
Na Benny Mwaipaja, WFM-Dodoma
Wizara ya Fedha na Mipango
imesema kuwa waliokuwa wafanyakazi wa Hoteli ya Seventy Seven ya mkoani
Arusha, walioachishwa kazi mwaka 2000, wameshalipwa mafao yao kwa
mujibu wa sheria na taratibu hivyo hawastahili kudai malipo yoyote ya
nyongeza.
Hayo yameelezwa Bungeni mjini
Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango (MB), Dkt. Ashatu Kijaji
alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maaluum (CCM)
Arusha, Mhe. Catherine Magige aliyetaka kujua ni lini Serikali itawalipa
mafao waliokuwa wafanyakazi wa hoteli hiyo.
Mhe. Magige aliliambia Bunge kuwa
waliokuwa wafanyakazi wa hoteli hiyo ambao waliachishwa kazi mwaka
2000, hawajalipwa mafao yao hadi sasa.
Akijibu swali hilo, Dkt. Kijaji
alisema kuwa katika zoezi la ulipaji wa mafao kwa wafanyakazi hao
Serikali ililipa Sh. 217,366,296 mwezi Januari, 2000 ambapo baadae
walipokea malalamiko kutoka kwa wafanyakazi hao kuwa wamepunjwa.
“Serikali baada ya kupokea
malalamiko hayo, ilihakiki na baada ya kujiridhisha mwezi Agosti, 2000,
ilitoa idhini ya kulipa tena kiasi cha Sh. 273, 816, 703 kwa ajili ya
mapunjo ya mishahara na mafao ya wafanyakazi hao” aliongeza.
Hata hivyo, Mhe. Magige
hakuridhishwa na majibu ya Dkt. Kijaji na alipopewa nafasi ya kuuliza
swali la nyongeza alisema kuwa Serikali imewalipa wafanyakazi hao awamu
ya kwanza tu na hawakupewa nyongeza yoyote licha ya kuwasilisha
malalamiko hayo.
Mhe. Magige aliongeza kuwa Wizara
ya Fedha ilishawahi kwenda kufanya uhakiki na kubaini kuwa kulikuwa na
mapungufu, na Serikali iliipa jukumu la kusimamia malipo hayo Wizara ya
Maliasili na Utalii ambapo mpaka sasa bado haijalipa.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri
wa Maliasili na Utalii (MB), Mhe. Ramo Makani aliliomba Bunge limpe muda
wa kufuatilia jambo hilo kwa ukaribu ili aweze kutoa majibu sahihi.
Post a Comment