- Habari za Taarifa za Kamati za Kuchunguza Makinia zatawala ulimwengu
- Bosi wa Barrick akubali yaishe
Said Amer
Maelezo
Kwa kipindi cha zaidi miezi 4 sasa suala la mchanga wa dhahabu au Makinikia limetawala vichwa vya habari vya vyombo vya habari vya ndani na nje. Katika Makala hii Mwandishi Said Ameir wa Idara ya Habari- MAELEZO anaeleza uzito wa habari kwa kuangalia mustakbala wa makampuni ya madini na mataifa yanayotoka.
Ni dhahiri kuwa dunia hivi
sasa inatafakari kuhusu namna ya kukabiliana na dharuba hii ya Rais
Magufuli dhidi ya makampuni ya madini. Mabepari wa madini wamepatwa na
kiwewe kwa sababu msimamo wa Rais Magufuli unawaamsha wengine waliolala
nao kudai haki zao kama wanavyofanya watanzania.
Kwa lugha za vijana wa kileo
wanasema ‘JPM ameliangusha ‘Dude’ ambalo limeleta taharuki kubwa katika
viota vya biashara ya madini- mfano majiji ya London, New York, Geneva,
Otawa, Vancouver na kwengineko katika sekta nzima ya biashara ya madini
ulimwenguni.
Kwa karibu miezi miwili sasa
vyombo vya habari katika majiji hayo vimekuwa vikiandika habari za
Tanzania kuhusu mgogoro huo ambao umeitikisa sekta ya madini
ulimwenguni.
Katika majarida ya sekta ya madini
katika nchi za Canada, Australia, Marekani na Uingereza yamekuwa
yakiandika habari za taarifa za Kamati za Rais kuchunguza mchanga wa
madini. Kama kawaida mengi ya majarida hayo yanaelekeza shutuma kwa
Mheshimiwa Rais na wengine kama si hivyo wamekuwa wakiripoti tu kile
kinachotokea bila kutoa maoni.
Kwa wafuatiliaji wa masuala ya
mwenendo wa uvunaji wa rasilimali katika nchi zinazoendelea unaofanywa
na makampuni makubwa kutoka nchi tajiri hawatashangazwa hata kidogo na
haya yanayotokea hivi sasa nchini Tanzania.
Kwa miaka mingi viongozi wa nchi
masikini ikiwemo Tanzania wamekuwa wakipiga kelele dhidi ya makampuni
hayo kuvuna maliasili za nchi zao kwa kutumia mikataba ya kinyonyaji
ambayo pamoja na mambo mengine ni matokeo ya udhaifu wa nchi masikini wa
kukosa utaalamu na uzoefu katika sekta hiyo.
Katika nchi tajiri, mara nyingi
tumeona katika mikutano ya kimataifa, sauti za kupinga vitendo hivyo
zimekuwa zikipazwa na wanaharakati wanaotetea rasilimali za nchi
masikini na wale wa haki za binadamu pekee huku viongozi wa nchi hizo
wakilipuuzia suala hilo kwa manufaa ya makampuni yao.
Si katika mikutano hiyo wala
wakiwa nchini mwao, hatujaona viongozi wa nchi tajiri wakichukua hatua
madhubuti kuyadhibiti makampuni yao kuacha kuzinyonya nchi masikini
kupitia mikataba ya uvunaji wa maliasili. Kama ilivyoelezwa jukumu hilo
la kupinga uporaji wa rasilimali za nchi masikini limeachwa kwa
waharakati pekee.
Wamekuwa wakizitia nchi masikini
katika migogoro huku wakivuna maliasili za nchi hizo wakati huo huo kwa
kutumia wasomi na wataalamu wao kuendeleza ukoloni mamboleo wa kifikra
na kuleta nadharia mpya kama “laana ya maliasili” (natural resource
curse) kuonesha kuwa kosa ni la nchi masikini si lao. Kwamba maliasili
zimeleta laana… tunapigana na kuuana na kumbe nyuma wao ndio chanzo.
Kama inavyojitokeza hapa nyumbani,
huko ‘duniani’ nako wako wanaowatetea wanyonyaji kama Acacia na wala
haishangazi kwa kuwa wana maslahi yao lakini pia wako wanaowatetea
watanzania kwa sababu ni waumini wa kukataa unyonyaji hata kama
unafanywa na ndugu zao.
Nchini Canada kwenyewe,
mshikemshike umewakuta viongozi wa Kampuni ya Barrick inayomiliki
asilimia kubwa ya hisa za kampuni ya Acacia kwani wanaharakati wameanza
kuhoji usafi wa uongozi wa kampuni hiyo kwamba wanawezaje kuendeleza
unyonyaji na udanganyifu kwa nchi masikini.
Ieleweke kuwa Acacia wameikosesha
Serikali mapato yake kwa njia za udanganyifu kitendo ambacho kinaonesha
kampuni hiyo haina maadili na si adilifu; inakwenda kinyume na misingi
ya haki na utawala bora.
Kwa bahati mbaya huko ‘duniani’ na
hata hapa Tanzania wanaowatetea Acacia wanazungumzia zaidi zuio la Rais
la kusafirisha mchanga nchi za nje na hawaoni kabisa ubaya wa vitendo
hivi vya udanganyifu kana kwamba wamevaa miwazi za mbao. Hawazunguzii
kabisa hasara ya zaidi ya shilingi trilioni 108 iliyopata Tanzania na
wananchi wake.
Hawataki kuona kuwa vitendo hivyo
ni vya kuhujumu uchumi; wanakwepa kodi za aina mbalimbali kwa kutoeleza
hali halisi ya biashara yao kwa njia mbalimbali kama kuwasilisha nyaraka
zisizo kamilifu kwa kupunguza idadi ya makontena, kutotoa taarifa za
madini mengine yanayopatikana katika mchanga unaosafirishwa.
Katika nchi za Magharibi makosa
haya hayavumiliwi na ni kati ya makossa makubwa yenye adhabu kali, na
katika baadhi ya nchi, kuliko za kosa la kuua kwa kukusudia. Kwa hiyo
inapotokea huku kwetu, baadhi wakayaona madogo inashangaza!
Ni ukweli usiopingika kuwa
‘kishindo’ cha Rais Magufuli sio tu kimetikisa hisa za Kampuni ya Acacia
katika masoko ya hisa ya London na New York lakini pia imetia doa
katika taswira nzima ya kampuni hiyo na Kampuni mama ya Barrick.
Ukitaka kupima uzito wa jambo hili
ni kuangalia namna ya hatua ilizozichukua kampuni ya Barrick kuja
Tanzania kuonana na Rais Magufuli. Ujio wa Profesa John Thornton ambaye
ni Mwenyekiti wa Barrick usichukuliwe kuwa ni kitendo cha kawaida bali
ni hatua muhimu kwa kampuni kutafuta suluhu kwa njia za amani.
Wahenga walisema’kweli ikidhihiri
uongo hujitenga’ na ndivyo ilivyo kwani Barrick walishatanabahi kuwa
taarifa zote mbili zina ukweli na Rais Magufuli asingeweza kusema hicho
alichokisema dhidi ya Acacia kama hana hakika ya anachokisema.
Tofauti na baadhi ya watu
wanavyofikiri, Barrick na Acacia haimuoni Rais Magufuli kama mtu pekee
bali wanaangalia pia uwezo na ushawishi iliyonayo Tanzania katika ngazi
ya kidiplomasia. Wamepima taswira ya Rais Magufuli hivi sasa kwa
kuzingatia namna anavyoonekana shujaa nje ya Tanzania. Katika hali hiyo
Barrick na Acacia wamejiona hawana budi waepuke kiburi badala yake
watafute njia salama na itakayowapunguzia machungu ya kuzidi kuchafua
jina la kampuni yao.
Profesa Thornton, alisindikizwa na
Balozi wa Canada nchini Bwana Ian Myles wakati alipokutana na Rais
Magufuli. Hili linathibitisha uzito zaidi wa tuhuma dhidi ya Acacia. Kwa
wafuatiliaji wa masuala ya kidiplomasia watakubaliana na mwandishi wa
makala haya kuwa kadhia hii imeifedhehesha Serikali ya Canada na ndio
maana balozi alihudhuria mazungumzo hayo.
Kama inavyojulikana Canada ni
miongoni mwa ‘vinara’ wa kuhubiri na kufundisha utawala bora kwa nchi
zetu na katika kufaya hivyo nchi hizi zinatuaminisha kuwa nchi zao na
taasisi zao zinaendeshwa kwa misingi ya uwazi, sheria na utawala bora.
Inapotokea hali kama hii kampuni
yao kushutumiwa kwa mambo ambayo wao wenyewe wanayapinga na wakati
mwingine kuwadhihaki hata viongozi wa mataifa masikini nao uso
‘unawashuka’. Ni fedheha kubwa kwao!
Akiwa mwanadiplomasia namba moja
wa Tanzania, Rais Magufuli amekuwa muwazi kwa yeyote kama ambavyo
‘hapepesi macho’ kwa wananchi wake katika kusema ukweli ndivyo hivo kwa
wageni.
Kwa hivyo hapana shaka yeyote,
kuwa Rais Magufuli aliwaeleza wageni wake kila kitu kinagaubaga na kwa
hisia zile zile ambazo alizionesha kwa watanzania wakati akipokea
taarifa za Kamati alizoziunda.
Ndio maana Profesa Thornton
alizielewa vyema hoja za Rais Magufuli na kuzipima uzito wake
unaostahiki ndipo alitafakari na kutoa ombi la kutaka majadiliano na
Serikali na hapo hapo aliahidi kurejesha fedha zote ambazo Tanzania
ilipaswa kupata katika biashara ya madini ya Kampuni ya Acacia.
Kuja kwa ‘matawi ya chini’ kwa
Mkuu huyo wa Barrick kunaonesha pia uwezo wa kampuni ya Barrick kupima
athari za kulipeleka jambo hili katika vyombo vya usuluhisho wa
kimataifa kwa kampuni yake.
Ni mtu mwenye matatizo ya kufikiri
tu anayeweza kudhani katika ‘timbwili’ hili Acacia na Barrick wako
salama salimini. Kesi hii ikifika katika mahakama za kimataifa itakuwa
ni kashfa nzito kwa Acacia na wanahisa wake na inaweza kuharibu kabisa
biashara zao.
Itakuwa hivyo kwa misingi kuwa
ushahidi utakaotolewa ‘utaivua nguo’ kampuni hiyo na inaweza ukawa
mwanzo wa kuporomoka biashara yake. Kwa kutanabahi huko ndiko
kulikomfanya Profesa Thornton akasema ‘funika kombe mwanaharamu
apite’.Tuyazungumze!
Aidha kesi hiyo inaweza kuchochea
migogoro mingine sio dhidi ya kampuni hiyo tu lakini dhidi ya makampuni
mengine ya madini kama si ya hata mafuta na gesi katika nchi kama zetu
ambazo zinanyonywa na makampuni hayo kupitia mbinu chafu kama
zinazotumika humu nchini.
Kwa hiyo, kama walivyosema wahenga
‘heri nusu ya shari kuliko shari kamili’ ndio tafsiri ya hatua ya
Kiongozi wa Barrick Profesa Thornton ya kutaka suluhu kwa mazungumzo na
kwa hakika kwa lugha nyingine ni sawa na kusema ‘amekubali yaishe’.
Post a Comment