Mkuu wa Kitengo cha Geology wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dr. Elisante Mshiu akiongea katika hafla hiyo.
|
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Helium One, Thomas Abraham-James akizungumza kuhusiana na suala la gesi ya Helium nchini Tanzania |
Prof. Christopher Ballentine kutoka Chuo Kikuu cha Oxford akiongea katika hafla hiyo.
|
· Helium One yatangaza udhamini kwa wanafunzi wawili kwenda kusoma Chuo Kikuu Oxford
Kampuni ya Helium One ambayo imekuwa ikifanya shughuli za utafutaji wa Helium mkoani Rukwa kwa kushirikiana na idara ya Geolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Oxford cha nchini Uingereza, imeandaa kongamano la siku moja yenye lengo la kujenga uwezo juu ya chimbuko na utafutaji wa gesi ya Helium hapa Tanzania
Lengo la kongamono hilo lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni kuwaleta pamoja wataalamu, wanasayansi na wadau wengine kutoka ngazi ya kitaifa na kimataifa na kuwezesha kubadilisha ujuzi, uzoefu na matokeo mbali mbali yanahusu gesi ya Helium katika muktadha wa Tanzania ya viwanda.
Kongamano hilo lilihusisha wanasayansi magwiji wa masuala ya gesi kutoka Chuo Kikuu maarufu cha Oxford ambao walishirikiana na wataalamu kutoka idara ya Geolojia ya UDSM, wafanya maamuzi, wadau wa maendeleo, watunga sera, watafiti na sekta binafsi kujadili mambo mbali mbali kuhusu gesi ya Helium.
Akizungumza katika kongamano hilo, Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Helium One, Thomas Abraham-James alisema kampuni hiyo imeomba na kupewa Leseni za Utafutaji 23 na maombi 3 tayari yakiwa yamewasilishwa na kuongeza kuwa leseni hizo zinamilikiwa kwa asilimia 100 na kampuni hiyo.
“Kampuni ya Helium One inaamini kuna fursa ya kutengeneza vipaji vya wazawa vyenye hadhi ya kimataifa katika shughuli za utafutaji na maendeleo ya gesi ya Helium kwa hapa Tanzania. Tutaendelea kujenga ushirikiano wetu na UDSM kupitia kubadilishana ujuzi, mafunzo kwa wanafunzi pamoja na wafanyakazi wa Wizara ya Madini kupitia ufadhili wa masomo,” alisema
Wakati wa kongomano hilo, Helium One ilitangaza ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wawili wa UDSM ambao watakwenda kusoma Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Oxford, ikiwa ni jitihada ya kuwajengea Watanzania uwezo wa kimataifa wa kisayansi juu ya masuala ya gesi pamoja na kuendeleza ushirikiano na UDSM.
Kampuni hiyo tayari imegundua takribani 98,9bcf za gesi ya Helium ikiwa ni sehemu muhimu ya ugunduzi kutokana na kupungua sana kwa upatikanaji wa gesi hiyo na ongezeko la mahitaji duniani.
“Tunaamini ugunduzi wetu wa Rukwa utakuwa na mchango muhimu na mfano mzuri kwa ajenda ya Tanzania ya viwanda pamoja na mpango wa maendeleo wa 2016/17-2020/21,” aliongeza
Mgeologia kutoka Wizara ya Nishati Mr Mussa Abbasi aliisifia shughuli za utafutaji na ugunduzi zinazofanywa na kampuni hiyo na kuongeza kuwa, Tanzania itaendelea kujenga mazingira mazuri kwa wawekezaji wote wenye nia njema ambao wanataka kuwekeza katika shughuli mbali mbali za kiuchumi.
“Serikali kupitia Wizara ya Madini inapenda kuwahakikishia wawekezaji wote kwenye sekta hii kuwa itatoa kila ushirikiano kuhakikisha kuwa wanafanikiwa katika shughuli zao. Tunachukulia sekta binafsi kama sehemu muhimu ya ukuwaji wa uchumi wa nchi yetu na ndiyo maana Serikali inavutia uwekezaji moja kwa moja na usio wa moja kwa moja,” alisema Abbasi.
Kwa upande wake Profesa John Machiwa kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam alisema kongamano hilo litatoa fursa kwa wanafunzi, wafanyakazi na jumuiya nzima ya wanataaluma wa chuo hicho kujua mambo mbali mbali kuhusu gesi ya Helium na kutengeneza namna za kufanya kazi pamoja katika kujengeana uwezo katika eneo hilo.
“Tunaamini Helium One na UDSM wana mengi ya kushirikiana kupitia kubadilisha ujuzi na maarifa ya kitaalamu ambayo yatasaidia kuboresha vijapaji vya vijana hapa chuoni na katika taasisi nyingine za elimu ya juu,” alisema Prof Machiwa.
Post a Comment