Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
akiwahutubia Wananchi wa Wilaya ya Sikonge Mjini leo Agosti.10.2017
katika viwanja vya Tasaf Waziri Mkuu yupo Mkoani Tabora kwa ziara ya
Kikazi
PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
…………………..
*Ataka apate maelezo kwa nini ameshindwa kukusanya mapato
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amempa siku 15 Mweka Hazina wa Wilaya ya Sikonge, Bw. Evans Shemdoe
ajieleze ni kwa nini ameshindwa kufikisha asilimia 80 ya makusanyo ya
ndani.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo
leo asubuhi (Alhamisi, Agosti 10, 2017) wakati akizungumza na watumishi
na watendaji wa wilaya hiyo, mjini Sikonge.
“Nataka maelezo
yakayoniridhisha ni kwa nini hamkufikisha asilimia 80 ya makusanyo ya
halmashauri ambacho ni kiwango cha chini. Nzega TC wamefikisha asilimia
112, Kaliua wana asilimia 91, Nzega DC wana asilimia 80, ni kwa nini
wewe umeshindwa kufikisha kiwango hicho?,” alihoji Waziri Mkuu.
“Ninataka nipate maelezo pia
ni ipi mipango yenu ya kukusanya mapato kwa maeneo mliyoshindwa kufanya
vizuri, na pia mmejipangaje kwa mwaka ujao wa fedha. Niyapate maelezo
hayo ifikapo tarehe 25 Agosti,” amesema.
Alipopewa nafasi ya kujieleza,
Bw. Shemdoe alisema wamefikisha asilimia 76.7 na wameshindwa kufikia
lengo kwa sababu ya upungufu wa mvua katika msimu uliopita, hali ambayo
ilichangia kushuka kwa mavuno ya zao la tumbaku miongoni mwa wakulima.
Hata hivyo, Waziri Mkuu
aliwataka watumishi wa wilaya hiyo, washirikiane na watendaji na
madiwani ili kuongeza mapato ya wilaya hiyo badala ya kuwaachia
watendaji wa kata peke yao.
Jana, mara baada ya kupokea
taarifa ya mkoa wa Tabora, Waziri Mkuu alizitaka Halmashauri tano kati
ya nane za mkoa huo zitoe maelezo ni kwa nini zimeshindwa kufikisha
asilimia 80 ya makusanyo kama ambavyo waliagizwa na Serikali.
“Halmashauri zilizovuka
malengo ni tatu tu, Nzega TC, Kaliua na Nzega DC. Nataka taarifa za
halmashauri zilizobakia ifikapo Agosti 25, wakijieleza ni kwa nini
hawajafikia malengo ya ukusanyaji mapato yaliyowekwa ambayo ni asilimia
80,” alisema.
Taarifa ya mkoa huo inaonyesha
makusanyo kwa kila Halmashauri ni kama ifuatavyo:- Tabora Manispaa
asilimia 64.1; Nzega Mji (asilimia 112); Nzega Wilaya (asilimia 80.8);
Igunga (asilimia 64.6); Tabora (asilimia 77.3); Sikonge (asilimia 76.7);
Urambo (asilimia 70.9) na Kaliua (asilimia 91.5).
Pia amezitaka Halmashauri zote
zihakikishe zinafanyamakusanyo kwa kutumia mfumo wa kielektroniki.
“Ukusanyaji wote wa mapato ni lazima ufanyike kwa mfumo wa
kielektroniki. Halmashauri ambazo hazijafanya hivyo, zitumie makusanyo
ya mwaka jana kununulia mashine za EFD. Hatutaki kuona risiti za
kuandika kwa mkono zinatumika,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu ameutaka uongozi wa mkoa wa Tabora uhakikishe wanapatikana
watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika wilaya hiyo ili
waweze kusaidiana na watendaji wa halmashauri hiyo kukusanya mapato.
“Hapa Sikonge naambiwa hakuna
ofisi za TRA. Lazima tupate maafisa wa TRA katika kila Halmashauri ili
watoe elimu na washirikiane na madiwani, watendaji wa vijiji na
watumishi wa Halmashauri juu ya ukusanyaji mapato,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, AGOSTI 10, 2017.
Post a Comment