JUMLA ya shilingi milioni 202
zimetolewa kwa vikundi 89 na Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora
ikiwa ni sehemu ya mikopo ya kuwezesha vijana , wanawake na walemavu.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri |
Fedha hizo zimekabidhiwa jana na Mkuu
wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa sherehe fupi ya uzinduzi wa Jukwaa la
Wanawake na kukabidhi mkopo iliyofanyika mjini Kaliua na kuhudhuria na
wabunge wa majimbo yote mawili ya Wilaya hiyo.
Alisema mkopo huo ni sehemu ya
utekelezaji wa maagizo ya viongozi wa juu ya kutaka kila Halmashauri itenge
asilimia kumi ya mapato ya ndani kwa ajili ya uwezeshaji wa vikundi vya
wanawake asilimia nne, uwezeshaji vijana asilimia nne na uwezeshaji watu wenye
ulemavu asilimia mbili.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora alitoa
wito kwa vikundi vya wanawake vilivyofanikiwa kupata fedha hizo kuzitumia
katika malengo waliyoweka ili waweze kuzirejesha kwa ajili ya kuwakopesha
wengine.
Alisema kuwa ni vema fedha
walizokopeshwa wakazitumia kwa ajili ya shughuli zao za maendeleo na kisha
wazirudishe ili kije kigezo cha siku nyingine kuweza kukopesheka.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Abel
Busalama aliwakumbusha vikundi vilivyokeshwa kutambua kuwa fedha hizo sio
hisani bali ni mkopo ambao wanapaswa kuufanyia kazi ili waweze kupiga hatua na
kisha waurejeshe ili vijana na wanawake wenzao nao wapate fursa ya kukopa.
Alisema kuwa wanaimani kuwa kundi
hilo likitumia vizuri mikopo hiyo jamii yote ya wilaya itakuwa na maendeleo na
uchumi wa Wilaya hiyo utaimarika.
Kwa upande Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Kaliua John Pima alisema kuwa wataendelea kuhakikisha kuwa kila
mwezi wanatenga fedha kutokana na mapato ya ndani ili baadae wawakopeshe
wanawake, vijana na walemavu kwa ajili ya kusaidia kuboresha maisha yao na
jamii inayowazunguka.
Naye Mbunge Jimbo la Ulyankulu John
Kadutu alitoa wito kwa wakazi wa Wilaya ya Kaliua kuungana katika shughuli za
maendeleo bila kujali tofauti za itikadi zao za vyama.
Alisema kuwa yeye na mbunge wa Kaliua
ambaye anatoka Chama cha waananchi CUF wamekuwa mstari wa mbele kupigania
maslahi ya wananchi wote na kuwataka viongozi vingine waige mfano huo.
Wakati huo huo Halmashauri ya Wilaya
ya Kaliua imetoa pikipiki nane zenye thamani ya shilingi milioni 18.9 kwa ajili
ya Maafisa Ugani wanne na Watendaji wa Kata wanne ili kuimarisha utoaji wa
huduma kwa wakazi wa maneo yao.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri hiyo Pima , pikipiki hizo zinalenga kuwaondolewa Maafisa Ugani
uhaba wa usafiri ili waweze kuwahudumia vizuri wakulima na kuwasaidia ili
waweze kupata mazao mengi na bora.
Alisema kuwa wakati mwingine ilikuwa
vigumu kwa Maafisa Ugani kuwafikia wakulima kwa sababu ya kuwa mbali na hivyo
vyombo hivyo wa usafiri vitasaidia kuondoa visingizio kwa watumishi hao.
Kuhusu watendaji wa Kata kupata
usafiri huo alisema kuwa zitawasaidia kuimarisha shughuli za utawala ikiwemo
kusikiliza kero na matatizo mbalimbali ya wananchi na kuwaondolea shida ya
wananchi kusafiri umbali mrefu ili kuwafuata viongozi.
Akiongea wakati wa kukabidhi pikipiki
hizo kwa watumishi hao Mkuu wa Mkoa wa Tabora aliwaonya kutumia vyombo hivyo
kuwasaidia wananchi na sio kwa maslahi binafsia kama vile kubeba mizigo na
wakati mwingine kuzigeuza bodaboda.
Alisema kuwa atakayebainika atachukuliwa
hatua kali ili ije iwe fundisho kwa wengine.
Watendaji walipata pikipiki wanatoka
kata za Ilege, Igwisi, Usimba na Nhwande na kwa upande wa Maafisa Ugani watoka
kata za Seleli, Zugumlole, Silambo na Ukimbisiganga.
Post a Comment