Na Tiganya Vincent, RS-Tabora
23
Septemba 2017
SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imeagizwa kutafutwa
na kuletwa Mkandarasi na Mshauri wa Mkandarasi aliyehusika na ujenzi wa Choo
katika Shule ya Sekondari ya Milambo na kusababisha hasara ya shilingi milioni
50.
Agizo hilo limetolewa jana mjini hapa na Mkuu
wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa ziara yake ya kukagua miradi
mbalimbali inayotekelezwa na Mradi wa Miombo ikiwemo ujenzi wa majiko ya kisasa
yanayotumia kuni kidogo na mengine gesi
ya chooni.
Alisema kuwa haiwezekani Serikali itumie
fedha nyingi hizo kisha choo kititie kwa muda mfupi toka kilipojengwa mwaka
2013.
“Mkandarasi huyo aliyejenga hata kama
mnavyosema kuwa ameshastaafu ,nataka ndani ya wiki moja aje na maelezo ofisini
kwangu juu ya nani anabeba hii hasara ya jengo kutitia muda mfupi baada ya
kukamilika” alisisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Mwanri alisema kuwa Mshauri huyo ambaye
ametajwa kwa jina moja la Kuya na aliyekuwa Mkuu wa Shule hiyo ambaye hivi sasa
yuko Urambo na Mkandarasi ni lazima wapeleke maelezo juu ya utaratibu mzima
ulitumika katika ujenzi huo.
Alisema kuwa kitendo cha jengo hilo kutitia
kimezalisha hasara nyingine ya milioni 18 ambazo Mradi wa Miombo ulikuwa
umejenga mtandao wa gesi kwa ajili ya kusafirisha hadi katika jiko la shule
hiyo ili liweze kupunguza gharama ya matumizi ya kuni.
Mwanri alisema mradi huo umeshindwa
kufanyakazi kwa sababu ya ukosefu wa malighafi ya uzalishalishaji wa gesi kwa
matumizi ya jikoni.
Alimwaagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa
ya Tabora kuhakikisha anamtafuta popopte alipo aliyekuwa Mkandarasi na Mshauri
wake na kumleta ili aweze kueleza kuwa hiyo hasara nani anaibeba.
Mwanri alisema asipokuja kwa hiari yake
atalazimika kutumia Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama
kumsaka na kumleta ili ajibu hoja ya kusababishia hasara Serikali.
Aidha Mkuu wa Mkoa huyo alimwagiza Mkuu wa
Shule ya Sekondari ya Milambo kuhakikisha anasimamisha mara moja matumizi ya
Choo hicho kilichotitia ili kisije kinasababisha maafa kwa wanafunzi.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa wa
Tabora amewaagiza viongozi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Tabora na
Mkurugenzi Mteandaji wa Manispaa ya Tabora kuhakikisha wanakarabati choo cha
wasichana ambayo kimesababisha kuzagaa kwa maji taka na kutishia afya za
wanafunzi.
Alisema kuwa ndani ya wiki moja kama atakuta
kazi hiyo haijatekelezwa atalamizika kuwachukulia hatua Mwalimu Mkuu na
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Tabora kwa kushindwa kujali afya za
wanafunzi.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora yuko katika kutembelea
shughuli mbalimbali zinazofadhiliwa na Mradi wa Miombo ambayo ni pamoja na
ujenzi wa majiko ya kisasa yanatumia kuni kidogo, ufugaji nyuki, ufugaji kuku,
matumizi ya gesi ya kinyesi kwa ajili ya kupika na mingine mingi.
Post a Comment