Kitaifa, Kimataifa, Siasa, Michezo na Burudani

Ripoti ya Makinikia ya Almasi na Tanzanite kutua Bungeni kesho


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, kesho anatarajiwa kukabidhiwa taarifa za kamati mbili zilizoundwa na Bunge katika Mkutano wa Saba wa Bunge la 11 kuhusu na makinikia ya almasi na biashara ya madini ya tanzanite.

Kwa mujibu wa taarifa za bunge hafla fupi ya makabidhiano hayo itafanyika katika viwanja vya bunge na viongozi wa kitaifa watakuwepo. Kabla ya Waziri Mkuu kukabidhiwa taarifa hizo, kamati hizo mbili zitakabidhi taarifa zake kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye naye atakabidhi kwa Waziri Mkuu.

Taarifa hizo mbili zinazosubiriwa kwa makini hasa baada ya taarifa za kamati zilizoundwa na Rais John Magufuli kuibua makubwa katika makinikia kwenye makontena bandarini. Kamati hizo maalumu zote zilikuwa na idadi sawa ya wabunge ambao ni tisa na zililenga kushauri juu ya mfumo bora wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa biashara ya madini ya almasi na Tanzanite hapa nchini.

Kamati iliyohusu almasi ikiongozwa na Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu ilitajwa kabla ya kuhitimisha shughuli za Bunge la Bajeti. Spika Ndugai aliunda kamati hiyo kupitia Waraka wa Spika namba 3 wa mwaka huu, na kusema: “Kamati hii itatathmini mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya almasi nchini kisha kuandaa mapendekezo mahsusi kwa ajili ya kuishauri Serikali kuhusiana na uendeshaji bora wa biashara ya madini hayo nchini,” alisema.

Uundaji wa kamati hizo umefanyika kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli katika kukabiliana na ‘wizi’ wa mali asili za taifa. Wakati akiunda Kamati hizo alisema pia kwamba ilitokana na pendekezo la Rais Magufuli la kuunda Tume ya kuchunguza na kufuatilia madini ya almasi alilolitoa Juni 12 mwaka huu alipohudhuria mkutano wa kupokea Taarifa ya Kamati yake ya Pili ya Kuchunguza Masuala ya Kiuchumi na Kisheria kuhusu usafirishaji wa makinikia, Kamati ya Profesa Nehemia Osoro na pia kutokana na hoja aliyoitoa wakati akikabidhiwa ripoti ya makinikia.

Wajumbe wa Kamati hiyo ni Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Dk Immaculate Sware Semesi, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Shally Raymond, Mbunge wa Tumbe (CUF), Rashid Ali Abdallah, Mbunge wa Iramba Mashariki (CCM), Allan Kiula, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Restituta Mbogo na Mbunge wa Wawi, Ahmed Juma Ngwali (CUF).

Wengine ni Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM), Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka (CCM) na Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Zungu ambaye ni Mwenyekiti. Kamati zote mbili ya almasi na Tanzanite zilitakiwa kuanza kazi Julai 10, na Kituo Kikuu cha kazi kilikuwa katika Ofisi ya Bunge hapa Dodoma.

Aidha, alisema hadidu za rejea za kamati ya almasi ilikuwa ni kuchambua taarifa za Tume na Kamati mbalimbali zilizowahi kuundwa na Serikali kwa ajili ya kushughulikia mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya almasi nchini na kuona Mapendekezo yake na namna yalivyotekelezwa na Serikali.

Nyingine ni Kutathmini mfumo uliopo wa uchimbaji, usimamizi na udhibiti wa biashara ya madini ya almasi nchini na kubainisha manufaa ambayo Serikali inapata kutokana na uwekezaji uliopo katika madini hayo na kubainisha na kushauri kuhusu utaratibu bora unaoweza kutumika katika kusimamia uwekezaji, uchimbaji na biashara ya madini ya almasi nchini.

“Hadidu nyingine ni kushughulikia jambo jingine lolote linalohusiana na mfumo wa uchimbaji, usimamizi na udhibiti wa madini ya almasi nchini,” alisema Kamati ya ufuatiliaji wa uchimbaji wa madini ya Tanzanite yenyewe ilipewa kazi ya kuchakmbua mkataba kati ya shirika la taifa la uchimbaji wa madini Stamico na Tanzania One (TML) na kubainisha faida na hasara kutokana na ubia uliopo. Aidha kamati hiyo pia iliangalia mfumo wa uchimbaji na udhibiti.
Labels:

Post a Comment

[facebook]

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget