Meya Mwita ashauri Vijana wasichague kazi za kufanya
NA CHRISTINA MWAGALA, OFISI YA MEYA WA JIJI DAR
MSTAHIKI Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita amewataka vijana kuacha tabia ya kuchagua kazi za kufanya, kutegemea ajira serikalini badala yake wawe wabunifu na kuwa tayari kufanya shughuli yoyote isipokuwa ya kiuhalifu.
Meya Mwita ametoa kauli hiyo jijini hapa leo wakati akizungumza na wanafunzi wanaohitimu elimu ya kidato cha nne katika shule ya Sekondari Minazini iliyopo Kata ya Vijibweni ,Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni .
Meya Mwita ameeleza kuwa vijana wengi wanachagua kazi kwa malengo ya kusubiri ajira kutoka serikalini jambo ambalo alisema sio sawa na kwamba wanapaswa kufanya shughuli yoyote ambayo itawaingizia kipato na kuweza kuendesha maisha yao.
“ Vijana wangu tufanyeni kazi, tuache habari za kuchagua kazi ipi unataka kuifanya, kazi ni kazi tu ilimradi inakuingizia kipato cha kuendesha maisha yako, lakini msifanye zile ambazo mnajua sio halali mana vyombo vya dola vitawashugulikia” amesema Meya Mwita.
Mbali na hilo ,Meya Mwita amewapongeza walimu kutokana na kujitoa kwao kuwafundisha wanafunzi licha ya changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.
Amesema walimu wamekuwa na changamoto kadha wa kadha lakini bado wamekuwa wavumilivu ikiwemo kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri katika masomo yao ambapo alitumia nafasi hiyo kuwataka wazazi, kamati za shule kutoa ushirikiano wa kutosha ili waweze kutimiza majukumu yao.
“ Naelewa kwamba zipo changamoto nyingi zinazo wakabili, lakini bado mnafanya kazi kwa moyo mmoja, kutokana na juhudi hizo nawapongeza sana, zile changamoto ambazo ninauwezo wakuzitatua tutashirikiana” amesema.
Katika hatua nyingine Meya Mwita ameahidi kuwachimbia kisima cha maji shuleni hapo ili kuondokana na changamoto ya kutumia gharama kubwa ya kununua maji jambo ambalo alielezwa wakati wa risala iliyosomwa na wanafunzi washule hilo.
Hata hivyo Mkuu wa shule hiyo Maria Abihudi amesema kuwa shule hiyo inachangamoto ya Umeme ambapo kwasasa upo katika jingo moja la walimu hivyo bado kusambazwa kwenye madarasa mengine ambapo Meya Mwita aliahidi kulishughulikia jambo hilo.
Post a Comment