MKUU wa Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, Simon Odunga, ambaye hivi karibuni alimcharaza viboko mzazi wa mtoto aliyemtuhumu kupiga mawe gari lake, Chindika Pingwa, amemwomba radhi mzazi huyo na kumpa zawadi ya mbuzi jike na Sh. 100,000.
Kipigo cha DC huyo, kilimsababishia Chindika maumivu makali na kushonwa nyuzi tisa kichwani.
Tukio hilo lilitokea Agosti 11, mwaka huu, katika barabara ya Kondoa – Dodoma kwenye kijiji cha Paranga wilayani Chemba. Katika tukio hilo, gari la DC huyo lenye namba za usajili STL 669 lilipigwa mawe na watoto na kusababisha kioo cha nyuma kuvunjika.
Akizungumza na Nipashe jana, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mrongia kilichoko Kijiji cha Kambianyasa wilayani Chemba, anachoishi mzazi huyo, Marius Roman, alisema Odunga alifika juzi katika kitongoji hicho na kukutana na mzee Chindika pamoja na uongozi wa kijiji na hatimaye kuomba msamaha kwa kitendo alichokifanya.
Alisema pamoja na kuomba radhi, Odunga alimpa mzee Chindika Sh. 100,000 na mbuzi jike kama sehemu ya kuonyesha kujutia kosa alilolifanya.
Alisema pamoja na kuomba radhi, Odunga aliahidi kuendelea kugharimia matibabu yake hadi pale afya yake itakapoimarika, ili aweze kuendelea na shughuli zake za kila siku.
Roman alisema kitendo alichofanya DC huyo, kimeonyesha uungwana mkubwa kwa sababu ameona kosa lake na kuamua kuomba radhi kwa mwananchi huyo.
Kwa upande wake, Chindika alimshukuru mkuu huyo wa wilaya kwa kuonyesha uungwana na kuomba radhi kwa kitendo alichokifanya. Pia alikiri kupewa mbuzi, lakini alikataa kuzungumzia kiasi cha pesa alizopatiwa.
Alipozungumza na Nipashe, Odunga alikiri kukutana na mzazi huyo pamoja na uongozi wa kijiji kuzungumzia suala hilo, ikiwamo kuomba msamaha kwa yale yaliyotokea na kumpatia Chindika mbuzi na fedha taslimu Sh. 100,000.
Odunga alisema ameamua kufanya hivyo baada ya kuona alifanya kitendo kile akiwa na jazba na ameona ni vyema kuomba radhi, ili aendelee kushirikiana na wananchi wake.
Alisema pia atahakikisha anaweka mikakati ya kusimamia usalama barabarani kwenye eneo hilo, ili kuwakinga watoto wanaojitokeza barabarani kurusha mawe kwenye magari yanayopita.
“Tumeweka mikakati na viongozi wa kijiji hicho, ili kuhakikisha usalama wa barabarani unakuwapo,” alisema Odunga.
Post a Comment