PAMOJA na serikali kuongeza
uwekezaji katika sekta ya elimu, ikiwa ni asilimia 17 ya bajeti nzima,
mazingira ya kufundisha na kufundishwa nchini bado si mazuri.
Akiwasilisha mada kuhusu bajeti ya
elimu baada ya kupitishwa Bungeni kwenye kongamano la siku moja la
majadiliano ya kitaifa ya bajeti ya serikali 2017/18 katika elimu na
kilimo Dk Joviter Katabaro kutoka Skuli ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar
es salaam pamoja na kuwekwa maeneo ya kuangaliwa kwanza ipo haja ya
kufanya zaidi ili kufikia malengo.
Dk Katabaro katika mada yake
alisema kwamba pamoja na serikali kutenga zaidi ya TZS
1.366,685,241,000.00 katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Ufundi huku
Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI) ikipatiwa
sh 201,655,446,000/- kwa ajili ya elimu, alisema kwamba anaona ipo haja
ya kuongeza nguvu katika maeneo kadhaa ili kuweka sawa mazingira ya
kufundisha na kufundishwa.
Katika mjadala huo wa kitaifa
uliodhaminiwa na Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk
Katabaro alisema kwamba kwa sasa vifaa vya kufundishia na kujifunzia
vinakosekana katika shule nyingi na taasisi zinazohusiana na elimu na
hivyo kukwamisha ufanisi na tija katika elimu.
Aidha katika mada yake alitaka
juhudi inayofanywa ya kuweka sawa mizania ya walimu pale walipo wengi
kuhamishwa inabidi iendelee ili kuweka uwiano sawa wa elimu nchini.
Pia alisema kuwa uwiano wa sasa wa
walimu nchini sio sawa huku katika masomo, baadhi yakiwa na walimu wa
ziada na mengine yakiwa na upungufu mkubwa.
Mwaka 2016 kwa mujibu wake
kulikuwa na walimu wa ziada katika masomo kadha huku kukiwa na upungufu
katika masomo mengine hasa Hesabu na Sayansi: Basic Mathematics – 7,291
(Upungufu);Biolojia – 5181 (Upungufu);Kemia – 5373 (Upungufu);Fizikia –
6873 (Upungufu);Kilimo 508 (Upungufu);Kingereza– 1267 (ziada); Jiografia
– 3281 (ziada); Historia – 4764 (ziada) na Kiswahili – 4795 (ziada).
Pamoja na masomo Dk. Katabaro
aliangalia bajeti hiyo katika maeneo muhimu yanayofanya mtoto kuwa na
akili kama viwanja vya michezo na upatikanaji wa maji safi kwa ajili ya
kunywa na usafi.
Maji haya ni muhimu sana kwa watoto wa kike ambao usafi wao ndio siri ya mahudhurio ya shule kila siku.
Mada hiyo pia ilitahadharisha
kuhusu takwimu ikitaka zitumike vyema ili kuondoa mipango mibovu hasa ya
uandikishaji wa watoto wa darasa la kwanza na wale wanaoingia kidato
cha kwanza.
Wakati huo huo katika mada
iliyowakilishwa kwa pamoja kati ya Profesa haidari Amani na John
Shilinde, kilimo pamoja na kutegemewa na wengi na kuwa chachu ya
maendeleo ya viwanda bajeti yake iliyotengwa bado ni ndogo
Walisema kwamba sekta hiyo ilipata
kiasi cha karibu asilimia 10 ya bajeti nzima, bajeti ambayo ukiiangalia
utaona kwamba haiwezi kubadili kilimo.
Wamesema kwamba kilimo ambacho
huajiri asilimia 70 ya wananchi ikichangia asilimia 28 ya pato la taifa
huku ikipatia asilimia 30 ya mapato ya kigeni na kuchangia asilimia 65
ya mali ghafi, bado sekta haijapewa nguvu za kutosha kusonga mbele.
Wamesema kilimo kitabadilika kwa fedha za utafiti na sayansi na ubunifu ili kuiweka sekta katika hali bora zaidi.
Walisema kwamba sayansi na ubunifu ni kichocheo kikubwa cha mabadiliko katika kilimo.
Wataalamu hao walitaka bajeti
zaidi kwa ajili ya utafiti na maendeleo, kilimo cha umwagiliaji,
kuongeza ruzuku, kuboresha kilimo cha kisasa cha kutumia zana kupunguza
upotevu wa mazao baada ya mavuno, kuongeza kazi zenye staha vijijijni,
kuongeza mnyororo wa thamani na matumizi endelevu ya ardhi na maji.
Post a Comment