
Na Suleiman Msuya,
Lindi
MBUNGE wa Jimbo la
Mchinga mkoani Lindi, Hamidu Bobali amesema kitendo cha Serikali kulazimisha
mapato ya halmashauri kukusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kitaua
halmashauri nchini kwa kukosa mapato.
Bobali aliyasema hayo
wakati akichangia bungeni Bajeti ya Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora na
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ambayo
imewasilishwa na mawaziri husika.
Alisema uamuzi wa
Serikali kuu kukusanya mapato ambayo yanapaswa kukusanywa na halmashauri
utaathiri ufanisi katika ofisi hizo na kukwamisha miradi mbalimbali.
Alisema Serikali kuu
kupitia TRA ilitangaza kukusanya kodi ya majengo ambapo matokeo yake ukusanyaji
katika Manispaa ya Kinondoni umeshuka kutoka lengo la sh, bilioni 29 hadi sh.
bilioni 4.
Mbunge huyo alimtaka
waziri husika kutafakari kabla ya kuchukua uamuzi ambao anapatiwa na mawaziri
wenzake akitolea mfano ushauri wa kukubali kodi ya majengo ikusanywe na TRA.
Bobal alisema
amechunguza katika nchi mbalimbali ambazo zinaendeshwa kwa mifumo inayofanana
na Tanzania lakini hazikusanyi fedha kwa mfumo huo.
“Mapato hayakusanywi
ipasavyo kutokana na TRA kuingilia mamlaka ambazo si zake na sijui kwanini
waziri wa Tamisemi alivyoshauriwa hakushirikisha ushauri kutoka nje leo hii
mapato yanakosekana na dalili za kufa kwa halmashauri zipo,” alisema.
Aidha, mbunge huyo
amehoji ni vigezo gani vinatumika kwa wakuu wa wilaya kuondoa Serikali za
Vijiji madarakani akitolea mfano mkuu wa wilaya ya Dodoma hivi karibuni
aliagiza mwenyekiti aondoke na kuhoji je hayo ni maagizo ya Rais.
Mbunge huyo aliomba
Serikali kuwapatia watumishi wa idara ya afya ambapo alibainisha kuwa vipo
vituo vinne vipya ila havina wafanyakazi.
Bobali alisema pamoja
na agizo la Rais John Magufuli ambalo alilitoa katika ziara yake ambayo
aliifanya katika mkoa huo bado utekelezaji umeshindika.
Aidha, alisema mkoa wa
Lindi unakabiliwa na uhaba wa walimu jambo ambalo linachangia wanafunzi kufeli
katika mitihani kuanzia msingi na sekondari.
Kwa upande mwingine
mbunge huyo ameitaka Serikali kuachana na mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii
(Tasaf) kama hauwezi kufikia jamii kubwa zaidi.
Alisema Tasaf
inapatikana katika tarafa chache akitolea mfano katika jimbo lake ambapo katika
tarafa nne ni tarafa mbili zinapata.
Aidha, ameitaka Tamisemi
kukemea baadhi ya wakurugenzi ambao wameonesha kushindwa kuendana na kasi ya
utumishi wa umma kutokana na kukosa mafunzo.
Post a Comment