Na Tiganya Vincent
RS-Tabora
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewaonya wamiliki wa maduka ya madawa
ya binadamu na watumishi wa sekta ya afya wanaochukua dawa ambazo
zinapaswa kupelekwa katika Hospitali za Serikali ili kuwahudumia
wananchi na kuziweka katika maduka yao.
Mhe. Majaliwa alitoa kauli hiyo jana Wilayani Sikonge katika mkutano wa hadhara na wananchi katika Kiwanja cha TASAF.
Alisema kuwa vitendo hivyo ndivyo
vimekuwa vikisababisha upungufu wa dawa katika Zahanati, Vituo vya Afya
na Hospitali mbalimbali za Serikali na kufanya baadhi ya wananchi
kuendelea kuteseka na maradhi kwa sababu ya kushindwa gharama za ununuzi
wa dawa katika maduka ya watu binafsi.
Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa
aliwaonya watumishi wa afya na wamiliki hao wenye tabia hizo kuacha mara
moja endapo watabainika kuendesha vitendo hivyo watachukuliwa hatua
kali.
Alisema kuwa Serikali inatumia
fedha nyingi kwa ajili kununua dawa ili zinasaidia kutoa huduma ya
matibabu kwa wananchi wake lakini kuna baadhi ya watumishi wa afya wasio
waadirifu ambapo wamekuwa wakitorosha dawa na kuwauzia wamiliki wa
maduka ya dawa na ksuababisha upungufu katika vituo vya Serikali.
Waziri Mkuu kuwa Serikali haiwezi
kuwavilimia watumishi wa afya wasio waaminifu wanaochukua dawa na
kuzipeleka katika maduka binafsi huku wakisababisha upungufu katika
baadhi ya hospitali za umma.
Alisema kuwa hospitali ni lazima ziwe na dawa za kutosha ili kuepusha usumbufu kwa wananchi.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu
ameikabidhi Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Tabora orodha ya watu
wenye tabia ya kuwarubuni wakulima wa tumbaku na kununua katika mfumo
ambao si rasmi na kisheria (soko huria) na kuwanyonya ili wahojiwe.
Alisema kuwa watu hao kwa muda
mrefu ndio wamekuwa wakiwanyonya wakulima kununua tumbaku zao kwa
vishanda na kuwa fedha ambazo zinazidi kuwakandamiza.
“Nina majina ya watu ambao
wamekuwa wakipita kwa wakulima na kununua tumbakuza wakulima kwa njia ya
vishada ….huku wakiwanyonya kwa kuwapa fedha kidogo nawataka waache
mara moja.” Alisisitiza Mhe. Waziri Mkuu.
Aliongeza “leo siwataji majina yao
lakini nakuachia Mkuu wa Mkoa ili wewe na Kamati yako ya Ulinzi na
Usalama muwaite na kuwahoji na kisha ziwaonye wasiendelee na biashara
hiyo, kama wanataka kuendelea na uuzaji wa tumbaku wahakikishe
wanayopeleka sokoni ni ile waliolima wenyewe na sio ya kununua kwa
wakulima”
Aidha Waziri Mkuu alitoa onyo kwa
watumishi wa umma ambao wamekuwa na tabia ya kugonja wakulima walime
tumbaku na wakisha kuvuna na kukausha wao wanakwenda kununua kwa ajili
ya kuipeleka katika makampuni ya tumbaku.
Alisema mtumishi hakatazwi kulima kulima tumbaku bali atakiwi kununua tumbaku kutoka kwa mkulima.
Waziri Mkuu huyo aliwaagiza
viongozi wa Mkoa wa Tabora kukamata watu wote wanajihusisha na ulanguzi
wa tumbaku ya wakulima na kuongeza kuwa watakamatwa wakiwa na tumbaku ya
ulanguzi ichukuliwe pamoja na chombo cha usafiri kinachotumika
kusafirishia.
Alisema kuwa tumbaku yote inauzwa kupitia vyama vya msingi na kila mtu atauza tumbaku kwa kiwango alicholima.
Post a Comment