MBUNGE wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga wamefikishwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya leo Jumatatu, Januari 22, 2018 kusikiliza kesi inayomkabili ya kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.
Sugu na Masonga walifikishwa mahakamani hapo Ijumaa iliyopita Januari 19, 2018 lakini mahakama ilizuia dhamana zao na kuwarejesha rumande hadi leo ambapo hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo, Michael Mteite alitoa uamuzi huo na kwamba kesi hiyo inatakiwa isikilizwe mfululizo kwa muda mfupi huku washtakiwa wakiwa wanafika mahakamani hapo wakitokea mahabusu.
“Mahakama hii inataka kusikiliza kesi hii kwa muda mfupi sana, ndani ya wiki moja kuanzia Jumatatu ijayo (leo) iwe imeamuriwa, hivyo washtakiwa wataendelea kuwekwa mahabusu,” amesema Mteite.
Sugu na Masonga wameshtakiwa kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli ambayo waliyatoa katika mkutano wa hadhara walioufanya Desemba 30 mwaka jana katika viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya wakati wakiwahutubia wananchi.
Post a Comment