Kitaifa, Kimataifa, Siasa, Michezo na Burudani

Mradi wa PS3 Kuwezesha Halmashauri 93 Kufungiwa Intaneti

Mwagala

1
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Clifford Tandari alipokuwa akifungua mafunzo ya Mfumo ulioboreshwa wa kuandaa Mpango wa Bajeti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa ujulikanao kama ‘planRep’. Mafunzo hayo yamefunguliwa jana Mkoani Morogoro.
3
Meneja Mifumo ya TEHAMA kutoka kwenye Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma, Revocatus Mtesigwa akizungumza kuhusu malengo ya mafunzo ya Mfumo ulioboreshwa wa kuandaa Mpango wa Bajeti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa ujulikanao kama ‘planRep’ wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo jana Mkoani Mororgoro.
…………………………..
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Morogoro.
Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) unategemewa kuziwezesha halmashauri 93 nchini kufungiwa miundombinu ya mtandao (Intaneti) ili kuimarisha utendaji kazi wa Halmashauri hizo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Clifford Tandari ametoa taarifa hiyo jana mjini Morogoro wakati akifungua mafunzo ya Mfumo ulioboreshwa wa kuandaa Mpango wa Bajeti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa ujulikanao kama planRep.
Tandari alisema kuwa kutokana na mabadiliko na kurahisishwa kwa teknolojia, mfumo huo mpya unafanya kazi kwa kutumia mtandao katika kuwezesha halmashauri nchini kuingiza taarifa za mipango na bajeti kwa njia ya mtandao kwa hiyo kufungiwa miundombinu ya mtandao katika halmashauri ni jambo la muhimu na lisiloepukika.
“Kwa kuwa mradi huu utasaidia kupata mitambo ya Intaneti kwa halmashauri 93 basi natoa angalizo kwa watumiaji wa mfumo huo kuwa hakutokuwa na kisingizio cha kutokuwepo kwa mtandao bali tunatarajia matokeo mazuri ya kuongezeka kwa kasi na ari ya kufanya kazi kwa ufanisi,” alisema Tandari. 
Ameongeza kuwa, kwa Halmashauri ambazo hazitapata fursa ya kufungiwa mitambo hiyo wajitahidi kutumia vyanzo vya mapato yake ya ndani kupata fedha za kugharamia ukamilishaji wa mitambo hiyo katika halmashauri zao kwani bila mitandao itawawia vigumu kutumia mfumo huo mpya.
Tandari ametoa rai kwa waboreshaji wa mfumo huo kuangalia namna ya kutumia mfumo hata kwa sehemu ambazo kuna changamoto ya upatikanaji wa intaneti.
Kwa upande wake Meneja Mifumo ya TEHAMA – PS3, Revocatus Mtesigwa amesema kuwa mradi huo umesaidia pia katika eneo la uimarishaji wa miundombinu ya TEHAMA katika ngazi ya mikoa na halmashauri ambapo kwa kushirikiana na Serikali ilifanyika tathmini ya miundombinu (LAN) na mifumo ya TEHAMA katika Sekretarieti za Mikoa 13 na halmashauri 93 zilizo chini ya mradi huu.
“Matokeo ya tathmini hii yaliainisha maeneo yanayohitaji kuboreshwa na tayari tumeanza kuweka miundombinu hiyo ambapo ifikapo Agosti 15 mwaka huu, halmashauri zote zilizo chini ya mradi zitakuwa na mifumo hiyo na ni matumaini yetu kuwa uboreshaji wa mifumo hii utaongeza ufanisi wa mifumo mingine ikiwemo ya GOT-HOMIS, LGRCIS, EPICOR, PLANREP, BEMIS na DHIS2,” alisema Mtesigwa.
Mtesigwa ameongeza kuwa eneo lingine linaloboreshwa ni katika ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mfumo wa kielektroniki (LGRCIS) ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa watumiaji wa mfumo huo kwa lengo la kuimarisha na kuboresha ukusanyaji wa mapato katika halmashauri nchini.
Aidha, kwa kushirikiana na Wakala wa Serikali mtandao (eGA) pamoja na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, mradi umetengeneza tovuti za Sekretarieti za mikoa na halmashauri ambazo tayari zimeshaanza kutumika kwa ajili ya utoaji wa taarifa muhimu na ushirikishwaji wa wananchi.
Labels:

Post a Comment

[facebook]

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget