WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ametembelea na kujionea mtambo wa kisasa wa kusafisha dhahabu kwa
asilimia 99 unaomilikiwa na kampuni ya Sunshine Group uliopo katika
kata ya Matundasi wilayani Chunya mkoani Mbeya.
Ametembelea mtambo huo leo
(Jumanne, Agosti 1, 2017) wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi
mkoani Mbeya na kusema kuwa mtambo huo ni wa kwanza kuweza kusafisha
dhahabu kwa kiwango hicho hapa nchini.
Amesema kwa Tanzania kampuni
ya Sunshine Group ndiyo yenye mtambo wa kuweza kusafisha dhahabu na
kufikia asilimia 99 ukilinganisha na makampuni mengine yanayomiliki
migodi.
Pia Waziri Mkuu amesema
Serikali inaendelea kufanya mazungumzo na makampuni mbalimbali kwa ajili
ya kuwekeza katika mradi wa ujenzi wa mtambo wa kuchenjulia makinikia
ili kuweza kusafirisha dhahabu halisi.
Naye Ofisa Madini Mkoa wa
Mbeya, Mhadisi Said Makwama amesema dhahabu inayosafishwa katika mtambo
huo ikipelekwa nje ya nchi inaingizwa sokoni moja kwa moja tofauti na
migodi mingine.
Mhandisi huyo alisema Sheria
mpya ya Madini imesaidia Serikali kupata kodi ya juu itokanayo na
Mrabaha wa asilimia 6 na ‘clearance and inspection fee’ ya asilimia moja
ya thamani ya madini yanayosafirishwa ukilinganisha na mrabaha wa
awali wa asilimia nne.
“Uzalishaji uliofanyika kwa
mwezi Julai tu Serikali imepata mrabaha wa sh. milioni 333
ukilinganisha na sheria ya zamani Serikali ingepata shilingi milioni
191. Sheria mpya imewezesha Serikali kupata mapato zaidi ya sh. milioni
142. Awali ilikuwa inapata sh. milioni 191 kwa gramu 52. 518 kwa mgodi
mmoja wa Sunshine.”
Kwa upande wake mbunge wa
Chunya, Mheshimiwa Victor Mwambalaswa ameiomba Serikali kukubali maombi
ya Kampuni ya Sunshine ya kujenga mtambo wa kuchenjulia mabaki ya
mchanga wa dhahabu wilayani Chunya ili kuweza kuongeza fursa za ajira,
ambapo Waziri Mkuu amesema suala hilo linashughulikiwa.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa
Kampuni ya Sunshine Group Bw Leo Le alisema kampuni ya Sunshine Group ni
ni miongoni mwa makampuni makubwa kutoka nchini China yaliyowekeza
Tanzania, ambapo thamani ya uwekezaji wao ni zaidi ya Dola za Marekani
milioni 100.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, AGOSTI 1, 2017
Post a Comment