
Na Jacquiline Mrisho
Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mhe.
Shaibu Ndemanga amewataka wazazi kuacha tabia ya kuiachia Serikali na
mashirika binafsi kuwawezesha vijana na badala yake washiriki kuwasaidia
vijana hao ili waweze kujitegemea.
Ameyasema hayo wakati akizungumza
na waandishi wa habari kuhusu nafasi ya Serikali katika kusaidia
maendeleo ya vijana waliomaliza mafunzo ya ufundi chini ya Mradi wa
Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) unaoratibiwa na Shirika la Plan
International.
Ndemanga amesema kuwa mradi huo
umeleta mabadiliko makubwa kwa vijana katika eneo hilo kwani
wamefundishwa sio tu mafunzo ya ufundi bali pia ujasiriamali, namna ya
kuweka hisa, kujiwekea fedha kwa ajili ya matumizi ya baadaye pamoja na
masuala ya kodi lakini tatizo linalojitokeza ni wazazi kuwaachia
Serikali na wadau wengine kushughulikia kila kitu.
“Changamoto ni nyingi katika
kusaidia vijana hasa ambao tayari walishapata mafunzo kwa sababu wazazi
wakishafahamu kuwa vijana wao wako chini ya mradi basi wanawaachia mzigo
wote Serikali na wadau mbali mbali hivyo nawasihi wazazi wawasaidie
vijana wao katika kujitafutia ajira”.alisema Ndemanga.
Ametoa rai kwa vijana kujitokeza
kwa wakati pindi miradi hiyo inapotokea kwa sababu wengi wao wamekuwa
wakichelewesha kuleta maombi hayo mpaka muda wa mafunzo unafika hivyo
kwa kuwa mafunzo hayo hufanyika kwa muda maalum, vijana wanatakiwa
wajitokeze mapema kwa idadi kubwa.
Aidha, Ndemanga amewataka vijana
waliopata mafunzo kuwafundisha wenzao na pia wanaojiajiri wakumbuke
kuwaajiri vijana wengine ili kupunguza mrundikano wa vijana wanaozagaa
mitaani bila kuwa na kazi za halali.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti
Maalum, Mhe. Hamida Mohamed amekabidhi cherehani mbili kwa vijana
wawili waliomaliza mafunzo ya ufundi chini ya mradi huo ikiwa ni njia
mojawapo ya kuhamasisha ushiriki wa wazazi katika kuwakomboa vijana hasa
kwenye masuala ya kiuchumi.
“Mradi huu umetusaidia sana
kuwaona vijana wenye mazingira magumu hasa walemavu na kufahamu matatizo
yao hivyo kutufanya sisi viongozi wa Serikali kufahamu namna ya
kuwasaidia huku tukisaidiana na wadau mbalimbali”, alisema Mhe. Hamida.
Mradi huo wa miaka mitatu 2015
hadi 2018 unatekelezwa kwa ushirikiano wa mashirika ya VSO, CCBRT, VETA,
UHIKI, CODERT pamoja na Serikali ya Tanzania huku ukiratibiwa na
Shirika la Plan International chini ya ufadhili wa Umoja wa Nchi za
Ulaya (EU).
Post a Comment