Kitaifa, Kimataifa, Siasa, Michezo na Burudani

MAHAKAMA YA WATOTO SULUHISHO YA KESI ZA WATOTO


unnamed
Mwuonekano wa jengo la Mahakama ya Watoto iliyopo katika Jiji la Mbeya.
…………..
Na Magreth Kinabo – Mahakama ya Tanzania
Hivi karibuni vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti kuhusu habari za vitendo  vya ukatili na unyanyasaji wa watoto.
Kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo, viongozi mbalimbali wamekuwa wakitoa  matamko ambayo yanaitaka jamii kufahamu haki za mtoto ikiwa  ni hatua ya  kuwaepusha watoto wasiathiriwe na tabia hatarishi.
Miongoni mwa viongozi hayo ni Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, na Waziri wa Afya,Jinsia na Maendeleo ya Jamii, Mhe.  Ummy Mwalimu akiwemo Naibu wake. Dkt. Hamis Kingwallah na baadhi ya viongozi wengine mbalimbali.

Serikali  kwa kushirikiana na viongozi  wa asasi za kiraia  na dini mbalimbali  wameungana ili kuhakikisha   watoto hao, wanakua katika maadili mema na kuweza kutimiza ndoto zao.
Mbali na hilo, kuhakikisha kwamba  watu wanaowarubuni  watoto  wanachukuliwa hatua za kisheria.
Mahakama  ya Tanzania  kupitia Mpango Mkakati  wa Miaka Mitano yaani 2015/16 hadi 2019/20, imejenga  Mahakama  nyingine  ya  watoto  ambayo  iko  katika Jiji la Mbeya.
Kupitia  mpango huo,  hivi  sasa Tanzania ina mahakama mbili za watoto ambazo moja iko katika jiji la Dares Salaam na nyingine  jiji la Mbeya.
Mahakama hizi mbili  ziko katika maeneo ya katikati  ya jiji, ikiwa dhamira  ya Mahakama ya Tanzania, kuhakikisha kwamba  inaboresha  huduma  za utoaji  haki    na kusongeza  huduma  zake karibu  na  wananchi.
Mahakama ya Watoto ni Mahakama ambayo imeanzishwa kisheria kwa lengo la kushughulikia kesi maalum zinazohusu watoto.
Umri ambao Mahakama hiyo mtoto ni mtu aliye na umri wa chini ya 18 kama Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inavyosema sura ya kwanza, kifungu cha 5.-(1) na ilivyo katika Sheria ya Mtoto  namba 21 ya mwaka 2009 pamoja na kanuni zake, marekebisho  ya mwaka 2006.
Mahakama hii inashughulikia makosa mbalimbali ambayo yanaweza kufanywa na watoto kama  shuleni, mitaani na sehemu nyinginezo.
Kuna   mambo mbalimbali  ambayo  pia Mahakama hii  inayashughulikia   mfano vile taratibu za kuasili watoto na mambo ambayo yanaweza kujitokeza kutokana na mchakato mzima wa kufanya hivyo, ikiwemo kupokea mashauri ya madai.
Usikilizaji wa mashauri katika Mahakama  hii, hufanyika faragha. Lengo la usikilizaji wa mashauri  haya kusikilizwa kwa siri  ni  kulinda maslahi ya mtoto.
Hivyo  jamii inapaswa  kuzifahamu  haki  za  mtoto kama vile  haki ya kuishi, kupata huduma bora za afya, mahali pa kuishi.kupata elimu, haki ya kutambuliwa, haki ya kurithi mali, haki ya kutonyanyaswa, ikiwemo kutofanyiwa  vitendo  vya ukatili wa kijinsia.
Kwa  mujibu  wa  taarifa  ya  Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya  Jamii, Jinsia,  Wazee  na Watoto Sihaba Nkinga, akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuzuia Ukeketaji,iliyofanyika Desemba  5, mwaka  jana, Sihaba Nkinga, alisema hali bado ni mbaya.
