Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mtaalam mbobevu wa Sheria za
Madini na Mafuta nchini, Dkt. Adelardus kilangi ametoa rai kwa
wanasheria watakaoteuliwa kwa ajili ya kurekebisha Sheria za Madini
kuanza kufanya kwanza uchunguzi katika Sheria za Kimataifa za Madini
ili waweze kuishauri vizuri serikali.
Rai hiyo imetolewa leo na mtaalam
huyo katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hii kuhusu maoni
juu ya ripoti ya uchunguzi wa mchanga wa madini iliyowasilishwa na
baadhi ya wachumi pamoja na wanasheria walioteuliwa na Rais Dkt. John
Pombe Magufuli.
Dkt. Kilangi amesema kuwa ripoti
iliyowasilishwa imeonesha madhaifu yaliyopo katika sekta ya madini
ambayo madhaifu hayo yamegawanyika katika maeneo ya mfumo wa Sheria
pamoja na mfumo wa usimamizi ambapo tatizo kubwa limekuwa ni kukosa
uzalendo kwa viongozi waliopewa dhamana ya kufanya maamuzi ya nchi.
“Katika eneo la mfumo wa Sheria,
kwanza nampongeza Rais Magufuli kwa kuwataka wanasheria na wataalamu
wengine kufanya mapitio ya Sheria hizo kwa sababu tukitaka kuleta
mabadiliko lazima tuanzie kwenye Sheria hivyo kwa kutengeneza Sheria
nzuri zenye manufaa kwa umma ni lazima tuanzie katika ngazi za kimataifa
kwani kuna vipengele vinavyoathiri sekta yetu ya madini,”alisema Dkt.
Kilangi.
Mtaalamu huyo ameongeza kuwa ni
lazima kufahamu kwanza mfumo wa Sheria za kimataifa kwa sababu nchi
zilizoendelea zimetengeneza kwa makusudi Sheria kandamizi kwa nchi
zinazoendelea.
Amefafanua kuwa, kabla ya kuanza
kuchunguza Sheria zetu za ndani wanasheria lazima wafahamu jinsi mifumo
hiyo mitatu inavyofanya kazi na inavyoathiri sekta yetu ya madini, yaani
sheria za kimataifa ikiwemo ya Sheria za Kimapokeo/kimila za kimataifa
(Customary International Law), Mikataba inayoingiwa na mataifa
mbalimbali (Multilateral Framework) pamoja na mikataba inayosainiwa kati
ya nchi mbili (Bilateral Framework).Baada ya hapo ndio waje kwenye
sheria zetu za ndani na hatimaye mikataba kati ya serikali na
wawekezaji.
Katika mapendekezo mengine, Dkt.
Kilangi alisema kuwa wasomi wanasheria na wataalamu wengine kama wachumi
wanatakiwa wapambane kisomi, wapewe hoja za kupambana na mfumo
gandamizi uliopo katika Sheria za kimataifa uliotengenezwa na mataifa
makubwa, na kutafuta mbinu za kupanga upya Sheria za madini nchini kwa
kuongozwa na mapungufu yaliyojitokeza katika ripoti mbili za mchanga wa
madini, tafiti mbalimbali pamoja na mitazamo kutoka nchi zingine juu ya
mambo wanayoyaangalia katika kubadilisha sheria zinazofanana na hizo.
Aidha, amependekeza wanasheria
kufanya marejeo haya kwa kuangalia pia falsafa ya uchumi inayopaswa
kutuongoza kwa kuangalia ufahamu wetu kama taifa kuhusu njia kuu za
uchumi na nyenzo kuu za uzalishaji (Political Economy Analysis) ambapo
wataweza kufahamu nani anamiliki njia kuu za uchumi, nani anamiliki
rasilimali, nani anatoa mtaji, nani anafanya kazi, nani anazalisha na ,
faida inapatikana kiasi gani, na nani anaipata faida hiyo, hali
itakayopelekea muwekezaji kuingia ubia mzuri na Serikali. Haya yote
yafanywe kwenye muktadha wa sekta ya madini.
Pia Dkt. Kilangi alisisitiza kuwa
katika mchakato huo wa kurekebisha sheria za madini ni vizuri
kushirikisha wananchi wa kawaida ili kupata maoni yao, kwani nao tayari
wameshafahamu athari za mikataba iliyopo sasa, na kwa kweli haya madini
ni yao. Kwa hiyo kuhusishwa kwao ni muhimu alisisitiza.
Post a Comment