Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Umoja wa Wavunaji Sao Hill (UWASA)
pamoja na Wadau wa mazao ya miti wamepongeza jitihada za Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli za ugawaji wa malighafi za
misitu kwa wenye viwanda vya mbao.
Akizungumza na waandishi wa
habari leo jijini Dar es salaam, Mwenyekiti wa UWASA, Christian Ahia
pamoja na wadau wa mazao ya miti wamesema kuwa hatua hiyo itawasaidia
katika kuboresha na kupanua soko la mbao hapa nchini.
“Tunaipongeza serikali kwa hatua
nzuri iliyofikia ambapo imetoa vibali 421 kwa wawekezaji wa viwanda vya
kuchakata mbao huko Mafindi mkoani Iringa, ukilinganisha na vibali
1,000 vilivyokuwa vimetolewa awali kwa watu ambao hawakuwa na
wawekezaji halali wa mbao” alisema Ahia.
Naye, Katibu Mkuu wa UWASA,
Dkt. Bazil Tweve alisema kuwa, serikali ina misitu zaidi ya 15 nchi
nzima, ambapo msitu wa Sao hill unazalisha asilimia 95 ya mbao zote
zinazotumika nchini, hali ambayo ilisababisha uhaba wa malighafi
katika viwanda vya kuchakata mbao kwa vile baadhi ya wavunaji hawakuwa
na sifa na vigezo vya kufanya shughuli hiyo.
“Serikali ilifanya upembuzi yakinifu
na kutoa vibali 421 kwa viwanda vya kuchakata mbao, tunaishukuru
serikali na kuipongeza kwa hatua hii muhimu ya kuona tija ya viwanda na
sisi tunaahidi kufanya shughuli zetu kwa kufuata taratibu na sheria
zilizowekwa alisema Dkt Tweve.
Hapo awali kabla ya upembuzi yakinifu
wa kubaini wawekezaji halali wa kuchakata mbao, kulikuwa na uhaba wa
malighafi ambao ulisababishwa na utaratibu usiofaa wa ugawaji wa
malighafi hizo.
Licha ya pongezi hizo kwa serikali
UWASA imesema inakabiliwa na changamoto za masoko ya mbao zinazochakatwa
nchini, na hivyo wameiomba serikali kuwasaidia kutafuta soko ndani na
nje ya nchi kwa ajili ya kuuza bidha zao.
Aidha, changamoto nyingine
inayowakabili UWASA ni kiwango kikubwa cha kodi zinazotozwa na Mamlaka
ya Mapato (TRA) pamoja na Halmashauri ambapo wameziomba Mamlaka husika
kuwapunguzia kiwango cha kulipa tozo hizo.
Post a Comment