Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
DAR ES SALAAM
8.8.2017.
KILIMO ndiyo Msingi wa Uchumi wa
Taifa letu ambapo takribani asilimia 70 ya Watanzania hutegemea sekta
hiyo kama shughuli kuu ya Kiuchumi.
Hata hivyo, pamoja na ukweli
kwamba Nchi yetu ina eneo kubwa linalofaa kwa Kilimo takriban Hekta
Milioni 29.4, ni Hekta 290,000 tu, sawa na Asilimia Moja (1%)
zinazotumika kwa Kilimo cha Umwagiliaji Maji.
Kwa maana hiyo, Kilimo cha
Umwagiliaji kinayo nafasi kubwa ya kuwezesha kufikia Mapinduzi ya Kijani
kwa kuwa kinatuhakikishia uzalishaji endelevu wa mazao badala ya
kutegemea mvua ambazo hazina uhakika wa kiasi na wakati wa kunyesha
katika msimu.
Serikali imekusudia kuongeza eneo
la umwagiliaji kufikia hekta 1,000,000 katika skimu za wakulima wadogo,
wa kati na wakubwa ifikapo mwaka 2020, ikiwa ni njia mojawapo ya
kuongeza uzalishaji wa Mazao ya chakula na biashara na kuongeza tija
katika kilimo.
Akiwasilisha Makadirio ya Bajeti
ya mapato na matumizi kwa mwaka 2017/18, Waziri wa Maji na Umwagiliaji,
Mhandisi Gerson Lwenge anasema hadi mwezi Machi 2017, eneo
linalomwagiliwa limeongezeka kutoka hekta 461,326 kwa mwaka 2015/2016 na
kufikia hekta 468,338.
“Eneo hilo linachangia asilimia 24
ya mahitaji yote ya chakula nchini kwa sasa, ambapo hekta milioni 2.3
zina uwezekano mkubwa, hekta milioni 4.8 zina uwezekano wa kati na hekta
milioni 22.3 zina uwezekano mdogo” anasema Mhandisi Lwenge.
Mhandisi Lwenge anasema katika
mwaka 20176/18, Serikali inatarajia kutekeleza Mpango wa miaka 5 wa
Programu ndogo ya Umwagiliaji iliyolenga katika kukamilisha ujenzi wa
miundombinu katika skimu na mabwawa ya umwagiliaji.
Waziri Lwenge anasema katika awamu
hiyo, Serikali imepanga kukamilisha ujenzi wa miundombinu katika skimu
176, ukarabati wa skimu 205, ukarabati wa mabwawa 30 na kujenga mabwawa
mapya 40 ili kuvuna maji ya mvua kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na
matumizi mengine kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Mhandisi Lwenge
anasema Serikali itaendelea kuwajengea uwezo wakulima na wataalam kuhusu
usimamizi na uendeshaji wa miundombinu ya umwagiliaji na kusajili vyama
vipya 100 vya wamwagiliaji katika skimu za wakulima wadogo; na
kuimarisha vyama 442 vya umwagiliaji vilivyopo.
Aidha Mhandisi Lwenge anasema
Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa mradi wa kuendeleza skimu
za umwagiliaji za wakulima wadogo kwa awamu tatu katika Halmashauri 68
nchini.
Anasema kuwa hadi kufikia mwezi
Machi 2017, ukarabati na ujenzi wa skimu 45 za awamu ya kwanza
umekamilika na utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi unahusisha ujenzi
na ukarabati wa skimu 63 ambapo ukarabati na ujenzi wa skimu 43
unaendelea; na taratibu za kuwapata Wakandarasi wa skimu 20 zilizobaki
zinaendelea katika Halmashauri husika.
“Katika mwaka 2016/2017, Wizara
kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya 32 imeendelea kusimamia
ukarabati na uboreshaji wa skimu 45 za umwagiliaji za awamu ya kwanza
zenye jumla ya hekta 13,722 na hivyo kumeongeza eneo la umwagiliaji
kutoka hekta 461,326 hadi kufikia hekta 468,338” anasema Waziri Lwenge.
Serikali inaendelea kupitia Mpango
Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002 ili kubaini maeneo
yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, ambapo kazi hiyo inatarajia
kukamilika katika mwaka 2018/2019.
Kukamilika kwa Mpango huo
kutasaidia kuleta Mapinduzi ya Kijani nchini ambayo yanahitaji matumizi
ya utaalamu, mbegu bora, mbolea, madawa, zana bora za kilimo pamoja na
kuongeza eneo la Kilimo cha Umwagiliaji.
Aidha Mpango huo umekusudia kuweka
mazingira mazuri ya kuongeza Uzalishaji katika Kilimo; kuongeza Pato la
Mkulima; kupunguza Umaskini Vijijini na kushirikisha Sekta Binafsi
kuleta uhakika wa Chakula katika Kaya.
Post a Comment