MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam leo Jumatatu, Januari 22, 2018 imemhukumu mwalimu wa sanaa ya kujihami, ‘Martial Arts’ na msanii wa filamu za Kibongo, Salum Njwete maarufu Scorpion miaka saba jela kwa kosa la kumjeruhi na kumtoboa macho kinyozi, Said Mrisho, pia mahakama imemtaka kulipa faini ya Sh. milioni 30 kwa ajili ya fidia kwa majeruhi huyo.
Kwa upande wake, mlalamikaji katika kesi hiyo Mrisho amelia mahakamani hapo akidai adhabu aliyopewa Scorpion haitoshi ikilinganishwa na kosa alilotenda huku akieleza kuwa atakwenda kwa Rais Dkt. John Magufuli kumueleza masikitiko yake.
“Sijaridhika na hii hukumu, huyu mtu amenitoboa macho nimekuwa kipofu, amenitia kilema cha maisha siwezi kufanya tena kazi zangu za kuniingizia kipato, nina watoto walikuwa wanasoma shule nzuri sasa hivi wanakwenda kuteseka, hata kama nikilipwa hiyo fidia ya Milioni 30 itanisaidia kitu gani? Nitakwenda kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda anipeleke kwa Rais Magufuli ili nikamueleze haya aweze kunisaidia,” alisema Mrisho.
Njwete alikuwa akikabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni unyang’anyi wa kutumia silaha na kumjeruhi Mrisho kwa kumchoma kisu sehemu mbalimbali za mwili zikiwemo tumboni na mabegani na kisha kumtoboa macho, kitendo anachodaiwa kutenda Septemba 6, mwaka juzi katika eneo la Buguruni Shell, jijini Dar es Salaam. Pia, anadaiwa kumwibia mali yenye thamani ya Sh 476,000/-.
Kesi hiyo imeamriwa na Hakimu Flora Haule ambapo wakili wa serikali alikuwa ni Hussein Hitu kwa niaba ya Juma Nassoro. Wakili wa upande wa utetezi alikuwa Frank Tawale kwa niaba ya Nassoro Katuga.
Post a Comment