Na Agness Moshi- MAELEZO,
Agosti 4, 2017
Ni takribani mwaka mmoja sasa
tangu taarifa za kujengwa kwa Mradi wa Bomba la Mafuta litakaloanzia
Hoima Nchini Uganda mpaka Tanzania kwenye bandari ya Tanga kuenea
kwenye vyombo vya habari ,mitandao ya kijamii na kwa wakazi wa Mkoa wa
Tanga ambao ndio wahusika wakuu kwenye mradi huu japo unajengwa kwa
manufaa ya mataifa haya mawili kwa ujumla.
Mradi huu ni moja kati ya miradi
mikubwa ambayo Nchi imeweza kutekeleza na utagharimu kiasi cha dola za
Kimarekani Billioni 3.5 ambazo ni sawa na Tsh Trillioni 8 kwa fedha za
kitanzania. Bomba hili linategemewa kuwa na urefu wa kilometa 1,445
likiwa na uwezo wa kusafirisha mapipa ya mafuta takribani 2,016,000 kwa
siku na kutoa ajira zaidi ya 1,000 na vibarua zaidi ya 30,000.
Taarifa hizo zilianza kuwa rasmi,
mnamo tarehe 14 marchi 2016 ambapo Makamu wa Rais wa kampuni ya Total
Afrika Mashariki Bw.Javier Rielo alimhakikishia Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kuanza kwa ujenzi wa Mradi
huo.
Nyota njema ya Mradi huu ilianza
kuonekana Aprili 24 ya mwaka jana, baada ya aliyekua Waziri wa Nishati
na Madini Prof.Sospeter Muhongo kurejea Nchini kutoka Uganda, kuongea na
waandishi wa habari kuhusu makubaliano yaliyofikiwa kwa mradi huo.
Bwana Muhongo alisema kuwa,
kulikua na mjadala mkubwa wa kuchagua wapi Mradi huo ujengwe na
wapinzani wakubwa kwa Tanzania walikua Kenya lakini kutokana na ubora
wa bandari ya Tanga ukilinganisha na bandari nyingine Tanzania
ilichaguliwa kunufaika na mradi huu.
“Bandari ya Tanga ni bora kwa
sababu ina kina kirefu ambacho ni zaidi ya mita 23 ambayo ndicho
kinayotakiwa Kimataifa kwasababu hiyo kinaweza kufanya kazi mwaka
mzima”, alisema Prof. Muhongo.
Chagizo la kuanza kwa mradi huu
lilipamba moto Marchi 28 mwaka huu, baada ya Rais Magufuli kukutana na
Mawaziri wa Nishati na Madini wa Serikali zote mbili katika Ukumbi wa
Baraza la Mawaziri Ikulu, Jijini Dar es Salaam ili kujadili Maendeleo ya
Mradi huo.
Wahenga walisema “Hata Mbuyu
ulianza kama Mchicha” wakiwa na maana kila kitu kikubwa kilianza kikiwa
kidogo vivyo hivyo Mradi huu ulianza kwa ahadi, makubaliano na hatimaye
utekelezaji.
Mei 21 mwaka huu, Rais Magufuli
na Rais wa Jamhuri ya Uganda Yoweri Kaguta Museveni walitia rasmi saini
ya tamko la pamoja ili kukamilisha majadiliano ya vipengele vya mkataba
wa utekelezaji wa mradi huo.
Wakazi wa Mkoa wa Tanga,
wanahesabu miezi miwili tangu kusainiwa rasmi kwa mkataba wa mradi huo
utakaowapeleka kwenye mafanikio mbalimbali ikiwemo fursa za ajira ,
ukuaji wa kasi wa maendeleo , na kuurudishia umaarufu uliopotea wa mji
huo.
Ikumbukwe Mkoa huo, ulikua maarufu
miaka ya 1960 na 1970 kutokana uwepo wa viwanda mbalimbali ikiwemo
vya uzalishaji katani ambalo ni zao kuu la biashara mkoani humo .Lakini
umaarufu huo ulipotea baada ya viwanda hivyo kushindwa kuendelea
kuzalisha bidhaa za kutosha kama vile kiwanda cha saruji Tanga.
Licha ya mji huu kupoteza umaarufu
bado ni kivutio kikubwa cha Utalii kwani kuna Mapango ya Amboni ambayo
yamekua yakiupamba mji huo wenye kilomita za mraba 27,348 na Wilaya 10
ambazo ni Handeni Vijijini, Handeni Mjini, Kilindi, Korogwe Vijijini,
Korogwe Mjini, Lushoto, Mkinga, Muheza, Pangani na Tanga Mjini pamoja na
majimbo 11 ya uchaguzi ambayo ni Tanga Mjini, Pangani, Handeni, Korogwe
Mjini, Korogwe Vijijini, Lushoto, Bumbuli, Mlalo, Kilindi Mkinga na
Muheza.
Miaka , na miezi ilipita hatimaye,
Mkoa huo umefufua umaarufu wake kupitia Kata ya
Chongoleani inayopatikana katika moja ya Wilaya mkoani humo, yenye
wakazi wapatao 4,737 , kwa mujibu wa sensa iliyofanyika mwaka 2012
,ambao pia karibu nusu ya wakazi wake ni wanufaika wa huduma ya umeme
tangu mwaka 2015 kufuatia mpango wa serikali wa usambazaji umeme
vijijini.
Agosti 5 mwaka huu (kesho), Tanga
inatarajia kurudisha sifa na umaarufu uliopotea kwa zaidi ya miaka
takribani 60 kufuatia shughuli za uwekwaji wa jiwe la msingi la Mradi
itakayofanywa na Rais Magufuli na Museveni ambao utapelekea Nchi zote
mbili kwenye mapinduzi ya kiuchumi kwa Nchi na wakazi wa Mkoa huo
kupitia fursa mbalimbali hususani kwenye upatikanaji wa Ajira, biashara,
chakula ,malazi, bima na huduma za kifedha.
Kwa Upande wake, Mkurugenzi Wa
Mawasialiano Ikulu Bw.Gerson Msigwa ametoa wito kwa Watanzania
wanaoishi mbali na Mkoa huo kufuatilia matangazo na machapisho
mbalimbali yanayotolewa ili kupata taarifa kuhusiana na shughuli hiyo na
kwa upande wa wakazi wa Mkoa huo amewasihi kuhudhuria ili waweze
kushuhudia tukio hilo la kihistoria.
Ifike wakati Watanzania tujivunie
na tumpongeze Rais Magufuli kwa juhudi anazozifanya ili kuinua kipato
kwa Wananchi kuanzia ngazi ya chini kwa kutengeneza fursa mbalimbali za
ajira, miundo mbinu ili kurahisha shughuli za biashara na Afya kwa
ujumla badala ya kushabikia mambo yasiyo na tija kwa maendeleo.
Kwa wakazi Mkoa Tanga, Serikali
imetekeleza ahadi iliyotolewa hivyo basi ni wajibu wao kuunga mkono
Mradi huu kwa kutoa ushirikiano hususani katika kufanya kazi kwa bidii,
kulinda ili kuzuia uharibifu au kukwamisha shughuli hizo kwa namna
yoyote.
Post a Comment