Na Tiganya Vincent-RS-Tabora
TABORA
Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imetoa wito kwa watumishi wa umma kuharakisha uhakiki wa majina yaliyomo kwenye mifumo ya mishahara ili yawaiane na yaliyoandikwa katika Akaunti za Benki wanazochukulia fedha zao kwa ajili ya kuepuka usumbufu wakati wa malipo ya mshahara wa Julai mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa jana mjini Tabora na Meneja Msaidizi wa Fedha wa BOT Rajab Ibrahim wakati wa mafunzo ya siku moja kwa wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo juu ya utambulizi wa alama za noti na utunzaji sahihi wa noti ili kuepuka kupatiwa noti bandia na kuchakaa mapema kwa fedha hizo.
Alisema kuwa endapo mtumishi atashindwa kurekebisha taarifa zake na kuonekana kuna tofauti katika jina na lile lile lilipo katika Akaunti yake katika Benki ambapo mtumishi ndipo anapoingiziwa fedha , Benki Kuu itashindwa kulimpa hadi atakapofanya marekebisho ya tofauti zilizojitokeza.
Ibrahim alisema kuwa ni vema mtumishi wa umma akajiridhisha kuwa jina leke liliandikwa katika hati ya malipo (salary slip) yake iko sawa na Benki yake kabla ya kumalizika kwa mwezi Juni mwaka huu ili aweze kupata mshahara wake kwa wakati.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Tabora, Afisa Tawala Mussa Khalid alisema kuwa watumishi wengi mkoani hapo wanayo taarifa ya zoezi hilo na wamejitokeza kufanya marekebisho ya kasoro hizo.
Alitoa wito kwa waliobaki kufanya haraka ili wasije wakapata usumbufu pindi watakapokwenda Benki kuchukua fedha kukuta hawajaingiziwa chochote kwa sababu ya wao kushindwa kufanyia marekebisho ambayo yaliyokuwa yanasababisha jina lake la hati ya malipo kuwa tofauti na Benki.
Post a Comment