Katibu Mkuu huyo alifafanua kwamba taarifa zinaonyesha kuwa mtoto mmoja kati ya watatu wa kike na mtoto mmoja wa kati ya saba wa kiume walifanyiwa ukatili wa kingono.
Kupitia maadhimisho  hayo, Mkuu wa Wilaya ya Pangani, mkoani Tanga, Bi Zainabu Issa ametaka jamii ipige vita vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, ili kuwawezesha kufikia ndoto zao ikiwa ni hatua ya kuwawezesha ustawi wa maisha yao na  hatimaye kulijenga taifa la kesho.
“Ninasema kesi dhidi ya ukatili wa watoto sasa zisizidi miezi sita au mwaka, kesi zisikae, muda mrefu Mahakamani.Ninasema sasa mtu akipatikana na hatia ya kuumpa ujauzito mwanafunzi au kubaka afungwe miaka 30 jela,” alisema Mkuu huyo wa wilaya wakati siku ya maadhimisho hayo yaliyofanyika Mkoani Tanga, wilaya ya Pangani.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Appi akizungumza maadhimisho hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, alipiga marufuku vitendo vya baadhi ya walimu kuwafungia mageti wanafunzi wanapochelewa kufika mashuleni kwa kuwa vinaweza kuwasababishia watoto kujiunga na makundi yenye tabia hatarishi.
 Alisema  ili  kuweza  kuwaepusha  watoto kutoathiriwa  na tabia hatarishi, Mkuu huyo  alipendekeza walimu watumie adhabu mbadala pale baadhi ya wanafunzi  wanapofanya makosa  wakiwa  mashuleni.
 Alisema  adhabu mbadala  zinaweza kutolewa na walimu,  wakati wa  kipindi  cha  mapunziko.
Hakimu   Mkuu  wa  Mahakama  ya  Mwanzo   Mjini Mbeya, Mhe. Onesmo  Zunda akizungumzia  kuhusu uzoefu wa usikilizaji  kesi za watoto  zinazohusiana na  madai  alisema  amekuwa akisikiliza kesi za ndoa na talaka nyingi  kutoka  vijijini  kuliko mjini.
“Kuna   changamoto  katika  kusikiliza kesi  hizi. Miongoni mwa changamoto tunazokabiliana  hizo ni mgawanyo wa mali hasa pale inapotoa  mtu  anapokuwa amefariki dunia  au wazazi kutengana mmojawapo akiwa  ana fedha au mali au kaoa mke mwingine.  Nyingi hivyo  mgawanyo  wa mali huwa unaleta  malalamiko katika  baadhi ya familia,” alisema Mhe. Zunda.
Alifafanua kwamba  katika kesi  hizo ni Baba anapotaka kubaki na watoto halafu mama hataki. Hata hivyo  anasema  Mara nyingi   mama huwa anataka kubakia na watoto, lakini  baba hataki  kutokana na tabia ya mama.
“Hivyo tunatumia  sheria pale  ndoa  inapotaka kuvunjika  tunachoangalia zaidi  ni maslahi ya mtoto hata kama  mtoto ana umri wa  zaidi ya miaka 7,” anasititiza Mhe.  Zunda.
Akitolea mfano wa  kesi mojawapo, ambapo alisema alitoa maamuzi  kwamba  mtoto  abaki  kwa  baba kwa sababu  mama  alikuwa  na tabia  ya  ulevi. Alisema  uamuzi huo kwa mujibu wa shuhuda za watoto.
Ingawa  kulingana na sheria ya ndoa  ya mwaka 1971 ni jukumu la baba kuwapa watoto matunzo japo  jukumu la kuwalea watoto ni  la wazazi wote. Hatahivyo, mwanamke anatakiwa  achangie katika  kuhudumia watoto. Iwapo  wazazi wametengana amri  ya matunzo hutolewa na  Mahakama ili baba  asiyeishi na mtoto.
 Matunzo  hayo  huwa  ni pamoja  na kutoa  nguo, chakula, kugharamia masomo shuleni na matunzo yataendelea hadi kufikia umri wa miaka 18.
“Licha ya changamoto tunazozipitia tunajitahidi kuzitatua kwa kutumia  sheria ,hakuna rufaa zinazofunguliwa,”alisema Mhe. Zunda.
Mhe. Zunda  alizitaja takwimu   za kesi za ndoa na talaka walizozipokea kwa kipindi cha mwaka huu yaani  Januari hadi Machi 23,mwaka huu, kuwa  26 na hivyo kati ya hizo  11 bado zinaendelea kushughulikiwa na nyingine zinaendelea kufanyiwa  kazi.
Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mwanjelwa, Mhe. Happiness Chuwa, alisema  ili kukabiliana na tatizo la kesi zinazo husiana na watoto ni vema jamii ikiwa ina tabia ya kuwatambulisha watoto na kuandika wosia.  
Kwa mujibu wa Hakimu  Mfawidhi wa Mahakama ya Watoto, iliyopo eneo la  Mahakama ya Kisutu  jijini Dar es Salaam, Devotha Kissoka,  akizungumza wakati wa Wiki ya Sheria iliyofanyika mwaka huu kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam, alisema mtoto akikosa anaweza kupelekwa katika  makao ya watoto.
Ikiwa kuna tatizo, ambalo limeleta mabishano kuhusu mtoto  baba yake au wazazi wake ni wakina nani? Mahakama hiyo inatoa amri  Mkemia Mkuu wa Serikali kufanya vipimo vya utambuzi (DNA testing).
Alizitaja  takwimu zinazohusu kesi za madai katika Mahakama  hiyo za kipindi cha   mwaka 2016 ni 154 na katika kipindi cha mwaka 2015 zilikuwa kesi 19.
Hakimu huyo alifafanua kwamba sababu ya kuongezeka kwa kesi hizo ni hali ya uchumi, hivyo  hali hiyo imetokea kwa watoto walio nje ya ndoa.
Alisema Mahakama hiyo, pia huwa  inasikiliza kesi za jinai  mfano wizi wa kutumia silaha,  kujeruhi  na kuua.
Mhe.  Kissoka  aliongeza kwamba ieleweke kwa mujibu wa Sheria, mtoto aliyechini ya umri wa miaka kumi hawezi kutenda kosa la jinai.
Desemba 5, mwaka huu Tanzania iliazimisha Maadhimsho ya Kupiga Vitendo vya Ukatili dhidi ya Watoto, mfano kufanyishwa kazi ngumu, kubaka na kuolewa chini ya umri mdogo, au kutopewa fursa ya kupata elimu bora kwa ajili ya maisha yao ya baadae.
Mtoto ana haki ya kupata dhamana katika  mashitaka yote isipokuwa yale, ambayo sheria imemtaka  hayana  dhamana.
Mhe. Kisoka  alizitaja  adhabu ambazo hutolewa kwa mtoto, miongoni mwa adhabu hizo ni kuachiwa kwa masharti kwa kipindi fulani, lakini kisizidi miaka mitatu, adhabu ya kulipa faini, adhabu  ya kuripoti  kwa Afisa Ustawi  wa  Jamii, adhabu ya kupelekwa katika shule maalum.
Pamoja na adhabu hizo mahakama ina uwezo wa kutoa amri mbalimbali kama vile kulipa faini, kuachiwa bila masharti yoyote.
Kutokana  na maoni ya watu mbalimbali  mfumo mmoja wa kisheria  na nguvu za pamoja zitasaidia kupunguza au kutokomeza vitendo vya kikatili na unyanyasaji  dhidi ya watoto.
Hii  inatokana na sababu bado umri wa mtoto bado ni tatizo kwa kuwa mtoto ana weza kuolewa   akiwa na umri  wa miaka 14 au kuoa   wakati huohuo mtu  anaitwa mtoto  akiwa na umri   chini ya miaka 18.
Labels:

Post a Comment

[facebook]

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget