Kitaifa, Kimataifa, Siasa, Michezo na Burudani

TANGA: HAYAWI HAYAWI SASA YAMEKUWA

Na Agness Moshi- MAELEZO,
Agosti 4, 2017
Ni takribani mwaka mmoja sasa tangu taarifa za kujengwa kwa Mradi wa  Bomba la Mafuta   litakaloanzia Hoima Nchini  Uganda mpaka Tanzania kwenye bandari ya Tanga kuenea kwenye vyombo vya habari ,mitandao ya kijamii na kwa wakazi wa Mkoa wa Tanga ambao ndio wahusika wakuu kwenye mradi huu japo unajengwa kwa manufaa ya mataifa haya mawili kwa ujumla.
 Mradi huu ni moja kati ya miradi mikubwa ambayo Nchi imeweza kutekeleza na utagharimu kiasi cha dola za Kimarekani Billioni 3.5 ambazo ni sawa na Tsh Trillioni 8 kwa fedha za kitanzania. Bomba hili linategemewa kuwa na urefu wa kilometa 1,445 likiwa na uwezo wa kusafirisha mapipa ya mafuta takribani 2,016,000 kwa siku na kutoa ajira zaidi ya 1,000 na vibarua zaidi ya 30,000.
Taarifa hizo zilianza kuwa rasmi,  mnamo tarehe 14 marchi 2016 ambapo Makamu wa Rais wa kampuni ya Total Afrika Mashariki Bw.Javier Rielo alimhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  John Pombe Magufuli kuanza kwa ujenzi wa Mradi  huo.
Nyota njema ya Mradi huu ilianza kuonekana Aprili 24 ya mwaka jana, baada ya aliyekua Waziri wa Nishati na Madini Prof.Sospeter Muhongo kurejea Nchini kutoka Uganda, kuongea na waandishi wa habari kuhusu makubaliano yaliyofikiwa kwa mradi huo.
Bwana Muhongo alisema kuwa, kulikua na mjadala mkubwa wa kuchagua wapi Mradi huo ujengwe na wapinzani wakubwa kwa Tanzania  walikua Kenya lakini kutokana na ubora wa bandari ya Tanga ukilinganisha na bandari nyingine Tanzania ilichaguliwa kunufaika na mradi huu.
 “Bandari ya Tanga ni bora kwa sababu ina kina kirefu ambacho ni zaidi ya mita 23 ambayo ndicho kinayotakiwa Kimataifa kwasababu hiyo kinaweza kufanya kazi mwaka mzima”, alisema Prof. Muhongo.
Chagizo la kuanza kwa mradi huu lilipamba moto   Marchi 28 mwaka huu, baada ya Rais Magufuli kukutana na Mawaziri wa Nishati na Madini wa Serikali zote mbili katika Ukumbi wa Baraza la Mawaziri Ikulu, Jijini Dar es Salaam ili kujadili Maendeleo ya Mradi huo.
Wahenga walisema “Hata Mbuyu ulianza kama Mchicha” wakiwa na maana kila kitu kikubwa kilianza kikiwa kidogo vivyo hivyo Mradi huu ulianza kwa ahadi, makubaliano na hatimaye utekelezaji.
 Mei 21 mwaka huu, Rais Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda Yoweri Kaguta Museveni walitia rasmi saini ya tamko la pamoja ili kukamilisha majadiliano ya vipengele vya mkataba wa utekelezaji wa mradi huo.
Wakazi wa Mkoa wa Tanga, wanahesabu miezi miwili  tangu kusainiwa rasmi  kwa mkataba wa mradi huo utakaowapeleka kwenye mafanikio mbalimbali ikiwemo fursa za ajira , ukuaji wa kasi wa maendeleo , na kuurudishia umaarufu uliopotea wa mji huo.
Ikumbukwe Mkoa huo, ulikua maarufu miaka ya 1960 na 1970 kutokana uwepo   wa viwanda mbalimbali ikiwemo vya uzalishaji katani ambalo ni zao kuu la biashara mkoani humo .Lakini umaarufu huo ulipotea baada ya viwanda hivyo kushindwa kuendelea kuzalisha bidhaa za kutosha kama vile kiwanda cha saruji Tanga.
Licha ya mji huu kupoteza umaarufu bado ni kivutio kikubwa cha Utalii kwani kuna Mapango ya Amboni ambayo yamekua yakiupamba mji huo wenye kilomita za mraba 27,348 na Wilaya 10 ambazo ni Handeni Vijijini, Handeni Mjini, Kilindi, Korogwe Vijijini, Korogwe Mjini, Lushoto, Mkinga, Muheza, Pangani na Tanga Mjini pamoja na majimbo 11 ya uchaguzi ambayo ni Tanga Mjini, Pangani, Handeni, Korogwe Mjini, Korogwe Vijijini, Lushoto, Bumbuli, Mlalo, Kilindi Mkinga na Muheza.
Miaka , na miezi ilipita hatimaye, Mkoa huo umefufua umaarufu wake kupitia Kata ya Chongoleani inayopatikana katika moja ya  Wilaya  mkoani humo, yenye wakazi wapatao  4,737 ,  kwa mujibu wa sensa iliyofanyika mwaka 2012 ,ambao pia karibu nusu ya wakazi wake ni wanufaika wa huduma ya umeme tangu mwaka  2015 kufuatia mpango wa serikali wa usambazaji umeme vijijini.
Agosti  5 mwaka huu (kesho), Tanga inatarajia kurudisha sifa na umaarufu uliopotea kwa zaidi ya miaka takribani  60 kufuatia shughuli za uwekwaji wa jiwe la msingi la Mradi  itakayofanywa na Rais Magufuli na Museveni  ambao utapelekea Nchi zote mbili kwenye mapinduzi  ya kiuchumi  kwa Nchi na wakazi wa  Mkoa huo kupitia fursa mbalimbali hususani kwenye upatikanaji wa Ajira, biashara, chakula ,malazi, bima  na huduma za kifedha.
Kwa Upande wake,  Mkurugenzi Wa Mawasialiano Ikulu Bw.Gerson Msigwa ametoa wito kwa Watanzania   wanaoishi mbali na Mkoa huo kufuatilia matangazo na machapisho mbalimbali yanayotolewa ili kupata taarifa kuhusiana na shughuli hiyo na kwa upande wa wakazi wa Mkoa huo amewasihi kuhudhuria ili waweze kushuhudia tukio hilo la kihistoria.
Ifike wakati Watanzania tujivunie na tumpongeze Rais Magufuli kwa juhudi anazozifanya ili  kuinua kipato  kwa Wananchi kuanzia ngazi ya chini  kwa kutengeneza fursa mbalimbali za ajira, miundo mbinu ili kurahisha shughuli za biashara na Afya kwa ujumla badala ya  kushabikia mambo yasiyo na tija kwa maendeleo.
Kwa wakazi Mkoa Tanga, Serikali imetekeleza ahadi iliyotolewa hivyo basi ni wajibu wao kuunga mkono Mradi huu kwa kutoa ushirikiano hususani katika kufanya kazi kwa bidii, kulinda ili kuzuia uharibifu au kukwamisha shughuli hizo kwa namna yoyote.
Labels:

Post a Comment

[facebook]

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget