Maiti za viroba zapimwa DNA
SIKU mbili baada ya gazeti hili kuripoti kuhusu uwapo wa maiti 15 zilizoopolewa baharini mfululizo katika siku za karibuni, zikiwa zimefungwa ndani ya viroba katika pwani za Dar es Salama na Zanzibar,-
Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP) Simion Sirro, amesema miili hiyo inafanyiwa uchunguzi wa vinasaba (DNA) ili kuwatambua.
IGP Sirro alisema jeshi lake linazo maiti zilizookotwa katika pwani ya Bahari ya Hindi na miili hiyo iko katika hatua ya uchunguzi zaidi.
Akizungumza na ITV jana, IGP Sirro alisema miili hiyo inachukuliwa vinasaba kwa ajili ya utambuzi ili kujua ni raia wa nchi gani.
"Jeshi la Polisi tayari limeshachukua hatua za awali za utambuzi kwa kuchukuliwa vinasaba maiti hizo ili kufahamu ni raia wa wapi na tukishakamilisha kazi hiyo, tutatangaza watu waliopotelewa na ndugu zao kuja kufanya utambuzi," alisema.
Alisema ingawa watu wanadhani kwamba mauaji hayo yamefanywa na Polisi, jeshi lake huwa halina kificho pindi linapokabiliana na wahalifu kwenye mapambano.
Alisema inapotokea polisi ikaua majambazi katika mapigano ya kurushiana risasi, huweka wazi tukio hilo na siyo kwenda kuwatumbukiza baharini.
Mwanaharakati Sheikh Issa Ponda juzi aliitaka serikali kutoa kauli kuhusu jambo hilo ambalo lilifichuliwa na Nipashe kwa mara ya kwanza Jumatatu.
Akizungumza na Nipashe kwa simu juzi, Sheikh Ponda ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu Tanzania, alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakipaza sauti kuhusu uwapo wa mauji ya raia kwenye mikoa ya kusini mwa Tanzania lakini haijasikilizwa.
"Tunapongeza Nipashe kwa habari hii," alisema Sheikh Ponda kwa sababu "imefichua mambo mengi."
"Haya tumeshayasema lakini hakuna aliyetusikiliza. Ni wakati mwafaka serikali ikatoa tamko kwa vile vyombo vya dola vimeonyesha kushindwa kueleza miili hiyo ni ya watu gani na inatoka wapi, (na kibaya) zaidi wanasema wanatambua miili mitatu iliyookotwa ambayo kwa sasa iko Muhimbili."
Sheikh Ponda alisema mauaji hayo ni makubwa na hayajawahi kutokea katika serikali zilizopita, kwa miili kusambaa baharini na wavuvi kuipoa.
Alisema jambo hilo si la kawaida, lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa wala kutolewa taarifa ya kina na serikali kuhusu hali hiyo.
"Jumuiya inaona ni wakati mwafaka kwa serikali kutueleza kwa kuwa vyombo vya dola havijui au havitaki kutoa taarifa juu ya kile kinachoendelea hadi maiti kuokotwa zikiwa ndani ya viroba baharini," alisema.
Kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika vilivyozungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki iliyopita, miili hiyo iliokotwa kwa nyakati tofauti na wavuvi ambao waliwajulisha polisi, waliofika kuichukua.
Kuwapo kwa idadi kubwa ya miili inayoopolewa kutoka baharini au kukutwa fukweni ikiwa imefungwa kama mzigo kumefanya wavuvi na wafanyabiashara wa samaki kaskazini mwa wilaya ya Kinondoni kuingiwa na hofu pia.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Boaz, juzi alikiri kuopolewa kwa miili kwenye fukwe za Bahari ya Hindi ikiwa imefungwa kwenye mifuko maalum inayofanana na viroba.
"Zipo maiti zimeopolewa na wavuvi katika Pwani ya Dar es Salaam, zikiwa ndani ya mifuko zimeshonewa ndani," DCI Boaz alithibitisha.
Alipoulizwa idadi na maeneo zinakotoka na zinakohifadhiwa, alisema: "Hilo waulize makamanda wa polisi wa mikoa ya kipolisi, siwezi kuwa na takwimu hizo."
Alisema zaidi: "Pia kuhusu zinatoka wapi ni mapema sana kujua kwa kuwa zimebebwa na mawimbi ya bahari hadi kuokotwa maeneo husika.
"Bahari ni pana sana na maiti hizo zinasombwa na mawimbi, hatujui zinatoka wapi, ila waulize ma-RPC (makanda wa polisi) wa mikoa husika."
Wavuvi waliozungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki walisema uwapo wa idadi kubwa ya miili hiyo umesababisha baadhi yao kunyamaza wanapoona miili zaidi ikielea baharini.
“Polisi tunawajulisha, wanakuja, wanabeba maiti lakini hakuna siku wametueleza ni za kina nani," alisema mvuvi mmoja wa Kunduchi aliyezungumza na Nipashe kwa sharti la kutotajwa jina gazetini akihofia usalama wake.
"Wavuvi tunafahamiana na ikitokea mwenzetu amekufa au chombo kimezama majini tunafahamu.
"Lakini tangu Agosti mwanzoni tunaokota miili ikiwa imeandaliwa (imefungwa) kabisa na siyo ya wenzetu.”
Wavuvi hao walisema wamepokea taarifa kutoka wenzao wa eneo la Kizimkazi, Zanzibar, kwamba huko nako pia zimeokotwa maiti tano.
Mvuvi mmoja wa Kunduchi alisema mwishoni mwa wiki iliyopita ziliokotwa maiti tano katika eneo la Bongoyo na nne nyuma ya kisiwa cha Mbudya, jijini Darc es Salaam.
Alisema kati ya maiti tisa hizo, moja ilikuwa ya mwanamke na kwamba zilikuwa zimefungwa kamba miguuni, kichwani na tumboni.
Post a Comment