Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan
amesema jukumu kubwa la nchi za Afrika ni kuhakikisha zinaweka
mazingira wezeshi ya kuwaendeleza wanawake katika nyanja zote.
Samia ameyasema hayo leo kwenye
Uzinduzi wa Jukwaa la Kuwawezesha na Kuwaendeleza Wanawake Afrika
lililoandaliwa na Asasi ya Graca Machel na kufanyika kwenye Hoteli ya
Hyatt Regency, jijini Dar es salaam.
Makamu wa Rais alisema pamoja na
kuwepo kwa jitihada mbalimbali za kuwaendeleza wanawake bado mazingira
hayampi nafasi mwanamke haswa yule anayeishi kijijini.
Aidha, aliainisha baadhi ya
changamoto hizo kuwa ni pamoja na sheria na sera zilizopo ambazo bado
zinawanyima wanawake fursa ya kumiliki ardhi pamoja na haki ya kurithi
hata kama haki hizo zipo kisheria.
“Hii inatokana na utekelezaji
mbaya wa sheria, unaosababishwa na uwepo wa mianya ya ubaguzi kwenye
kwenye sheria hizo jambo ambalo linakinzana na mfumo rasmi wa kisheria
zilizowekwa,” alisema Makamu wa Rais.
Aidha alisema “Inasikitisha kuona
kuwa ni zaidi ya miaka 20 baada ya Ulingo wa Beijing; kukamilika kwa
utekelezaji wa Malengo ya Milenia; pamoja na kuanza kwa utekelezaji wa
Malengo mapya ya Maendeleo Endelevu ambapo kuna lengo la pekee
linalosimamia masuala ya usawa na kuwawezesha wanawake na watoto wa
kike, bado kuna baadhi wanawake miongoni mwetu ambao wapo kwenye lindi
la umasikini, wanafanya kazi kwenye mazingira magumu; kupata kipato
tofauti na wanaume kwa kazi sawa; kutokuwa na sauti ya kufanya maamuzi
kwenye maisha yao wala maamuzi ya kisiasa; kutokuwa na fursa ya kumiliki
na haki ya kurithi ardhi, kukosa huduma za mikopo, afya na elimu;
Ingawa wamezingirwa na fursa tofauti na mazingira wezeshi bado wanawake
wengi wa Afrika hawachukuliwi kuwa sawa na wenzao wa kiume mbele ya
sheria.
Alimalizia kwa kusema kuwa muda
umefika sasa kwa wanawake kuwa mfano, Kuungana na kuinuana ilikuweza
kumkomboa mwanamke wa Kiafrika na kuhakikisha hamna anayebaki nyuma
kwenye fursa za maendeleo.
Post a Comment