Kitaifa, Kimataifa, Siasa, Michezo na Burudani

MSIWATOZE KODI YA MAJENGO WAZEE WA MIAKA 60-MAJALIWA


MAJALIWA TRA CHATO CUE IN


*Ataka TRA wafanye sensa ya majengo kwenye miji
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka maafisa wa Mamlaka ya Kodi ya Mapato nchini (TRA) wakusanye kodi za majengo kwa kuzingatia sheria na wasitoze kodi ya majengo wazee wenye umri zaidi ya miaka 60.
“TRA ijipange kukusanya kodi za majengo kuanzia Julai Mosi 2017. Katika kutekeleza jukumu hilo, zingatieni sheria. Tusisikie mnawadai kodi ya majengo wazee wenye umri zaidi ya miaka 60 kwa majengo wanayotumia kama makazi yao,” amesema. 

Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Juni 22, 2017) wakati akizungumza na wananchi na viongozi wa wilaya ya Chato waliohudhuria uzinduzi wa jengo la TRA, wilayani humo, mkoani Geita. 
Waziri Mkuu amewataka maafisa hao wakusanye kodi ya majengo kwenye maeneo ya mjini na siyo vijijini kwani kodi hiyo haiwahusu. “Msiende vijijini. Nyumba za nyasi au za tembe hazihusiki. Tembeleeni nyumba za mijini.  Piteni kwenye mitaa, muainishe aina zote za nyumba zinazostahili kulipiwa kodi. Mkishafanya sensa, wekeni utaratibu wa kuwawezesha wananchi kulipia kodi hizo,” amesema huku akishangiliwa.
Pia amewataka wananchi wanaonunua bidhaa wadai risiti lakini wahakikishe wanapewa risiti yenye kiwango halisi walicholipia.  “Ukipewa risiti uiangalie kama ina kiwango halisi cha fedha uliyotoa. Kuna watu wachache wasio waaminifu wanaamua kukupa risiti lakini imeandikwa bei ndogo kuliko ile uliyolipia, ukitoa laki moja anakuparisiti ya sh 10,000.”
Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo la ghorofa moja, Kamishna Mkuu wa TRA, Bw.  Charles Kicheere alisema ujenzi huo ulianza Julai 12, mwaka jana na ulikamilika Juni 12, mwaka huu. 
“Ujenzi wa jengo hili umegharimu sh. bilioni 1.4 na ulichochewa na ongezeko kubwa la idadi ya walipakodi wa Chato kutoka watu 150 mwaka 2010/2011 hadi kufikia watu 600 mwaka 2016/2017”, alisema. 
Pia alisema wamejenga ofisi hizo ili kuwapunguzia umbali wafanyabiashara wa wilaya hiyo ambao walilazimika kwenda Geita mjini kupata huduma za TRA ambako ni umbali wa zaidi km.120.
Alisema hivi karibuni watakamilisha ukarabati wa ofisi za mikoa ya Mara, Iringa, ikiwemo kujenga ofisi kwenye mikoa mipya ya Simiyu, Katavi, Njombe na Manyara. “Pia tutajenga ofisi kwenye mkoa mpya wa kikodi wa Kahama,” alisema. 
Alizitaja wilaya ambazo ziko mbioni kupatiwa ofisi zake kuwa ni Kondoa, Longido, Bunda na Arumeru. 
Alisema katika mwaka ujao wa fedha, TRA imelenga kukusanya sh. trilioni 17.106 na watahakikisha wanafikia lengo hilo. 
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,            
ALHAMISI, JUNI 22, 2017.
Labels:

Post a Comment

[facebook]

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget