Kitaifa, Kimataifa, Siasa, Michezo na Burudani

Sumatra yawatangazia vita madereva Mbezi- Mlandizi

MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) mkoani Pwani, imetangaza adhabu nzito kwa madereva wa mabasi ya abiria yasiyopita katika kituo cha Loliondo, Kibaha Maili Moja.

Kwa mujibu wa Sumatra, madereva watakaokaidi kupitia katika kituo hicho ambacho kimeanzishwa baada ya kufungwa kwa kile cha Maili Moja, watafutiwa leseni na kufikishwa mahakamani.

Ofisa Mfawidhi wa Sumatra mkoani wa Pwani, Omary Ayubu, alisema hayo jana wakati wa ukaguzi wa magari ya abiria yanayofanya safari kati ya Mbezi, Dar es Salaam na na Mlandizi mkoani Pwani. Ukaguzi huo ulifanywa kwa ushirikiano kati ya mamlaka hiyo, Jeshi la Polisi na kamati ya Usalama Barabarani mkoa wa Pwani.

Alisema Sumatra haitawafumbia macho madereva wasiopita Loliondo kwa kuwa ndicho kituo cha mabasi madogo na kuwa endapo kuna malalamiko, yafikishwe katika ofisi zake badala ya kugoma na kuwanyima haki abiria.

"Coaster na Hiace zote zinazotoka Mbezi kwenda maeneo ya Kwa Mathias, Visiga hadi Mlandizi sharti zote zipite Loliondo. Kama kuna mtu ana malalamiko kuna njia rafiki za kuyafikisha na si kugoma na kuwashawishi madereva wengine wagome, hilo ni kosa", alisema Omary.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Pwani, Salum Morimori, aliwataka wamiliki wa mabasi kuhakikisha wanaboresha vyombo vyao sambamba na matairi na viti, ili gari liwe bora na kukidhi viwango vya usafirishaji.

Alisema madereva wakifuata maelekezo hayo wataepuka faini mbalimbali za barabarani, lakini pia huduma ya usafiri itakuwa bora na hakutakuwa na malalamiko kutoka kwa jamii.

"Ukaguzi huu una lengo la kutathmini ubora wa magari na kujua matatizo yanayowakuta abiria pindi wanaposafiri kwani tumekuwa tukipata malalamiko mengi ikiwamo abiria kutokupewa tiketi wawapo safarini, lakini pia madereva kukatisha ruti jambo linalosababisha usumbufu mkubwa kwa abiria,” alisema Morimori.

Mmoja wa wamiliki wa mabasi hayo, Daniel Minja, aliiomba serikali kuongeza kiwango cha nauli cha Sh. 500 kutoka Mbezi hadi Maili Moja na kile cha Sh. 1,600 cha Mbezi hadi Mlandizi 1600. Alisema viwango hivyo ni vidogo kulinganisha na gharama za uendeshaji.

Magari 35 yalikaguliwa na kukutwa na makosa mbalimbali na madereva wanane waliokutwa na makosa na wanatarajiwa kupelekwa mahakamani na wengine watatozwa faini kulingana na makosa waliyoyafanya.
Labels:

Post a Comment

[facebook]

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget