Kitaifa, Kimataifa, Siasa, Michezo na Burudani

TATHIMINI KUELEKEA MCHEZO WA KESHO KATI YA SIMBA SC NA YANGA SC NGAO YA HISANI

yanga-na-simba-300x200Na Samuel Samuel
Kwa mara nyingine tena jiji la Dar es salaam linakwenda kushuhudia mtanange wa watani wa jadi kati ya Simba SC na Yanga SC katika dimba la kisasa la uwanja wa Taifa milango ya saa kumi na moja kamili.
Mechi hii inajulikana sana kama Kariakoo Derby ikishika namba tatu barani Afrika kwa umaarufu ikitanguliwa na Al Ahly dhidi ya Zamaleki jijini Cairo nchini Misri na ya pili ni Soweto Derby kati ya Kaizer Chiefs na Orlando Pirates nchini Afrika kusini. Kwa Afrika mashariki na kati ni ya kwanza ikifuatiwa na mashemeji derby ya nchini Kenya ambayo huwakutanisha AFC Leopards na Gor Mahia.
Mechi ya kesho inatarajiwa kuwa na mvuto wa aina yake kwa pande zote mbili ikizingatiwa ndio kwanza wanatoka kwenye kipindi cha usajili na maandalizi ya timu kwa msimu ujao wa ligi . Timu zote zikiwa na maandalizi ya kutosha na kufanya usajili ambao kwa namna moja ama nyingine unapata tafasiri kama ‘ tambo ‘ kwa upande wa pili.
SIMBA SC
Baada ya takribani misimu minne kushindwa kucheza mechi hi ya Ngao ya hisani akiziacha Yanga na Azam kutanua mbawa zao sasa amerudi akiwa na uchu mkali kulinyakua kombe hilo mbele ya mahasimu wao wakubwa Yanga SC hapo kesho.
Maandalizi ya Simba kuelekea mchezo huu pia msimu mpya wa ligi ni kengele tosha ya tahadhari kw wapinzani wao hapo kesho na wengine kwenye ligi. Ni kama mwendelezo wa pale walipoishia msimu uliopita baada ya kufanikiwa kuibuka mabingwa wa kombe la ASFC na kupata tiketi ya kucheza mechi ya kesho jumatano dhidi ya mabingwa wa ligi kuu Yanga SC.
Simba wameweka kambi ya takribani wiki mbili nchini Afrika kusini wakijiandaa kwa mchezo huu . Wakiwa huko waliweza kucheza na moja ya timu ngumu kabisa kwenye ligi ya nchi hiyo Orlando Pirates na Bidvest . Licha ya kutopata matokeo mazuri kwa maana ya ushindi baada ya kufungwa na kutoka sare lakini ni mechi ambazo zitakuwa zimewajenga vyema kiufundi na kisaikolojia kabla ya kuwavaa Yanga SC hapo kesho.
Sanjari na hilo Simba waliweza kupata ushindi wa 1-0 dhidi ya mabingwa wa Rwanda katika tamasha la Simba Day hii yote katika maandalizi yao ya mchezo wa kesho kwa maana dhima ya kuimarisha kikosi chao kimbinu na kiufundi pia kuwajengea hali ya kujiamini wachezaji wao wapya kucheza mbele ya halaiki kubwa ya mashabiki.
Kikosi cha Simba dhidi ya Yanga kesho
Kamati ya usajili ya Simba SC chini ya Mwenyekiti wake Hans Poppe safari hii imefanya kazi nzuri kwa maana ya kusajili wachezaji ambao wakitunzwa vyema wanaweza kuwapa matokeo chanya sio kwa mechi ya kesho tu bali kwa msimu ujao wa ligi kuu na kwenye michuano ya kimataifa wanayokwenda kushiriki mwakani kwenye kombe la Shirikisho.
GOLINI
Safu ya ushambuliaji ya Yanga SC ina kazi ya ziada kesho kugusa nyasi za wekundu hawa wa msimbazi kutokana na aina ya magolikipa walionao. Simba imefanikiwa kusajili magolikipa wote wa Taifa Stars hii ina maana wamezingatia ubora wao na uzoefu kwenye mechi za ndani na za kimataifa . Aishi Manula ambaye Simba wamemsajili toka Azam FC ni golikipa bora mara mbili mfululizo nchini na ana uwezo mkubwa kuipanga safu yake ya ulinzi. Huyu ndie ambaye atasimama kesho kwenye milingoti ya Simba kulingana na uzoefu wake na idadi ya mechi za kirafiki alizodaka. Je kuwazuia washambulia wa Yanga wenye uchu wa mabao?! Muda utaongea.
SAFU YA ULINZI
Joseph Omog anakwenda kupambana na Yanga SC akiwa hana shaka hususani na walinzi wake wa kati. Takribani mechi mbili au tatu kombinesheni ya nahodha Method Mwanjali na Salumu Mbonde imekuwa muhimili wa timu hiyo eneo la kati na bila shaka hao ndio wataanza eneo hilo. Mbadala wa hilo ni kama mwalimu huyo akiamua kuwa na idadi kubwa ya viungo wakabaji ndani ya timu yake akiamua kumuanzisha James Kotei kama sentafu akicheza na Mwanjali na Jonasi Mkude kusimama na Haruna Niyonzima kati . Hii itakuwa plan B kuwadhibiti Yanga kwenye pressing kutokana na ubora wa kiungo chao baada ya ujio wa Paapy Tshishimbi ambaye ameonekana kuwa na uwezo mkubwa kuisukuma timu mbele kwa kasi.
Ni dhahiri Erasto Nyoni mkongwe huyu anaweza kuanza kushoto kama hataamua kumuanzisha Jamali Mwambeleko. Erasto ni mzoefu wa mechi hizi zenye ushindani na anawajua vyema wachezaji wa Yanga . Endapo Lwandamina atamuanzisha Ajibu kama namba saba ina maana huyu ndio atakuwa anakutana na Erasto Nyoni kwenye wing na wanajuana vyema toka timu ya taifa. Kulia ni dhahiri ingizo jipya Ally Shomari ataanza. Amekuwa bora kwa mechi zote alizocheza akionesha kujiamini, kujua majukumu yake ya awali ya kukaba na kusaidia mashambulizi. Wing ya kushoto ya Yanga kama itaanza na Emanuel Martin ambaye hivi karibuni ameonesha uwezo mzuri kwenye kupanda juu kwa kasi na kutoa krosi nzuri, hivyo Omog atahitaji mtu mwepesi wa kuzima mashambulizi hayo.
KIUNGO
Hapa ndipo ulipo moyo wa Simba ambapo na uhakika panamnyima usingizi kocha mkuu wa Yanga SC George Lwandamina ambaye tayari ana rekodi mbaya na mechi ya watani wa jadi akipoteza mechi mbili mbele ya Omog.
Simba imekamilika vyema idara hii. Ni uwezo tu wa Omog na wachezaji binafsi kuamua jinsi gani wataimiliki Yanga eneo hili kama mabingwa hao watakosa umakini.
Usajili wa kiungo Haruna Niyonzima ndani ya kikosi cha Simba ni kama vile umekuja kunoa zaidi makali ya kiungo hicho. Kabla ya ujio wa Haruna, Simba walikuwa wakitamba na ubora wa Jonasi Mkude , Kotei , Mzamiru Yassin , Saidi Ndemla, Shiza Kichuya , na Mohamedi Ibrahimu ambao kwa hakika kwa msimu uliopita waliweza kuibeba vyema timu hiyo.
Licha ya ubora wa viungo hawa kwa mechi kadhaa wameonesha kukosa muunganiko mzuri na safu ya ushambuliaji. Mara nyingi wanashindwa kujenga mashambulizi ya moja kwa moja toka eneo la kiungo licha ya uzuri wa kumiliki mpira.
Yanga itawapasa kuwa makini na Haruna Niyonzima, Mzamiru Yassin , Mohamedi Ibrahimu na Saidi Ndemla eneo la kati . Ni dhahiri Mzamiru na Niyonzima wataanza pia MO Ibrahimu na Ndemla mara nyingi hutumika kama super sub . Hawa wote wana kitu kikubwa cha kufanana; wana uwezo wa kukaa na mpira , kubadili mfumo wa kushambulia , kuvunja muhimili wa ulinzi kutokana dribbling skills zao pia ni wazuri kwenye pasi za mwisho na kufunga hususani Mzamiru na Mo Ibrahimu. Haruna ni passer midfielder kwa zaidi ambaye Yanga watatakiwa kumpa mtu wa kutembea nae ili kuzima mpira.
USHAMBULIAJI
Taarifa zisizo rasmi zinasema John Bocco anaweza kuukosa mchezo huu kutokana majeruhi . Huenda ni ‘ game mind ‘ lakini huyu ndio mtu sahihi kusimama kama mshambuliaji wa kati akitengeneza pacha yake na Emanuel Okwi.
Ubora wa safu ya kiungo ya Simba kwa mfumo wa 4-4-2 ambao Omg anapenda kuutumia , anahitaji strika ambaye muda wote anasimama ndani ya 18 timu inapojenga mashambulizi. Bocco ni bora zaidi katika hili kuliko Mavugo ambaye mara nyingi hurudi sana kati na kujikuta muda mwingine kukosa mashambulizi ya kushitukiza yanayojengwa kwa haraka tokea kwenye wings aidha na mawinga au fullbacks zikipanda.
Kikubwa ni Omog kumjenga vyema winga wake wa kulia Shiza Kichuya kucheza zaidi kama mchezeshaji wa pembeni na sio kulazimisha kufunga hali ambayo kwa mechi za hivi karibu ameonesha kuingiliana sana na mshambuliaji namba mbili ” deep playmaker ” Emanuel Okwi.
YANGA SC
Yanga wanakwenda kwenye mtanange huu wakiwa na hali ya kujiamini zaidi baada ya ujio wa kiungo wao wa chini toka Mbabane Swallows ya Swaziland Paapy Tshishimbi.
Kwa upande mwingine ni mechi ya tahadhari sana kwao baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya mahasimu wao hawa. January mwaka huu wakipoteza kwa matuta nusu fainali kombe la Mapinduzi na mechi ya mwisho mzunguko wa pili ligi kuu.
Ni mechi ambayo wengi wanaichukulia Yanga kama underdog mbele ya Simba kutokana sababu za hapa na pale nyingi zikiwa za kiuchumi na hii inatokana na aina ya maandalizi yake tofauti na misimu ya nyuma pia matatizo yaliyomkuta mwenyekiti wao bwana Yusufu Manji ambae mara kwa mara amekuwa akiifadhili timu katika maandalizi kabambe ya mwanzo wa ligi.
Huo ni mtazamo tu ambao unakinzana kwa uhalisia wa kikosi cha timu hiyo kuelekea mchezo wa kesho.
USAJILI
Yanga wamejitahidi sana kufanya usajili kulingana na mahitaji ya timu kutokana na kiwango chao msimu uliopita.
Ni timu ambayo ilikuwa na idadi kubwa ya wachezaji wakongwe tegemeo ambao kwa namna moja ama nyingine wanaelekea magharibi ya soka lao na wengi wao wakiwa aghali sana kwa kuigharimu timu fedha nyingi.
Msimu huu Yanga wamesajili kwa kuchanganya vijana wadogo na wazoefu ili kupata mseto mzuri kwa malengo ya karibu na mbali . Hali ambayo inampa mwalimu upana katika kikosi chake pia kuwa na uhakika wa kikosi cha muda mrefu.
GOLINI
Ujio wa golikipa mkongwe na mzoefu Youthe Rostand kunawapa jeuri Yanga SC katika mechi ya kesho ambaye anatazamiwa kukaa langoni. Rostand anajua vyema kulilinda lango lake , mrefu kwa maana ya kucheza mipira ya juu na krosi , kupanga walinzi wake , na anaijua vyema safu ya ushambuliaji ya Simba SC kutokana na kuwepo kwenye ligi msimu uliopita akiwa na African Lyon .
Ramadhani Kabwili ni back up ya Rostand endapo hatokuwa sawa kwa mchezo wa kesho au mpaka jioni ya leo pingamizi lake TFF lisipotolewa majibu. Kabwili ni kijana mdogo ambaye amekuzwa vyema kwenye academy za Azam FC pia akiwepo katika kikosi cha Serengeti boys. Ni dhahiri waalimu wa Yanga wamemuandaa vya kutosha kusimama langoni kesho kutokana na kudaka mechi nyingi za kirafiki.
ULINZI
Hili ndio eneo lenye utata kiasi kwa Yanga na ni dhahiri jopo la makocha la Simba wanalipigia mahesabu makali endapo Yanga watashindwa kujipanga vyema .
Kuondoka kwa mlinzi wa kati Vincent Bossou na kusajiliwa Shahibu ‘ Ninja ‘ toka Jang’ombe Boys bado kunawatia wasiwasi mashabiki wa Yanga wakiamini bado safu yao ya ulinzi wa kati si imara kama msimu uliopita alipokuwepo Bossou. Lakini hili kiufundi lina jibu hususani kwa kocha mzoefu kama Lwandamina.
Kesho atahitajika kuujenga ukuta wake kwa kuweka kombinesheni nzuri ya mlinzi mmoja wa kati mwenye uwezo wa ku ‘ command’ defense na mwingine kucheza kama sweeper ili kuhakikisha safu ya ushambuliaji ya Simba na kiungo chao kinakuwa marked muda wote . Kabla na baada ya mpira . Anaweza kumtumia Kelvin Yondani Shaibu au Nadir na Dante.
