Kitaifa, Kimataifa, Siasa, Michezo na Burudani

NEC yakiridhia kuhamishwa vituo 21 vya kupigia kura Mbweni

0V5A0017Mkurugenzi wa Uchaguzi Kailima Ramadhaniakiwa na kitabu cha wageni kwenye Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Malindi Estate ambayo ipo kwenye nyumba ya mmoja wa wagombea wa Uchaguzi Mdogo wa Madiwani Kata ya Mbweni.Picha na NEC.
Hussein Makame-NEC
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imejiridhisha kuwa uamuzi wa kuvihamisha vituo 21 vya kupigia kura katika Kata ya Mbweni, jimbo la Kawe katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, umezingatia Sheria na Kanuni za Uchaguzi.
NEC imetoa msimamo huo, baada ya kupokea taarifa kutoka kwa baadhi ya wananchi na vyama vya siasa wakilalamika kuwa Tume ya uchaguzi imehamisha vituo vinane (8) vya kupigia kura na kuvipeleka kwenye Kituo cha Polisi, hatua waliyoeleza kuwa ni kuwanyima haki wapiga kura katika kutimiza haki ya msingi.
Malalamiko mengine yaliyoifikia NEC ni kwamba Tume ilivihamisha vituo vingine 15 kutoka maeneo ya awali na kuvipeleka maeneo mengine jambo ambalo baadhi ya vyama havikukubaliana na uamuzi huo.
Kutokana na malalamiko hayo, jana Jumanne Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima Ramadhani akiambatana na watendaji wengine wa Tume, walitembelea maeneo hayo na kujiridhisha kuwa mabadiliiko ya vituo yaliyofanywa na msimamizi wa uchaguzi yamekidhi matakwa ya kisheria.
“Nimefika hapa jimbo la Kawe kata ya Mbweni, baada ya mwananchi mmoja kunitumia ujumbe akiniambia kuwa kuna chama kimoja kinachoshiriki Uchaguzi Mdogo wa Madiwani wa Kata ya Mbweni kinalalamika kwamba Tume imehamisha vituo vya kupigia kura kiholela,” alisema Ramadhani.
Mkurugenzi wa Uchaguzi aliongeza kuwa, chama hicho kimelalamika kuwa vituo hivyo vimepelekwa kwenye eneo la kituo cha Polisi, kwa hiyo huenda wapigakura wakanyimwa haki yao ya kupiga kura.
Alisema alipowauliza watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, majibu yao hayakumridhisha ndipo alipoamua kufika eneo la tukio.
“Kwanza wanalalamika kwamba vituo vilivyohamishwa ni 27, lakini ukweli ni vituo 21, vituo hivyo vimehamishwa kwa mujibu wa Sheria kwa sababu  Novemba mosi 2017, Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata aliviita vyama vinne na kufanya mkutano na aliwaambia tunavihamisha vituo hivyo kwa sababu mbalimbali.
“Sababu alizozitoa msimamizi wa uchaguzi ni kwamba vituo vinane  vilikuwa shule ya Sekondari New Era na vituo saba7 vilikuwa jirani na nyumbani kwa mgombea ambaye ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa na vituo sita vilikuwa kwenye eneo la Kanisa,” alifafanua Kailima.
Alibainisha kuwa kifungu cha 20 (2) cha Kanuni za Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura za Mwaka 2015 na Kifungu cha 21 cha Kanuni za Uchaguzi Mkuu wa 2015, vinabainisha kuwa vituo vya kupigia kura havipaswi kuwa kwenye maeneo ya watu binafsi, kwenye maeneo ya ibada na kwenye kambi za jeshi.
Kutokana na msingi wa kanuni hizo, Kailima alithibitisha kuwa uamuzi wa kuvihamisha vituo hivyo kwenye maeneo hayo ambao umefanywa na  msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Kawe ulikuwa sahihi.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ambaye ndiye  Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kawe ilipo kata ya Mbweni, Aron Kagurumjuri alisema malalamiko kuhusu kuhamishwa kwa vituo hivyo yalitolewa na chama kimoja kati ya vyama vinne ambavyo vitashiriki kwenye uchaguzi mdogo wa diwani wa kata hiyo.
Alisema Uchaguzi mdogo wa kata hiyo unafanyika baada ya mahakama kutengua uchaguzi wa awali kutokana na ukiukwaji wa baadhi ya taratibu za Uchaguzi.
“Tuko hapa kwa sababu chama kimoja kati ya vyama vinne vinavyoshiriki Uchaguzi huu mdogo, kulalamika kwamba tumehamisha vituo na kuvipelekea kwenye maeneo ambayo sio rafiki kwa wapiga kura,” alisema Kagurumjuri.  
Alifafanua kuwa hali halisi inaonesha kwamba kanuni  na taratibu za kupigia kura, haziruhusu kuweka kituo kwenye jengo la mtu binafsi,  na shule hiyo ambayo ilikuwa na vituo kadhaa ni shule ya mtu binafsi.
“Kwa hiyo kwa Uchaguzi huo wa mwakaa 2015 kanuni hizo zilikiukwa sasa kwa uchaguzi huu kwa sababu tunataka tufanye Uchaguzi kwa kufuata kanuni na sheria hatukutaka kuingia kwenye uvunjaji wa kanuni na taratibu,”
 “Baada ya kuhamisha vituo na kuvipeleka eneo hilo, ikazua sintofahamu kwa chama kimoja na vyama vitatu vilivyoridhia ambapo tulikuwa na mashaka inawezekana kilifaidika na vituo kuwepo maeneo hayo,” alisema.
Kagurumjuri alisema vituo vingine vimehamishiwa kwenye eneo la wazi na lenye usalama zaidi kwa wapiga kura pamoja na vitu vingine, na kwamba wanaona halina shida.

Post a Comment

[facebook]

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget