Kitaifa, Kimataifa, Siasa, Michezo na Burudani

Sekta Binafsi Chachu ya Maendeleo Kuelekea Tanzania ya Viwanda.

unnamed
Na Jacquiline Mrisho.
Tanzania ya viwanda inayoelekea kwenye uchumi wa kati ni moja kati ya mipango mikubwa ya Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli katika azma yake ya kuleta Maendeleo  nchini.
Akihutubia Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  kwa mara ya kwanza baada ya kuapishwa kuwa Rais wa awamu ya Tano, Magufuli alisema kwamba Serikali yake itaweka mkazo mkubwa katika ujenzi wa Viwanda.
“Natambua kwamba sekta binafsi ndiyo mhimili mkubwa wa kujenga uchumi wa viwanda. Tamaa yangu na kwa kweli jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano zitakuwa katika ujenzi wa uchumi wa kipato cha kati ambapo sura  na maisha ya Watanzania walio wengi yafanane na nchi za kipato cha kati” alisema Rais Magufuli.

Aidha katika hotuba hiyo Mhe. Magufuli aliongeza kuwa ifikapo mwaka 2020 idadi ya ajira itokanayo na viwanda imepangwa ifikie asilimia 40 ya ajira zote zitakazokuwepo nchini wakati huo.
Serikali pekee haitaweza kuyafikia malengo hayo bila kuwa na ushirikiano wa Wananchi pamoja na wafanyabiashara mbalimbali kutoka sekta binafsi hivyo kwa kutambua hilo, Sekta binafsi zimekubaliana kushiriki katika ujenzi wa viwanda.
Makubaliano hayo yalitangazwa rasmi mbele ya Rais Dkt. Magufuli kwenye kikao cha kumi cha Baraza la Taifa la Biashara (TPSF) kilichofanyika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam ambapo viongozi wa Baraza hilo walisema kuwa wameamua kwa moyo mmoja kusaidiana na Serikali katika kutekeleza azma hiyo ya kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda.
Katika ripoti ya Sekta binafsi iliyokabidhiwa kwa Mhe. Rais Magufuli ilieleza kuwa “Katika kuunga mkono jitihada za dhati za Rais, sekta binafsi ya Tanzania imependekeza agenda kuu ya Baraza hilo kuwa ni ‘Ushirikiano wa Sekta Binafsi na Serikali kuelekea Uchumi wa Viwanda’.
Kama inavyofahamika duniani kote sekta binafsi ndio muhimili mkubwa wa ukuaji wa uchumi wa taifa lolote,hivyo ni jukumu la Serikali kuweka mazingira wezeshi kama inavyofanya Serikali ya Awamu ya Tano ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Juhudi za makusudi zimeonyeshwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuhakikisha sekta binafsi inawezeshwa, mfano katika ziara ya Rais wa Uturuki Mh. Recep Tayyip Erdogan aliyoifanya hivi karibuni, wafanyabiashara zaidi ya 600 walioambatana naye walikutanishwa na sekta binafsi hapa nchini na kubadilishana mawazo pamoja na uzoefu katika biashara.
Kadhalika alipokuja Waziri Mkuu wa India Mh. Narendra Modi aliambatana pia na wafanyabiashara ambao kwa umoja wao walikubaliana na sekta binafsi jinsi ya kushirikiana katika kukuza uchumi wa viwanda hasa kuendeleza viwanda vidogo.
Aidha hivi karibuni Tanzania ilitembelewa na  Rais wa Afrika Kusini Mh. Jacob Zuma akiambatana na Mawaziri 6 akiwemo Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Rob Davies na wafanyabiashara 80 ambao waliungana na wafanyabiashara wa Tanzania kujadili mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo ya sekta hiyo.
Mchango mkubwa wa Serikali pamoja na sekta binafsi chini ya  uratibu wa TPSF ni wa kuigwa na wa mfano, uzalendo waliouonyesha utaleta maendeleo hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchumi wa Kati unaoshamirishwa na ujenzi wa viwanda.
Kwa mujibu wa taarifa za TPSF,Sekta Binafsi inalenga kukuza pato la taifa kufikia asilimia 60 pamoja na kutoa asilimia 40 ya ajira kwa watanzania.
Hatuna budi kuwapongeza wafanyabiashara na Sekta Binafsi kwa ujumla kwa kukubali kwa moyo mmoja kushirikiana na Serikali katika kusukuma gurudumu la kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya Viwanda.
Hongera TPSF, hongera Serikali kwa kuonyesha njia, ama kwa hakika mabadiliko yanakuja na Tanzania yenye neema inakaribia.
Labels:

Post a Comment

[facebook]

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget