WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali imeadhimia kupambana vilivyo dhidi ya biashara haramu
ya dawa za kulevya na kuhakikisha inakuwa historia nchini.
Pia ametoa wito kwa wazazi wote
nchini waendelee kufuatilia nyendo za watoto ili wasijiingize kwenye
mtego wa dawa za kulevya na wala wasisubiri vijana wao waanze kutumia.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi,
Juni 29, 2017) kwenye maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa
za Kulevya Duniani, iliyoadhimishwa mjini Dodoma.
Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu
amesema Serikali imejidhatiti kuhakikisha kuwa uzalishaji, usambazaji na
matumizi ya dawa za kulevya unadhibitiwa kikamilifu nchini.
Amesema katika kutimiza azma hiyo,
ambayo pia inaelekezwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Serikali ilifanya
mabadiliko ya Sheria ya Dawa za Kulevya kwa kuanzisha chombo cha
kisheria cha kupambana na biashara hiyo, ambayo imeongeza adhabu kwa
wanaoshiriki.
Waziri Mkuu amesema Serikali
itaendelea kuimarisha chombo hicho kinachoongoza mapambano ya dawa za
kulevya ili kiendelee kufanya kazi kwa weledi na kwa kutumia mbinu za
kisayansi.
“Tunaponadi uchumi wa viwanda
lazima tuwe na nguvu kazi yenye siha njema kuweza kushiriki kwenye kazi
halali za kujenga Taifa letu na yeyote anayetaka kudhohofisha nguvu kazi
ya Taifa letu au kuhujumu jitihada za uchumi wa viwanda atashughulikiwa
bila huruma,” amesema.
Aidha, kauli mbiu ya maadhimisho
hayo kitaifa ni ‘Tuwasikilize na Kuwashauri Vijana na Watoto ili
Kuwaepusha na Dawa za kulevya.’
Waziri Mkuu amesema kauli mbiu
hiyo imetokana nan a takwimu za waathirika wakubwa wa dawa za kulevya
ambao ni vijana wenye umri kati ya miaka 15-35.
“Hili ndilo kundi kubwa kwenye
jamii jetu na ndilo tegemeo kubwa kwa ustawi wa nchi yetu. Hili ndilo
kundi litakalotoa askari wa kulinda Nchi yetu, wanasiasa wa kuongoza
Taifa letu na wataalamu mbalimbali wa kuisaidia Tanzania,” amesema.
Awali Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu), Mheshimiwa Jenista
Mhagama alisema matumizi ya dawa za kulevya yamelisababishia Taifa
madhara makubwa ya kiafya na kiuchumi hivyo kila mwananchi ashiriki
katika mapambano hayo.
Mapema Waziri Mkuu aliweka jiwe
la msingi la Kituo cha Kutoa Huduma ya Tiba kwa Waathirika wa Dawa za
Kulevya katika eneo la Itega mkoani Dodoma na kuwashauri wakazi wa mkoa
huo kutojihusisha na biashara hiyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
- L. P. 980,
DODOMA.
ALHAMISI, JUNI 29, 2017
Post a Comment