Kitaifa, Kimataifa, Siasa, Michezo na Burudani

MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA ALAANI VURUGU ZILIZOTOKEA KATIKA MKUTANO WA WANAOSEMEKANA KUWA NI VIONGOZI WA CUF NA WAANDISHI WA HABARI


331 

Nimesoma na kuona katika vyombo mbalimbali vya habari kuhusu vurugu zilizotokea tarehe 22 Aprili, 2017 katika hoteli ya Vina, Mabibo hapa Dar es salaam, zinazosemekana kuhusisha wanachama wa CUF.

Ni ukweli usiopingika kuwa, suala la mgogoro wa uongozi katika chama cha CUF lipo mahakamani, lakini nikiwa msimamizi wa Sheria ya Vyama vya Siasa na kutambuliwa na jamii kuwa ni mlezi wa vyama vya siasa; nimelazimika kuwasihi wadau wa siasa hususani wanachama wa chama cha CUF, kutambua kwamba, kuwapo kwa shauri mahakamani siyo fursa ya kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani, kwani jambo hili ni uvunjifu wa sheria na linaleta sura mbaya kwa jamii.

Hivyo, ninalaani vurugu hizo, ambazo zilionekana kuvunja amani na utulivu na watu kuumizwa, tofauti na tunu zetu za taifa za amani na utulivu. Pia, nawaasa wanachama wa CUF pamoja na tofauti walizonazo, madhali masuala haya yapo mahakamani hebu tuheshimu utawala wa Sheria.


Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na hata Jeshi la Polisi lipo kushughulikia malalamiko yoyote yanayohusu uendeshaji na shughuli za chama chochote cha siasa. Hivyo, hakuna haja ya wanachama wa chama cha CUF kukiuka taratibu za kuendesha chama hicho au kujichukulia Sheria mkononi.

Aidha, ninaviasa vyama vya siasa kuelewa kuwa havipo juu ya Sheria, vinapaswa kuheshimu na kufuata Sheria za nchi, ikiwamo kutunza amani na utulivu tulionao.

Mwisho, ninaomba vyombo vya ulinzi na usalama katika nchi yetu kulifanyia kazi tukio hilo, ili wahusika wafahamike na kuchukuliwa hatua za kisheria. Kwa upande wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inayosimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa, haitasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria.


                                              Jaji Francis S.K. Mutungi                                
MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA
24 Aprili, 2017
Labels:

Post a Comment

[facebook]

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget