
Na: Lilian Lundo
Kikosi cha Makomandoo wa Jeshi la
Wananchi Tanzania (JWTZ) kitapamba maadhimisho ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar yatakayoadhimishwa Aprili 26, mwaka huu Mjini
Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa
na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana
na Watu Wenye Ulemavu Jenista Mhagama maadhimisho hayo yatafanyika
katika uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma ambapo mgeni Rasmi atakuwa Rais
Dkt. John Pombe Magufuli.
Taarifa ya Waziri Mhagama ameteja
shughuli zinazotarajiwa kufanyika siku ya Muungano kuwa ni gwaride la
heshima lililoandaliwa na vikosi vya ulinzi na usalama (JWTZ,JKT,
Polisi na Magereza), maonyesho ya kikosi cha Makomandoo, onesho la Mbwa
na Farasi waliofunzwa.
Aidha, Mhagama aliongeza kuwa
mambo mengine yatakayofanyika ni gwaride la uzalendo la wanafunzi wa
shule za sekondari za Dodoma, burudani za vikundi vya ngoma za asili
kutoka Dodoma na Zanzibar Yamoto Band, Mchungaji Zayumba, Jacob Beats,
Mwenge Jazz Band na Mgosi Maturumbeta.
“Kauli mbiu ya sherehe za kutimiza
miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni Miaka 53 ya
Muungano; Tuulinde na Kuumarisha, Tupige Vita Dawa za Kulevya na Kufanya
Kazi kwa Bidii,” alifafanua Jenista Mhagama.
Hata hivyo ametoa wito kwa
wananchi wote nchini kusherehekea siku hiyo muhimu kwa kudumisha amani,
upendo, umoja na mshikamano kwa maendeleo ya nchi.
“Ninaomba kuchukua nafasi ya pekee
kuwaomba wananchi wote waliopo Dodoma kujitokeza kwa wingi uwanja wa
Jamhuri siku hiyo ya Jumatano tarehe 26 Aprili 2017 kuanzia saa 12:00
asubuhi ili kusherehekea kwa pamoja maadhimisho hayo muhimu kwa nchi
yetu,” alisema Jenista Mhagama.
Maadhimisho ya Muungano
yanafanyika kwa mara ya kwanza Mjini Dodoma Tangu Taifa Letu lipate
uhuru na kutangazwa kuwa Makao Makuu.
Post a Comment