Jovina Bujulu-MAELEZO.
01 Agosti, 2017.
Tanzania ni miongoni mwa nchi za dunia hii
imebabarikiwa kuwa na rasilimali nyingi ambazo zikitumika ipasavyo
itaondokana na tatizo la umaskini.
Hayo yalibainishwa hivi karibuni na Balozi
wa Tanzania nchini China Mhe. Mbelwa Kairuki alipokuwa akizungumzia
fursa za kibiashara zinazoweza kupatikana nchini China na kuinua hali
ya uchumi kwa wananchi wa Tanzania.
Balozi Kairuki alisema kuwa ni aibu kwa
nchi za Kiafrika ambazo zimepata uhuru kwa zaidi ya miaka 50 kuagiza
bidhaa kutoka nje ya nchi hususan nchini China.
“Nchi yetu imebarikiwa kuwa na ardhi yenye
rutuba, maji, mito na maziwa hivyo tukitumia rasilimali hizi kwa
kuunganisha na nguvukazi, uwezo na mitaji tuliyo nayo tunaweza kabisa
kupaisha uchumi wa nchi yetu sisi wenyewe” alisema Balozi Kairuki.
Kwa mujibu wa nyimbo za kujenga uzalendo
kwa nchi zinakiri kuwa ni nchi nzuri, yenye mito na mabonde mengi ya
nafaka, nasema kwa kinywa halafu kwa kufikiri, nchi hiyo mashuhuri
huitwa Tanzania. Ni vema kuijenga kuisimamia kwa manufaa ya Watanzania.
Balozi Kairuki alisema kuwa kufuatia
kusainiwa kwa mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na China, mwezi Mei
mwaka huu watanzania watapata fursa ya kuuza zao la muhogo mkavu nchini
China kwa kiwango kikubwa hatua ambayo itainua hali zao hilo kiuchumi na
kuweza kuanzisha viwanda nchini.
“Hii ni fursa, natoa rai kwa Watanzania
wenzangu tuichangamkie na tujitokeze kwenye maonesho ya biashara
yatakayofanyika nchini China mwezi wa 10 mwaka huu, na kuhakikisha
tunapata fursa ya kuona mashine za kuchakata na kulimia ili tuweze
kuzinunua na kuzitumia katika uzalishaji mazao ya muhogo” alisema
Balozi Kairuki.
Ili kuhakikisha zao hilo linawanufaisha
Watanzania, Balozi Kairuki alisema kuwa ni muhimu kuchangamka fursa hiyo
wasije wageni wakiwemo Wakenya na Wachina wakaanza kulima zao hilo na
kuwazidi Watanzania ambao ni walengwa wa kupeleka zao hilo nchini China.
Aidha, aliongeza kuwa kuwepo kwa fursa
hiyo ni fahari kwa nchi Tanzania hatua ambayo itatoa nafasi katika ngazi
mbalimbali kununua mitambo ya kuchakata mazao ya mihogo na kutengeneza
bidhaa zitokanazo na muhogo.
Mkataba huo utakuwa ni miaka mitano,
Watanzania wanatakiwa kuchangamka mapema ili kufaidi matunda ya uwepo
wake kabla hujamalizika kwa namna mbalimbali hata baada ya mkataba huo
kuisha. Fursa hiyo inatoa nafasi pia ya kuanzisha viwanda vya kuchakata
mazao yatokanayo na zao la muhogo na hatimaye kukamata soko la bidhaa
hiyo.
China ni nchi ambayo ina mahitaji makubwa
ya muhogo ambapo kwa mwaka wanaingiza muhogo wa thamani ya zaidi ya dola
za Kimarekani milioni tano.
Katika bara la Afrika nchi ya Nigeria
ndiyo pekee inayouza muhogo China, hivyo Tanzania itakuwa nchi ya pili
barani Afrika kuuza muhogo nchini humo.
“Kutokana na sababu za kijiografia
Tanzania inaweza kusafirisha bidhaa hiyo kwa urahisi zaidi kuliko nchi
ya Nigeria hivyo ni rahisi kuteka soko la zao hilo nchini China” alisema
Balozi Kairuki.
Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
inatakiwa kueleza taratibu za kufanya na kutoa elimu kwa umma kuelezea
taratibu za kufuata kuweza kulima muhogo na kuuza nchini China.
Aidha, wananchi wanatakiwa kulima kilimo
chenye tija kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kuzalisha mihogo yenye
ubora na inayokidhi mahitaji ya soko la kimataifa kwa wingi.
Balozi Kairuki alitoa wito kwa wadau wa
kilimo ambao ni pamoja na wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na
taasisi zilizo chini yake, Halmashauri na vituo vya utafiti wa kilimo
kuwasaidia wakulima kutatua changamoto zozote zinazoweza kujitokeza ili
waweze kujipatia mazao mengi na kuliteka soko la muhogo nchini China.
Nchi nyingine ambazo zinazouza mazao ya
muhogo nchini China ni pamoja na Thailand, Brazil na Indonesia ambayo
hutumika kutengeneza madawa, biskuti na kwa ajili ya chakula.
Post a Comment