Kitaifa, Kimataifa, Siasa, Michezo na Burudani

Wenye Tatoo Watolewa Hofu Uchangiaji Damu




Na Jacquiline Mrisho

WANANCHI waliojichora alama mbalimbali katika miili yao (Tatoo) wametakiwa kuchangia damu kama watu wengine kwani hakuna uhusiano wa  kisayansi kati Tatoo na uchangiaji damu.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Prof. Mohamed Janabi baada ya kuzuka kwa upotoshaji juu ya watu waliojichora Tatoo kuwa hawaruhusiwi kuchangia damu.

Profesa Janabi amesema kuwa damu inapochukuliwa kwa mwananchi lazima ichunguzwe ili kuonekana kama iko sawa kwa ajili ya kutumia kwa wagonjwa wenye upungufu wa damu hivyo zoezi hilo halijalishi mwananchi ana Tatoo au hana.

“Wananchi wanatakiwa waelewe kuwa kinachoambukiza magonjwa sio Tatoo bali ni wale wadudu waliopo katika damu hivyo tunawashauri wananchi wote waendelee kuchangia damu,”alisema Profesa Janabi.

Alifafanua kuwa jumla ya watoto takribani 150 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa magonjwa ya moyo katika hospitali hiyo hivyo uchangiaji wa damu unahitajika ili kusaidia utekelezaji wa suala hilo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala,   Sophia Mjema amesema kuwa ni jambo la kushukuru kuona watu wanajitolea kwa hiari kutoa damu kwani wamefanya jambo la maana katika kusaidia kuokoa maisha ya wengine.

“Suala la kuchangia damu sio la mtu mmoja pia linatakiwa lifanyike kila siku kwa sababu hakuna mtu anayejua lini ataumwa au kupungukiwa na damu mwilini hadi kupelekea ahitaji damu kwahiyo yatupasa sisi wenyewe tuwe na uhiari wa kuchangia damu,alisema  Sophia.

Nae, Mkurugenzi wa Huduma ya Tiba Shirikishi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Praxeda Ogweyo amesema kuwa kwa siku Hospitali hiyo inapokea jumla ya lita 50 mpaka 60 wakati mahitaji ya hospitali yanayotakiwa ni lita 100 mpaka 120 kwa siku hivyo utoaji damu bado ni changamoto kwa wananchi.

“Hospitali inajitahidi kutoa elimu juu ya umuhimu wa kuchangia damu ambapo tumeunda timu kwa ajili ya kuzunguka kwenye maeneo mbali mbali nchini ili kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kuchangia damu kwa manufaa ya maisha yetu sote,”alisema  Praxeda.

 Praxeda ametoa rai kwa wananchi, wizara mbalimbali, mashirika, taasisi na shule kufika katika kituo cha kutolea damu cha hospitalini hapo ili waweze kuchangia pia amewataka watanzania kuamini kuwa damu inayotolewa na kitengo hicho ni salama kwa ajili ya matumizi ya wagonjwa.

June,14 ya kila mwaka ni Siku ya Uchangiaji Damu inayoadhimishwa Duniani kote, kwa Halmashauri ya Ilala vituo vinavyotoa huduma ya uchangiaji wa damu ni Mnazi Mmoja, Hospitali ya Taifa Muhimbili,Karume Mchikichini, Hospitali ya Amana pamoja na JKCI.

Labels:

Post a Comment

[facebook]

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget