Kitaifa, Kimataifa, Siasa, Michezo na Burudani

RC TABORA: JENGENI TABIA YA KULIMA KILIMO KINACHOWAPA ZIADA

Image result for mkuu wa mkoa wa Tabora
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri

NA TIGANYA VINCENT

WAKULIMA wametakiwa kuhakikisha wanalima kilimo cha kisasa ambacho ndio kitawawezesha kuzalisha ziada ambayo ndio itawaletea faida kwa ajili ya kupata fedha za kujiletea maendeleo yatakayowaondoa katika umaskini.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa uhamasishaji wa kilimo cha kisasa cha pamba na mazao mengine katika maeneo mbalimbali.

Alisema kuwa kilimo cha mazoea cha kuzalisha mavuno kwa ajili ya matumizi ya kila siku tu hakiwezi kuleta mabadiliko chanya katika maisha yao na badala yake watakuwa wakitaabika pindi kunakuwepo na msimu mbaya wa mavuno.

Mwanri alisema kuwa ziada ndio itakayowasaidia kuleta maendeleo ikiwemo kujenga nyumba nzuri za kisasa, kulala pa zuri kula vizuri na kuwa na uwezo wa kuwaendeleza watoto wao kielimu.

Alisema kuwa kilimo cha kimazoea hakiwezi kuwasaidia kupiga hatua bali wataendelea kulima na kupata mazao ni kwa ajili ya kutumia  wakati wa mahitaji na sio kupata nyongeza kuuza kwa ajili ya kupata fedha za shughuli nyingine za maendeleo.

Mwanri alisema kuwa kwa kutambua kuwa kilimo kilichokuwa kinafanywa na wakulima walio wengi cha kutozingatia utaalamu wa Maofisa Ugani amewaagiza watumishi hao kwenda kwa wakulima vijijini ili waweze kuwasaidia kubadilisha mtindo wao wa ulimaji na kuja na mbinu mpya za kuwa na shamba dogo mavuno mengi.

“Mimi siwezi nikakaa hapa ninajivunia kuwa Mkuu wa Mkoa wakati watu wangu hawawezi kuzalisha ziada ambayo ndio itakayowawezesha kupata maendeleo…ni lazima tutoke Maofisi twende tukafundishe wakulima juu ya kilimo bora” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

Alisema kuwa ni vema Maofisa Ugani wakasaidia kuwafanya wakulima kuwa vifaa (assets)  na sio kuwa mizigo(liabilities) kwa kuwapa mbinu zitakazowasaidia kupiga hatua kutoka walipo na kusonga mbele kimaendeleo.

“Ningependa kirudi hapa mwakani nikute habari njema za kuniambia kuwa kutokana na elimu kutoka kwa Maafisa Ugani na viongozi mbalimbali mwaka huu nimepata pamba nyingi hadi nimejenga nyuma hiyo hapo…hayo ndio maendeleo tuyotaka…na sio kupata pesa unakwenda kulewa bila kufanya jambo lolote la maendeleo” alisisitiza Mwanri.

Mkuu huyo Mkoa wa Tabora ameamua kupitia katika vijiji mbalimbali kuhamasisha juu ya kilimo cha kisasa cha mazao mengi kwa ajili ya kupata malighafi za kutosha kwa ajili ya viwanda vilivyopo na vinavyotarajiwa.
Labels:

Post a Comment

[facebook]

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget