|
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege Tanzania (TAA), Bw.
Richard Mayongela (katikati mstari wa mbele), akinyanyua mikono juu
kuashiria mshikamano daima na baadhi ya viongozi wa matawi wa chama cha
wafanyakazi mahala pa kazi (TUGHE) matawi ya Makao Makuu na Kiwanja cha
Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), alipokutana nao leo.
|
|
Viongozi wa
Chama cha Wafanyakazi mahala pa Kazi (TUGHE) matawi ya Mamlaka ya Viwanja
vya Ndege Tanzania, Makao Makuu (TAA HQ) na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa
cha Julius Nyerere (JNIA), jana wakimsikiliza kwa makini Kaimu Mkurugenzi
Mkuu, Bw. Richard Mayongela (kushoto) alipokutana nao leo.
|
|
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw.
Richard Mayongela leo akiongea na baadhi ya viongozi wa Matawi ya Chama
cha Wafanyakazi mahala pa kazi (TUGHE), TAA Makao Makuu na Kiwanja cha
Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
|
Na Mwandishi
Wetu
KAIMU
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard
Mayongela amewataka viongozi wa wafanyakazi kupitia matawi mawili ya Chama cha Wafanyakazi, TAA Makao Makuu na
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), kutenda haki kwa
kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi wote bila kubagua na kuwasilisha kwa
mwajiri ili yaweze kufanyiwa kazi kwa wakati.
Bw.
Mayongela ametoa kauli hiyo leo wakati viongozi wa matawi hayo walipokwenda
kujitambulisha ofisi kwake TAA Makao Makuu, ambapo alisisitiza kuwa wafanyakazi
wa chini ndio wenye matatizo makubwa lakini wamekuwa hawasikilizwi na
kutatuliwa matatizo yao kwa wakati.
“Ninashukuru
uongozi mmekuja kuonana nami, ninahitaji ushirikiano wenu kama chama cha
wafanyakazi, muwatumikie wafanyakazi kwa kutenda haki mkisikiliza matatizo ya
kila mmoja na kufikisha sehemu husika na ninawaahidi kuwa nanyi bega kwa bega
kutatua matatizo ya wafanyakazi kwani wao ndio wanafanya TAA iwepo, endapo
wakifanya kazi bila manung’uniko wala makundi, mamlaka yetu itasonga mbele kwa
kuwa uongozi sio kupigana vita bali tunatakiwa kujenga na kuwa kitu kimoja.”
amesema Bw. Mayongela.
Hatahivyo
amesema, kwa sasa yupo mbioni kuangalia namna ya kuboresha maslahi ya
wafanyakazi kwa kupitia makusanyo
yatakayotokana na vyanzo mbalimbali vya mapato ili kuongeza tija na ufanisi wa
kazi, kwa kuwa inaonekana wengi wamekata tamaa kutokana na kufanya kazi nyingi
na wakati mwingine kupitiliza muda wa kazi wa kawaida bila kupata stahiki
yeyote.
“Kwa msaada
wa Mungu nina imani atanionyesha wapi fedha zilipo na jinsi ya kuzitumia
ipasavyo kwa masuala ya msingi, na ninakusudia hadi kufika Desemba mwaka huu
niweze kuboresha maslahi ya wafanyakazi. Watu wanafanya kazi sana lakini
maslahi ni madogo, unaona kabisa jinsi mtu anavyoitumikia taasisi kwa moyo,
lakini sura inaonesha jinsi alivyokata tamaa, ninaamini kwa kufanya hivi
itaongeza tija na bidii ya kazi.” amesema Bw. Mayongela.
Halikadhalika,
Bw. Mayongela amesema atahakikisha wafanyakazi wanapata vitendea kazi vya
uhakika kulingana na kazi zao, zikiwemo bajaji, pikipiki na magari kwa ajili ya
doria na kwa shughuli za uendeshaji ndani Viwanja vya Ndege.
Pia
amewataka viongozi hao kuwa karibu na wafanyakazi ili kuhakikisha
wanawahamasisha wanafanya kazi kwa bidii, uaminifu na uadilifu ili kuondoa
mianya na tabia za upokeaji wa rushwa, kwa kuwa TUGHE ni daraja kati ya mwajiri
na wafanyakazi.
Naye
Mwenyekiti wa TUGHE tawi la TAA Makao Makuu, Bw.
Nasib Elias mbali na
kumshukuru Kaimu Mkurugenzi Mkuu kwa kuwapa fursa ya kukutana naye, lakini
amemuomba kuendelea kudumisha mahusiano baina ya mwajiri na chama cha
wafanyakazi (TUGHE), na pia kumuomba aitake menejimenti yake kuwa na utaratibu
wa kuweka milango wazi kwa wafanyakazi kama yeye ili waweze kusikiliza na kutoa
majibu sahihi kwa baadhi ya masuala ya kiofisi yanayowasilishwa na wafanyakazi
kwao na sio kila jambo liwasilishwe kwake.
“Tunakuombea
kwa Mungu akutie nguvu kwa haya unayotaka kufanya likiwemo la kuboresha maslahi
ya wafanyakazi kwa kuwa litasaidia kuamsha morali ya kazi kwa wafanyakazi,
lakini hii sera yako ya kuwacha milango wazi tunaomba nayo itekelezwe katika
ngazi ya menejimenti yako kwani kuna mambo ambayo yanaweza kumalizwa na
Wakurugenzi na Mameneja wenyewe na sio lazima yafike kwako, “ amesema Bw.
Elias.
Katika kuboresha
maslahi ya wafanyakazi ambacho kimeonekana ni kipaumbele cha Kaimu Mkurugenzi
mkuu kwa wafanyakazi, Bw. Elias amemuomba kuangalia namna bora ya kusimamia
maslahi hayo ikiwemo kuuasili mkataba wa hali bora (SBA) kama inavyotekelezwa
na taasisi nyingine za serikali.