Walinzi wa pembeni ni dhahiri kulia ataanza na Juma Abdul ambaye anaijua vyema Simba na upande wake kuna kila dalili kukutana na viungo watupu yaani Erasto chini na Mzamiru juu yake . Abdul licha ya ubora kwenye marking lakini pia ni mzuri kwenye dead balls na kusaidia mashambulizi kwenye wings.
Kushoto ni changamoto kwa Lwandamina. Kuna Gadiel Michael na Hajji Mwinyi. Wote ni wazuri kwenye marking na kupandisha timu juu. Ukitazama safu ya kulia ya Simba ambayo itakuwa chini ya Ramdhani Kichuya mchezaji mwenye kasi , nguvu na uwezo wa kushambulia kutokea pembeni , ni dhahiri Lwandamina atahitaji mchezaji mzoefu wa derby na ambaye bila shaka Haji anaweza kuanza na Mbaga kutokea benchi ingawa pia kwa uzoefu wa kukaa timu ya taifa anaweza kuanza pia.
KIUNGO
Kabla ya ujio wa Pappy Tshishimbi Yanga walikuwa bado hawajiamini sana eneo hili kwa kukosa kiungo mkabaji asilia mwenye uwezo wa kuijenga vyema timu kwenye marking na kushambulia.
Ni dhahiri Lwandamina ataanza na Tshishimbi kati huku akisaidiana na Thabani Kamusoko juu huku kulia akicheza Ibrahimu Ajibu na kushoto Emanuel Martin na deep maker akisimama Donald Ngoma pia akiwa na majukumu ya kushambulia sambamba na mshambuliaji wa kati Amisi Tambwe.
Hii inaweza kuwa mipango ya awali ya mwalimu endapo atahitaji kuwadhibiti Simba kati pia akiwa vyema kwenye kushambulia . Kamusoko ni box to box midfielder ambaye anaweza kuelewana vyema na Tshishimbi kuwanyima uhuru viungo wa Simba na kuituliza Yanga kati. Kama mwalimu hatamuanzisha Tambwe ni dhahiri Ajibu atakuwa kati na Rafael Daudi kukaa kulia . Hapa utazidi kuona Yanga walivyokuwa na options za viungo wachezeshaji na washambuliaji ambao wanaweza kuifanya Yanga kuwa na uwiano mzuri wa kujaa kwenye box la Simba pia kulinda mfumo wao wa ulinzi.
Ni mechi ambayo inakwenda kuonesha ubora wa viungo wa timu zote mbili pia safu zao za ushambuliaji na ulinzi.
Kama Lwandamina atatumia 4-3-3 ni dhahiri atahitaji viungo washambuliaji wawili ili kuvunja muhimili wa ulinzi wa Simba chini ya Kotei au Mkude kama viungo wakabaji. Ajibu , Martini na Rafael Daudi pia Kamusoko ndio bunduki za Lwandamina kesho kulinda offensive patterns zake .
Maka Edward ni plan B kwa kocha wa Yanga eneo la kati Juma Saidi akiamua wote japo kuonjesha ladha ya derby kwa dakika kadhaa.
USHAMBULIAJI
Yanga ina safu bora ya ushambuliaji kuliko Simba . Hivyo Omog atahitajika kuwa makini sana kwa safu yoyote ambayo Lwandamina atampangia . Pacha ya Ngoma na Tambwe bado ni tishio kwa Simba ingawa Ngoma toka kutoka majeruhi anaonesha kutokuwa katika kiwango chake bora kabisa.
Lakini pia Lwandamina anaweza kuwatumia Ajibu na Ngoma ili Tambwe aje kama super sub akilenga kumiliki mpira kwenye final third pia kushambulia kwa kasi muda wote . Unapokuwa na Ajibu kama false 10 na Ngoma kati huku nyuma kuna Kamusoko na Tshishimbi ni dhahiri muunganiko wa ushambuliaji kwa njia ya kati unakuwa vyema na timu inaweza kutumia patterns za short passes wakihama box moja kwenda jingine vizuri tu . Ni kiasi cha viungo wa simba kuwa vyema kwenye intercepting na blocking kuzuia ‘ direct play ‘ kwa mfumo huo.
MWISHO
Dakika 90 au matuta ndio mwamuzi wa mwisho katika mchezo huo . Ni mechi ambayo nina uhakikoa pande zote zinakwenda kupata taswira sahihi ya vikosi vyao kwa msimu mpya wa ligi kuu 2017-18.
Wako katika uchambuzi :
Samuel Samuel 
brevis574@gmail.com
Labels:

Post a Comment

[facebook]

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget