AGIZO la Rais Dk. John Magufuli kuhusu wananchi
wanaofanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka vyanzo vya maji
wasibughudhiwe limeibua maswali bungeni ikielezwa kuwa kauli hiyo ya Rais
amevunja sheria.
Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa
katika swali la nyongeza bungeni amesema, “Kwanza niipongeze wizara mara nyingi
imejitahidi kuelimisha jamii itunze mazingira, lakini sisi kama wawakilishi wa
wananchi tumsikilize Rais au waziri? mara nyingi tumeambiwa akisema Rais ni
sheria jana amewaambia wananchi waingie
kwenye mabonde walime mpaka mvua itakapowatoa, lakini waziri unazuia.”
Akijibu swali hilo , Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira), Kangi Lugola amesema Rais Magufuli hajavunja sheria
kuagiza mamlaka zinazohusika na mazingira kuacha kuwabughudhi wananchi
wanaolima pembezoni mwa mito.
Pia, ameonya viongozi wanaochochea wananchi kuvunja sheria na
wananchi waliozoea kuzivunja akisema Serikali itapambana nao.
Lugola pamoja na waziri wa wizara hiyo, January Makamba leo
Jumatano Novemba 8,2017 wamesema sheria inatoa mamlaka kwa waziri kutoa kibali
kwa shughuli kufanyika katika maeneo hayo.
Waziri January amesema kutokana na maelekezo ya Rais Magufuli
ya jana Jumanne Novemba 7,2017 kwa eneo mahsusi kwa mujibu wa sheria wataweka
mwongozo wa matumizi.
Rais Magufuli alisema busara itumike wakati wa utekelezaji
wa sheria ya mazingira inayozuia shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60
kutoka kwenye chanzo cha maji ili kuwaondolea kero wakulima
wanaojitafutia chakula na kipato cha kawaida kwa ajili ya familia zao.
“Ni vyema utekelezaji wa sheria ya mazingira ya mita 60
ilenge zaidi kubana wanaotumia maeneo ya maziwa na bahari na si wananchi
wanaolima mazao ya chakula ya muda mfupi kando mwa mito,” aliagiza.
Rais Magufuli alitoa kauli hiyo baada ya kupokea malalamiko
kutoka kwa mwananchi aliyejitambulisha kwa jina moja la Roshi, mkazi wa Kyaka
wilayani Missenyi aliyedai kuwa mazao ya chakula yaliyokuwa kwenye shamba
lake lililopo kando mwa mto yalifyekwa na watu wa mazingira kwa madai
kuwa yalilimwa ndani ya mita 60.
Rais Magufuli alisisitiza agizo hilo wilayani Karagwe na hata
mjini Bukoba akiagiza wananchi hao kuendelea na shughuli za kujiongezea
kipato na wasiondolewe katika maeneo hayo.
Kuhusu wananchi wanaodaiwa kuvamia vyanzo vya maji, Rais
aliagiza watu zaidi ya 200 wanaodaiwa kuvamia vyanzo vya maji watafutiwe maeneo
mengine kwa sababu ni kosa la viongozi na mamlaka husika zilizozembea kuwazuia
mapema kuingilia maeneo hayo.
Post a Comment