhusiano baina ya Jumuiya na wadau wa
maendeleo..
Mbali na hayo Dkt. Magufuli
alibainisha baadhi ya changamoto zilizojitokeza katika uongozi wake
ikiwemo suala la Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi(EPA) ambapo Jumuiya
haikuweza kusaini mkataba huo.
Kwa upande wake Rais wa Uganda
Yoweri Kaguta Museven ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki ameshukuru kwa kuaminika na kuweza kuchaguliwa kuongoza
Jumuiya hiyo.
Aidha, Rais Museven amebainisha
baadhi ya masuala ya kuzingatia ili kuweza kuimarisha uhusiano uliopo
baina ya nchi hizi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo Ustawi wa
Maendeleo, Undugu na Ulinzi .
“tunapoongelea kuhusu Jumuiya ya
Afrika Mashariki, tunaongelea juu ya ustawi wa maendeleo yetu, familia
yetu, nchi zetu na hata soko letu, hivyo yatupasa kuzidisha utangamano
kwa maendeleo ya Jumuiya,” amesema Rais Museven.
Wakati huo huo katika Mkutano huo
baadhi ya viongozi wa Jumuiya hiyo waliapishwa. Viongozi hao ni pamoja
na Rais wa Mahakama kuu ya Afrika Mashariki Jaji Charles Oyo Nyawelo na
Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Steven Malekela Mlote aliyechukua nafasi ya
Enos Bukuku aliyemaliza muda wake.
Mbali na hayo katika Mkutano huo
washindi wa shindano la kuandika insha kwa wanafunzi wa shule za
Sekondari za EAC walikabidhiwa zawadi zao ikwemo vyeti na fedha kama
motisha ambapo mshindi wa kwanza anatoka nchini Burundi alikabidhiwa
fedha za Dolla za Kimarekani 1500.
Post a Comment