Washambuliaji wa Yangu Amissi AmissiTambwe na Obrey Chirw |
WASHAMBULIAJI wa Yanga, Mrundi Amissi Tambwe na Mzambia, Obrey Chirwa hawatasafiri kwa ajili ya mchezo dhidi ya Njombe Mji mwishoni mwa wiki.
Wawili hao wote walianza mazoezi mepesi jana Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam chini ya uangalizi maalum wa Daktari, lakini mapema tu imeonekana hawatakuwa tayari kwa mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Hivyo wote, Tambwe na Chirwa wameondolewa rasmi kwenye programu ya kocha Mzambia, Geroge Lwandamina ya mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya wenyeji Njombe Mji Jumapili Uwanja wa Saba Saba.
Pamoja na hao majeruhi wengine Yanga SC, ni kipa Benno Kakolanya na viungo Hussein Akilimali na Geoffrey Mwashiuya ambao wote tayari wameanza mazoezi mepesi.
Yanga wanatarajiwa kusaka ushindi wa kwanza Jumamosi katika jitihada za kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu watakapokuwa wageni wa timu iliyopanda Daraja msimu huu, Njombe Mji.
Ikumbukwe mabingwa hao wa Ligi Kuu, waliuanza msimu mpya vibaya baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Lipuli ya Iringa iliyopanda Ligi Kuu msimu huu pia.
Kwa ujumla Ligi Kuu itaendelea mwishoni mwa wiki kwa timu zote 14 kujimwaga viwanjani kusaka pointi za mapema.
Mechi nyingine za Jumapili; Singida United watakuwa wenyeji wa Mbao Uwanja wa Namfua, Mtibwa Sugar wataikaribisha Mwadui Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro, Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Lipuli wataikaribisha Stand United Uwanja wa Samora, Iringa na Mbeya City watakuwa wenyeji wa Ndanda Uwanja wa Sokoine.
Awali ya hapo, Jumamosi Azam FC watakuwa wenyeji wa Simba Uwanja wa Azam Complex, Chamazi na Tanzania Prisons wataikaribisha Maji Maji ya Songea Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Post a Comment