NA TIGANYA VINCENT
BODI ya Wakurugenzi wa Bodi ya Tumbaku ya Tanzania imetakiwa kufuatilia malalamiko ya baadhi ya wakulima ambao wamekuwa wakikataliwa kulima kwa sababu ya ueleza ukweli kuhusu unyanyasaji unaonywa na Viongozi vyama vya msingi vya wakulima wa tumbaku.
Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni mjini Tabora na Waziri wa Kilimo Dkt.Charles Tizeba wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Tumbaku ya Tanzania.
Alisema kuwa wakulima ambao wamekuwa wakifichua uovu unaofanywa na viongozi wa AMCOS wamekuwa wakifanyiwa visasi ikiwa na kufutwa katika unachama na wakati mwingine kuzuiwa kulima zao hilo.
Dkt. Tizeba aliiagiza Bodi mpya kuhakikisha kuwa inawalinda wakulima wote wanafichua madudu yanayofanywa na viongozi wachache kwa maslahi binafsi kwa ajili ya ustawi wa zao hilo.
Alisema kuwa wasipolindwa wakulima ambao wako mbele kusema ukweli uhai wa zao hilo unaweza kuwa mashakani kwa kuwakumbatia viongozi wa vyama vya msingi ambao ni wabadhirifu wanaogopwa.
Dkt.Tizeba alisema kuwa wakulima hao wakikubaliwa kulima , tumbaku yao itapewa bei ya chini ili kuwaziba midomo jambo ambalo ni uonevu.
Alisema kuwa pamoja na mambo mengine wajumbe hao wanajukumu la kuhakikisha kuwa wakulima hawaonewi na kunyanyasa na viongozi wao.
Katika hatua nyingine Waziri huyo wa Kilimo amewataka Bodi kuhakikisha kuwa wanasimamia wakulima wasije wakalima tumbaku nje ya mkataba(makisio) ili kuepuka usumbufu wa kukosa masoko.
Alisema kuwa wakati Serikali ikiendelea kutafuta masoko kwa wanunuzi wapya ni vema wakulima wakalima kulingana na makubaliano ili matatizo yaliyojitokeza katika msimu uliopita na kusababisha tumbaku kushindwa kununuliwa kwa wakati.
Naye Mwenyekiti wa Muda wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Tumbaku Tanzania Hassan Wakasuvi alisema kuwa watahakikisha hakuna mkulima atakayeonewa kwa kusema ukweli na kufichua uovu.
Alisema kuwa bila uadilifu kwa viongozi wa vyama vya msingi na usimamiaji wa haki zao hilo litaendelea kuyumba.
Post a Comment