Kitaifa, Kimataifa, Siasa, Michezo na Burudani

Majaliwa awapa onyo Mawaziri

Image result for waziri mkuu kasimu majaliwa
WAZIRI MKUU, KASSIM MAJALIWA.

WAZIRI Mkuu 
Kassim Majaliwa, amewaonya mawaziri na kuwataka  wasitumie madaraka yao kama fursa ya kujitajirisha wao binafsi badala yake wametakiwa watumie madaraka hayo kwa manufaa ya taifa.

Majaliwa alitoa angalizo hilo  jana alipozungumza na baadhi ya mawaziri, manaibu na makatibu wakuu katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Alisema Rais John Magufuli amesisitiza kwamba amewateua ili wafanye kazi, hivyo wasitumie madaraka waliyopewa kwa maslahi yao binafsi.

“Madaraka haya ya uwaziri si fursa ya kujipatia utajiri, tunatakiwa tufanye kazi kwa weledi, uadilifu, bidii na uaminifu mkubwa ili kuondoa kero za wananchi kwa wakati,” alisema Majaliwa.


Waziri   aliwataka mawaziri na manaibu waziri wazingatie Katiba ya nchi, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya serikali katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, mawaziri hao wanatakiwa wasimamie utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa kuanzia mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021.

Pia aliwataka kusimamia utekelezaji wa ahadi zote zilizopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 pamoja na ahadi alizozitoa Rais Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi.

Waziri Mkuu aliwaagiza mawaziri wahakikishe wanakwenda kufanya ufuatiliaji wa tathmini ya utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo inayohusu sekta zao.

Kadhalika, aliwataka mawaziri hao wakasimamie kikamilifu ukusanyaji wa mapato na kuanzisha vyanzo vipya vya ukusanyaji pamoja na kudhibiti mianya ya upotevu.

Vilevile aliwataka mawaziri hao wakapunguze urasimu katika utekelezaji wa malengo ya Serikali kwa sababu wananchi wanahitaji kuhudumiwa kwa wakati.

Mawaziri waliohudhuria kikao hicho ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Suileiman Jaffo pamoja na manaibu wake, Joseph Kandege na George Kakunda; Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na Naibu wake, Dk. Faustine Ndungulile.

 Wengine ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe na Naibu wake, Jumaa Aweso; Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage na Naibu wake, Mhandisi Stella Manyanya.

Wamo pia Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla na Naibu wake, Japhet Hasunga; Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako na Naibu wake, William ole Nasha; Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega na makatibu wakuu wa wizara hizo.
Labels:

Post a Comment

[facebook]

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget