
Na Alex Mapunda, Ruvuma
KATIBU wa timu ya Daraja la Pili,
The Mighty Elephant Fc toka Songea Rajabu Dau, amesikitishwa na viongozi
wa Shirikisho la soka hapa nchini TFF kwa kushindwa kupokea simu yake
zaidi ya mara nne pindi anapowapigia ili kuulizia kuhusu Rufaa yao
kuhusu upangwaji wa Matokeo kati ya Timu ya Mawenzi dhidi ya Saba Saba
zote za Morogoro.
Dau amesema kila akiwapigia simu
TFF simu zao zinaita bila Majibu, suala ambalo linaleta mashaka kwa kuwa
rufaa yao toka walipopeleka ina takribani miezi Miwili na TFF wako
kimya hadi leo wakati wao walifuata Taratibu zote za kukata rufaa
zilizowekwa na TFF.

“TFF wanatukosea, napiga simu ya
Katibu Mkuu wa TFF Selestine Mwesigwa hapokei, Eliud Mvela naye hapokei
simu. Kwanini wanakaa Kimya wakati Rufaa walishapokea na uthibitisho
walishanipa?
Mbona rufaa za timu kubwa
wanazifanyia maamuzi mapema? Au sisi kwa kuwa tupo ligi daraja la pili
hatuna haki?, TFF naomba watume majibu ya rufaa yetu, kabla hatujafanya
maamuzi magumu. ”
“Sisi tulikata rufaa kuhusu
kupinga matokeo ya Sabasaba na Mawenzi, matokeo ambayo yalipangwa na
chama cha soka mkoa wa Morogoro ili kuipandisha timu moja kwa nguvu.
Tuna sauti ya dakika 23 ya kikao
cha siri ambacho kiliwakutanisha viongozi wa soka Morogoro, viongozi wa
SabaSaba pamoja na Mawezi ambapo wote walikubaliana Sabasaba acheze
chini ya kiwango ili Mawenzi apate pointi tatu kitu ambacho ni kinyume
cha sheria na taratibu za mpira wa miguu”
“ Lakini baada ya Mawenzi kupata
pointi Tatu toka kwa Sabasaba, kwenye kikao hicho Mwenyekiti wa Chama
cha Soka Morogoro aliahidi kuisaidia Saba Saba isishuke daraja kwa
kutumia fedha. Katika kikao hicho walikuwepo hadi viongozi wa Serikali
na sauti zao zimesikika” alisisitiza Dau.
Lakini taarifa toka kijiweni kwa
wadau wa soka wao wanasema TFF wanashindwa kutolea uamuzi kuhusu suala
la The Mighty Elephnt Fc kwa kuwa Uchaguzi umekaribia na Chama cha Soka
cha Morogoro ni moja ya Kambi muhimu upande wa Malinzi.
Timu ya Mawenzi, Sabasaba na The
Mighty Elephant wote walikuwa kundi moja katika ligi daraja la pili
ambayo imemalizika hivi karibuni.
Post a Comment