Mwagala
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro,
Clifford Tandari alipokuwa akifungua mafunzo ya Mfumo ulioboreshwa wa
kuandaa Mpango wa Bajeti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa ujulikanao kama
‘planRep’. Mafunzo hayo yamefunguliwa jana Mkoani Morogoro.
Meneja Mifumo ya TEHAMA kutoka
kwenye Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma, Revocatus
Mtesigwa akizungumza kuhusu malengo ya mafunzo ya Mfumo ulioboreshwa wa
kuandaa Mpango wa Bajeti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa ujulikanao kama
‘planRep’ wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo jana Mkoani Mororgoro.
…………………………..
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Morogoro.
Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya
Sekta za Umma (PS3) unategemewa kuziwezesha halmashauri 93 nchini
kufungiwa miundombinu ya mtandao (Intaneti) ili kuimarisha utendaji kazi
wa Halmashauri hizo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro,
Clifford Tandari ametoa taarifa hiyo jana mjini Morogoro wakati
akifungua mafunzo ya Mfumo ulioboreshwa wa kuandaa Mpango wa Bajeti za
Mamlaka ya Serikali za Mitaa ujulikanao kama planRep.
Tandari alisema kuwa kutokana na
mabadiliko na kurahisishwa kwa teknolojia, mfumo huo mpya unafanya kazi
kwa kutumia mtandao katika kuwezesha halmashauri nchini kuingiza taarifa
za mipango na bajeti kwa njia ya mtandao kwa hiyo kufungiwa miundombinu
ya mtandao katika halmashauri ni jambo la muhimu na lisiloepukika.
“Kwa kuwa mradi huu utasaidia
kupata mitambo ya Intaneti kwa halmashauri 93 basi natoa angalizo kwa
watumiaji wa mfumo huo kuwa hakutokuwa na kisingizio cha kutokuwepo kwa
mtandao bali tunatarajia matokeo mazuri ya kuongezeka kwa kasi na ari ya
kufanya kazi kwa ufanisi,” alisema Tandari.
Ameongeza kuwa, kwa Halmashauri
ambazo hazitapata fursa ya kufungiwa mitambo hiyo wajitahidi kutumia
vyanzo vya mapato yake ya ndani kupata fedha za kugharamia ukamilishaji
wa mitambo hiyo katika halmashauri zao kwani bila mitandao itawawia
vigumu kutumia mfumo huo mpya.
Tandari ametoa rai kwa waboreshaji
wa mfumo huo kuangalia namna ya kutumia mfumo hata kwa sehemu ambazo
kuna changamoto ya upatikanaji wa intaneti.
Kwa upande wake Meneja Mifumo ya
TEHAMA – PS3, Revocatus Mtesigwa amesema kuwa mradi huo umesaidia pia
katika eneo la uimarishaji wa miundombinu ya TEHAMA katika ngazi ya
mikoa na halmashauri ambapo kwa kushirikiana na Serikali ilifanyika
tathmini ya miundombinu (LAN) na mifumo ya TEHAMA katika Sekretarieti za
Mikoa 13 na halmashauri 93 zilizo chini ya mradi huu.
“Matokeo ya tathmini hii
yaliainisha maeneo yanayohitaji kuboreshwa na tayari tumeanza kuweka
miundombinu hiyo ambapo ifikapo Agosti 15 mwaka huu, halmashauri zote
zilizo chini ya mradi zitakuwa na mifumo hiyo na ni matumaini yetu kuwa
uboreshaji wa mifumo hii utaongeza ufanisi wa mifumo mingine ikiwemo ya
GOT-HOMIS, LGRCIS, EPICOR, PLANREP, BEMIS na DHIS2,” alisema Mtesigwa.
Mtesigwa ameongeza kuwa eneo
lingine linaloboreshwa ni katika ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mfumo
wa kielektroniki (LGRCIS) ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa watumiaji
wa mfumo huo kwa lengo la kuimarisha na kuboresha ukusanyaji wa mapato
katika halmashauri nchini.
Aidha, kwa kushirikiana na Wakala
wa Serikali mtandao (eGA) pamoja na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, mradi
umetengeneza tovuti za Sekretarieti za mikoa na halmashauri ambazo
tayari zimeshaanza kutumika kwa ajili ya utoaji wa taarifa muhimu na
ushirikishwaji wa wananchi.
Post a Comment