Kila mwaka, tarehe 20 Juni, Mataifa
yote ulimwenguni huadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani (World Refugee
Day). Awali siku hiyo ilikuwa inaadhimishwa Barani Afrika peke yake
ikiitwa Siku ya Wakimbizi Barani Afrika na kuanzia mwaka 2001
Maadhimisho hayo yalianza kufanyika Duniani kote baada ya Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa kuelekeza hivyo katika kuadhimisha miaka 50
ya Sheria ya Kimataifa ya Wakimbizi.
Lengo la maadhimisho haya ya kila
mwaka ni kuhamasisha Ulimwengu kutambua uwepo wa mamilioni ya wakimbizi
na watu wengine wanaohama kutoka kwenye maeneo yao kwenda maeneo mengine
ndani ya nchi zao (internally displaced persons) kuogopa vita, migogoro
na mateso.
Maadhimisho haya huwahusisha viongozi
wa serikali, watumishi wa mashirika ya misaada, watu mashuhuri na
wakimbizi wenyewe. Maadhimisho haya huambatana na kauli mbiu ambayo
kutoa msisitizo wa jambo ambalo hupewa msukumo katika matamko ya mwaka
husika ambapo Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Tuko Pamoja na Wakimbizi’
ikiwa na lengo la kukumbusha jukumu la kila mmoja la kuwasaidia
wakimbizi na kutafuta ufumbuzi wa matatizo ambayo yamesababisha wao
kujikuta katika hali hiyo.
Kama inavyofahamika Tanzania imekuwa
na historia ndefu ya kuhifadhi wakimbizi toka nchi mbalimbali za Afrika
na kwingineko. Kwa vipindi mbalimbali wamekuwepo wakimbizi tofauti
tofauti kama vile wakati wa harakati za kupigania uhuru wa nchi za
Kusini ya Afrika ambapo kulikuwa na wakimbizi toka Afrika Kusini,
Namibia, Msumbiji, Angola na Zimbabwe ambao walirudi katika nchi zao za
asili baada ya ukombozi kupatikana katika nchi hizo.
Aidha, nchi yetu inaendelea kuhifadhi
wakimbizi toka nchi za jirani zinazokumbwa na migogoro ya kisiasa na
kivita hususani zile za Maziwa Makuu za Burundi na Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo na Pembe ya Afrika kama Somalia na wachache toka
nchi mbalimbali.
Maazimio ya mwaka huu, ya Siku ya
Wakimbizi Duniani yanaikuta nchi yetu ikiwa inahifadhi wakimbizi wapatao
345,000, wengi wao wakiwa wanatoka katika nchi za Burundi na Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo na ambao wanahifadhiwa katika kambi zilizoko Mkoa
wa Kigoma za Nyarugusu, Nduta na Mtendeli na wengine wachache
waliosalia baada ya wenzao wengi kupata uraia ambao wapo Katavi na
Tabora.
Kwa kuzingatia uwepo wa wakimbizi hao,
maadhimisho ya mwaka huu yatafanyika Dar es Salaam ambapo yatahusisha
Wakimbizi wenyewe, Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Viongozi wa Serikali,
Asasi zisizo za Kiraia, watumishi wa Mashirika ya Misaada, na Wasanii
maarufu, vyombo vya habari, wananchi na kwenye maeneo yanayohifadhi
wakimbizi katika Mikoa iliyotajwa.
Serikali yetu itapenda kutumia
maadhimisho ya mwaka huu kuihakikishia Jumuiya ya Kimataifa, wakimbizi
wenyewe pamoja na wadau mbalimbali kuwa itaendelea kuchukua hatua
muhimu za kuboresha huduma kwao katika sekta za elimu, afya, makazi na
kuihuisha Sera ya Wakimbizi ili ieandane na changamoto za wakati huu.
Kwa upande wa elimu, Serikali
inatambua tatizo la upungufu wa madarasa katika kambi za wakimbizi
linalotokana na upungufu wa fedha zinazotolewa na Wahisani kufadhili
mradi mzima wa kuhifadhi maelfu ya wakimbizi toka nchi za jirani na
kwingineko. Pamoja na hayo, nchi yetu kwa kushirikiana na UNHCR na wadau
wengine itafanya jitihada za kujenga madarasa na miundo mingine muhimu
kuhakikisha kuwa watoto wote wa wakimbizi wanapata elimu bora
kuwawezesha kupata taaluma na ujuzi utakaowanufaisha wao wenyewe na
jamii zao wakiwa kwenye kambi na wakati watakaporejea kwenye nchi zao za
asili .
Vile vile Serikali, kupitia taasisi
yake ya RITA, inakusudia kutoa vyeti vya kuzaliwa, kwa watoto wa
wakimbizi ambao wanazaliwa hapa nchini, katika kambi za wakimbizi, ili
kuwafanya watoto hao kuwa na hati zinazotambulika kisheria na zenye
kubainisha waziwazi uraia wao wa asili. Ni vema ikafahamika kuwa hati
hizo ni muhimu hata baada ya maisha ya ukimbizi. Uamuzi wa kuwapatia
hati unafuatia makubaliano baina ya serikali na UNHCR yanayowezesha
Shirika hilo kusaidia
nyenzo muhimu zinazohitajika katika zoezi hilo.
Ni nia ya Serikali kuhakikisha kuwa
wakimbizi wanapata hati zote muhimu zinazohitajika kama cheti cha
kuzaliwa, kitambulisho n.k kwa mujibu ya Mikataba ya Kimataifa mbayo
nchi imeiridhia. Ni matarajio ya Serikali kuwa vyeti vya kuzaliwa
vitaanza kutolewa kabla ya mwisho wa mwaka huu na utakuwa ni utaratibu
wa kudumu.
Eneo jingine ambalo litapewa
kipaumbele kwa lengo la kuboresha huduma kwa wakimbizi ni mradi wa
kuhuishwa Sera ya Wakimbizi na Sheria pamoja na mambo mengine, Sera
mpya na Sheria zitakazotungwa inakusudia kupanua wigo wa wakimbizi wenye
ujuzi na sifa za kupata ajira kama wataalamu katika sekta mbalimbali na
pia kupata fursa za kujiari wenyewe nje ya kambi.
Wakati dunia inaadhimisha siku ya
Wakimbizi Duniani, ni vema pia tukaikumbusha Jumuia ya Kimataifa kuhusu
wajibu wao kuongeza ufadhili kuzisaidia nchi changa, kama Tanzania,
kutekeleza jukumu la kuhifadhi wakimbizi. Misaada wanayotoa inasaidia
katika kupatikana kwa bidhaa mbalimbali ambazo zitatumiwa na wakimbizi
na huduma nyingine wanazohitaji. Ni vema ikaeleweka pia kuwa Jumuia ya
Kimataifa ina wajibu wa kuzisaidia jamii ambazo zinaathirika na uwepo wa
wakimbizi wengi kama Kagera, Kigoma, Katavi na Kigoma.
Imetolewa na
Balozi Hassan Simba Yahya
Kaimu Katibu Mkuu
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
20 Juni, 2017
Post a Comment