Hatua hiyo inakuja baada ya jana upande wa Jamhuri kumsomea maelezo ya awali mshtakiwa huyo ambaye pia anakabiliwa na kesi nyingine ya uchochezi katika Mahakama ya Wilaya ya Arumeru.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Devota Msoffe, alisema kutokana na kesi hiyo kuwa nje ya wakati, itasikilizwa siku tatu mfululizo kuanzia Novemba 27 hadi 29, mwaka huu.
“Tutasikiliza kesi hii siku tatu mfululizo kwani iko nje ya wakati na natoa agizo kwa mashahidi wa Jamhuri kuitwa ambapo tunatarajia kufunga ushahidi wao Novemba 29,” alisema Hakimu huyo.
Wakili wa Serikali, Agness Hyera, akimsomea Lema maelezo ya awali katika kesi hiyo namba 440 ya mwaka 2016, alidai kuwa mshtakiwa huyo anakabiliwa na shtaka moja la uchochezi ambapo anadaiwa kutenda kosa hilo Oktoba 22, mwaka jana katika eneo la Kambi ya Fisi, Kata ya Ngarenaro akiwa anahutubia mkutano wa hadhara.
Miongoni mwa maneno ya uchochezi anayodaiwa kuyatoa Lema ni pamoja na: “Rais Magufuli akiendelea na tabia ya kudhalilisha demokrasia na uongozi wa upinzani iko siku Taifa litaingia kwenye umwagaji wa damu,…. “Rais yeyote ambaye haheshimu mipaka ya sheria, mipaka ya Katiba, rais huyo ataliingiza Taifa katika majanga na umwagaji damu,watu watajaa vifua, wakiamua kulipuka polisi hawa wala jeshi halitaweza kudhibiti uhalifu utakaojitokeza.”
Baada ya kumsomea mashtaka hayo, Wakili Hyera aliiomba mahakama kupanga tarehe ya kuanza kusikiliza na kuwa hawakuwa tayari kuweka hadharani majina ya mashahidi wao wala vielelezo ambapo alisema wanatarajia kuwa na mashahidi wasiozidi 10.
Post a Comment